NYOTA wa zamani wa Yanga, Simba na Azam FC, Ivo Mapunda amesema kwa sasa anaachana na soka kwa muda ili apate nafasi ya kurejea tena darasani kwa ajili ya kuongeza elimu, itakayomfanya kupata sifa ya kuzifundisha timu kutoka Ligi Kuu Bara.
Ivo ametoa kauli hiyo baada ya kuachana na kikosi cha Songea United cha mkoani Ruvuma kinachoshiriki Championship, ikiwa ni muda mchache baada ya kipa huyo wa zamani kuamua kutangaza uamuzi huo, ili akapate fursa ya kujiendeleza kimasomo.
“Kwa sasa nina leseni ‘B’ ya CAF ambayo hainiwezeshi kupata nafasi ya kufundisha timu za Ligi Kuu Bara, nimeona ni muda mzuri kwangu kwenda kusoma tena na nimeomba nchi mbili za Marekani na Poland hivyo, nasubiria majibu yatoke,” alisema.
Kocha huyo aliyeiongoza Songea katika michezo 12, akishinda mitano, sare mitano na kupoteza miwili, aliushukuru uongozi wa timu hiyo kwa kumuamini katika majukumu hayo, huku akiiombea ifanye vizuri ili ipande Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Kitendo cha Ivo kujiweka pembeni ili kwenda kujiendeleza na masomo kikawafanya viongozi wa kikosi hicho kumsaka mrithi wake, huku Mwanaspoti likitambua wamefikia makubaliano na aliyekuwa Kocha wa Stand United, Meja Mstaafu Abdul Mingange.