Bodi ya nyama yatoa tahadhari kwa walaji na wafanyabishara

Dodoma. Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imewataka walaji wa nyama katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kuhakikisha kitoweo hicho kina alama ya mihuri inayoonesha imekaguliwa ili kuepuka madhara yatokanayo na ulaji wa nyama isiyokaguliwa.

Aidha, wafanyabiashara wa nyama wametakiwa kuacha kuchinja mifugo katika machinjio yasiyosajiliwa.

TMB imesisitiza kuwa, wataalamu wake watafanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye mabucha na machinjio kuhakikisha masharti yanatekelezwa ipasavyo.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wamesema idadi ya ng’ombe waliyochinjwa kipindi hiki ni ndogo ikilinganishwa na sikukuu zilizopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Desemba 24, 2025, Kaimu Msajili wa TMB, John Chassama amesema kipindi cha sikukuu mahitaji huongezeka, lakini hilo halipaswi kuwa sababu ya wafanyabiashara kuvunja sheria au kutofuata taratibu za biashara.

Chassama amesisitiza kuwa bidhaa zote zinazouzwa sokoni zinapaswa kufuata taratibu ili ziwe bora na salama kwa walaji.

“Tunajua mahitaji ni makubwa, lakini hatutavumilia njia za mkato kwa nia ya kujinufaisha kinyume cha sheria. Tutafanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye mabucha na machinjio,” amesema.

Aidha, Chassama amewataka walaji kununua nyama katika maeneo rasmi badala ya kununua kwenye vyanzo visivyo rasmi, hata kama bei itakuwa ya chini. Alibainisha kuwa mabucha yaliyoidhinishwa yana cheti cha usajili na vipeperushi vya kusimamia biashara ya nyama.

Chassama amesema adhabu kwa wauzaji wa nyama isiyokaguliwa ni pamoja na kuteketeza bidhaa husika, kulipa faini hadi Sh1 milioni na kwa wanaorudia makosa, kunyang’anywa leseni za biashara.

Naye Ofisa Ukaguzi wa TMB, Martin Mkindi amesema nyama iliyokaguliwa huwa na mihuri katika maeneo muhimu kama mikono, miguu, na mbavu.

“Wauzaji wameelekezwa kuhakikisha sehemu zilizo na mihuri kuuza mwisho ili kuendelea kuthibitisha ubora hadi inapomfikia mlaji,” amesema.

Mkindi ameeleza kuwa ulaji wa nyama isiyokaguliwa unaweza kusababisha magonjwa kama kifua kikuu, minyoo, tegu, brucellosis na uwepo wa mabaki ya dawa mwilini.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nyama Mkoa wa Dodoma, Musa Yohana amesema idadi ya mifugo waliyochinjwa mwaka huu ni ndogo ikilinganishwa na mwaka uliopita. Amesema machinjio ya Dodoma kawaida huchinja ng’ombe 200 kwa siku katika msimu wa sikukuu, lakini mwaka huu ni ng’ombe 150 pekee.

Yohana amesema kuwa, hali hiyo imefanya bei ya nyama kuongezeka, ambapo kilo moja inauzwa kuanzia Sh12,000.

Amesema ng’ombe mwenye uzito wa kilo 150 anauzwa hadi Sh2 milioni.

Kwa mujibu wa TMB, kuna mabucha 5,739 yaliyosajiliwa nchini, yakiwamo ya daraja la juu 21, daraja la kati 86, na daraja la kawaida 5,632. Aidha, magari ya kusafirisha nyama yaliyosajiliwa ni 302.

Kwa upande wa mabucha ya nyama pori, hadi sasa yamesajiliwa 11 na manne yapo Kanda ya Kati, matano Nyanda za Juu Kusini na mawili Mashariki.

Related Posts