Mwanza. Ule utamaduni wa watu kurejea majumbani ‘kuhesabiwa’ kipindi cha mwishoni mwa mwaka siyo kwa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro pekee, bali hata kwa jamii ya Mkoa wa Mara.
Leo Jumanne, Desemba 24, 2024 katika Kituo cha Mabasi cha Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, watu wenye asili ya Mkoa wa Mara wamejitokeza kutafuta usafiri wa kurejea nyumbani kujumuika na familia kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kutokana na wingi wa abiria, bei ya tiketi kutoka Mwanza kwenda miji ya Bunda, Musoma, Tarime na Sirari imepanda kwa kati ya Sh5,000 hadi Sh7,000 kwa tiketi.
Wakati bei ya tiketi kwa siku za kawaida ni Sh12,000, abiria wanaotoka Mwanza kwenda miji hiyo ya Mkoa wa Mara leo wamenunua tiketi kwa kati ya Sh17,000 hadi Sh20,000.
“Tena tiketi leo hazikatiwi kwenye gari au ofisini kama ilivyozoeleka, wajanja wameshanunua zote kwa Sh12,000 na wao wanauza kwa Sh17,000 hadi Sh20,000. Wanaotaka kusafiri wanazinunua tiketi hizo kwa kuzigombania,” amesema John Okello, mkazi wa Utegi aliyeuziwa tiketi ya kwenda Tarime kwa Sh17,000.
Abiria mwingine aliyekuwa akielekea Wilaya ya Magu, Joseph Mapunda amesema amelazimika kukata tiketi kwa Sh9,000 badala ya Sh3,000 kwa kuwa makondakta walikuwa wanakataa kubeba abiria wanaoshukia njiani.
Ili kuondoa adha ya usafiri kwa wakazi wanaotumia njia ya Mwanza-Musoma, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Mwanza imesema itatoa vibali maalumu kuruhusu magari kusaidia kutatua shida ya usafiri kwa wakazi wa Mara wanaorudi kwao.
“Tumeona kweli kuna changamoto ya abiria, kama mamlaka tutashirikiana na Jeshi la Polisi kuangalia zile njia ambazo uhitaji wake wa abiria ni mdogo kuwapa vibali maalumu kwa ajili ya kusaidia abiria hawa ambao wanaonekana wana changamoto katika njia hii,”amesema Ofisa wa Latra Mkoa wa Mwanza, Stephen Yohana.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema mabasi ya abiria 10 yamekutwa mabovu kati ya mabasi 250 yaliyokaguliwa Desemba 23, 2024 katika stendi ya mabasi Nyamhongolo na Nyegezi.
Amesema mabasi hayo yamekutwa na ubovu sehemu tofauti ikiwamo kwenye matairi na mifumo ya usukani, breki na bodi.
“Sasa haya magari 10 kama ulivyo utaratibu wa sheria za usalama barabarani, kanuni na taratibu zake inaeleza kwamba, mabasi yanapobainika ni mabovu jambo la kwanza ni kuondoa namba za usajili na kuelekeza mara moja mabasi hayo yakafanyiwe matengenezo ndipo yarudi kwa wakaguzi wa magari yakaguliwe,”amesema Mutafungwa.