Dar es Salaam. Wito wa kutangaza amani katika ngazi ya familia, taifa na binafsi, umetolewa ili kuienzi vema kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Kristo.
Kwa mujibu wa Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stephano Musomba, amani ndiyo chachu ya upatanishi miongoni mwa watu.
Askofu Musomba ameyasema hayo leo Jumatatu, Desemba 24, 2024 alipohubiri katika ibada ya mkesha wa sikukuu ya Krismas katika Kanisa la St. Peter, Dar es Salaam.
Amesema kuliko kuhubiri ugomvi na chuki, ni vema watu watangaze amani katika ngazi zote.
“Palipo na amani, pana upendo na ushirikiano na hivyo panakuwa na upatanisho na uvumilivu baina ya sisi kwa sisi,” amesema.
Hata hivyo, amesema kutangaza amani ni miongoni mwa njia sahihi za kuenzi kumbukumbu ya kuzaliwa kwa kristo.
Amesema kuzaliwa kwa kristo kunapaswa kuwatafakarisha watu kuwa leo wapo wakati gani.
Kwa mujibu wa askofu huyo, kwa sasa ni vema kuangalia utandawazi, mioyo na roho za watu ili kuhakikisha zinaendana na matakwa ya kuzaliwa kwa kristo.
“Kila mmoja anapaswa aangalie leo anapoadhimisha Noel yuko wapi,” amesema.
Ameyaelekeza mahubiri yake kwa kuwahoji waumini kuwa, maisha yao ya sasa yanaakisi unyenyekevu kama aliokuwa nao kristo.
“Je, utaweza kukiri kwamba una makosa au umemkosea mwenzako na unaomba msamaha?
“Jamii inapaswa kujiuliza kuzaliwa kwa Kristo ni sehemu ya maisha yao ya kila siku,” amehoji.
Amesema ni wajibu wa waumini kutangaza habari njema kwa wenzao.
Amesisitiza watu hawapaswi kununiana badala yake wawe na amani, kusameheana na kuvumiliana wakati wote.