WAKATI leo Simba ikiwa mwenyeji wa JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, kipa namba moja wa timu hiyo, Moussa Camara ameonekana kuweka mizizi kwenye nafasi yake.
Simba iliyocheza mechi 13 za ligi ikiongoza msimamo kwa pointi 34, msimu huu imetumia wachezaji 25 tofauti kupambania pointi.
Kati ya wachezaji hao 25, Camara pekee ndiye aliyetumika kwa dakika zote 1,170 jambo linalodhihirisha kwamba Kocha Fadlu Davids hajapata mbadala wake.
Ukimuondoa Camara, hakuna mchezaji mwingine aliyecheza mechi zote jambo ambalo limefanya kila mmoja kutokuwa na nafasi ya uhakika kikosini hadi sasa.
Wakati kipa huyo akicheza mechi zote 13 bila kupumzika, kuna nyota sita hawajaonja hata dakika moja.
Wachezaji hao ni makipa Ally Salim, Ayoub Lakred, Hussein Abel, Aishi Manula na beki David Kameta.
Nyuma ya Camara, mchezaji aliyecheza dakika nyingi ingawa sio mechi zote ni Che Malone aliyetumika kwa dakika 1,080.
Kwa upande mwingine, mchezaji aliyepata dakika chache zaidi za kucheza ni Saleh Karabaka akitumika kwa dakika tisa akifuatiwa na Hussein Kazi aliyecheza dakika 10. Hao wote wamecheza mechi moja pekee.
Wengine waliocheza na muda waliotumika katika mabao ni Kelvin Kijili (dk 130), Shomari Kapombe (957), Abdulrazack Hamza (620), Valentine Nouma (365), Mohamed Hussein (805), Chamou Karaboue (642), Mzamiru Yassin (279), Awesu Awesu (544), Debora Mavambo (774), Edwin Balua (317), Augustine Okejepha (510), Ladack Chasambi (459), Joshua Mutale (407), Fabrice Ngoma (667), Omary Omary (55), Yusuph Kagoma (158), Jean Charles Ahoua (832), Valentino Mashaka (68), Steven Mukwala (509), Kibu Denis (687), Leonel Ateba (667) na Elie Mpanzu (57) aliyesajiliwa dirisha dogo msimu huu.
Kitendo cha Fadlu kubadilisha kikosi mara kwa mara huku akionekana kuendelea kufanya vizuri, kimekuwa kikiwapa wakati mgumu wapinzani wake kushindwa kumsoma jambo linalompa faida.
Kuhusu mabadiliko ya kikosi, Fadlu alisema: “Mechi mfululizo zinatulazimu kumtumia kila mchezaji ili kuondoa hali ya uchovu kwa sababu ukiangalia ndani ya muda mfupi unatakiwa kucheza. Wachezaji wanachoka, hivyo kufanya mabadiliko pia inawaepusha na majeraha.”
Ushindi wa mechi saba mfululizo wa Simba, ni miongoni mwa mambo yanayoifanya iingie na morali ya juu leo dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam. Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 34, wanahitaji ushindi ili kujikita kileleni.
Fadlu anajivunia kiwango cha timu yake iliyofunga mabao 13 katika michezo mitano iliyopita dhidi ya Mashujaa (1-0), KMC (4-0), Pamba Jiji (1-0), KenGold (2-0) na Kagera Sugar (5-2).
Kwa upande wa JKT Tanzania iliyopo nafasi ya nane kwa pointi 19, inahitaji ushindi ili kuendelea kubaki katika nafasi za juu. Kwa sasa ipo nafasi ya nane. Timu hizo hazijapoteza katika michezo mitano iliyopita, jambo linaloongeza mvuto wa mchezo huu. JKT Tanzania chini ya kocha Ahmad Ally wameonyesha uimara katika ulinzi, kwani hawajaruhusu bao katika michezo hiyo. Hata hivyo, changamoto kubwa kwao ni safu ya ushambuliaji, ambapo licha ya kuwa na viungo wenye uwezo kama Said Dilunga na mshambuliaji mzoefu John Bocco, bado wanashindwa kutengeneza nafasi za kutosha za kufunga.
“Katika michezo yetu ya hivi karibuni tumeonyesha uwezo mkubwa kulinda na tunahitaji kuboresha zaidi safu ya ushambuliaji ili kupata mabao. Tuko tayari kwa mapambano na tunaamini tutapata matokeo chanya,” alisema Ahmad.
Simba, ikiwa na wachezaji kama Ahoua, Chasambi na Mpanzu inaonekana kuwa na safu imara ya ushambuliaji. Ahoua mwenye mabao sita katika ligi atakuwa na kazi ya kuhakikisha Simba inapata matokeo mazuri. Chasambi alitoa asisti tatu katika ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar juzi, huku Mpanzu akionyesha kuwa ni mchezaji muhimu katika mfumo wa Fadlu.
Swali kubwa linabaki kuhusu nani atacheza eneo la mwisho la ushambuliaji la Simba kwani Mukwala na Ateba wamekuwa na viwango vinavyolingana, ambapo Ateba alifunga mabao mawili dhidi ya KenGold na Mukwala akifunga idadi kama hiyo dhidi ya Kagera Sugar. Hii inampa Fadlu changamoto ya kuchagua wachezaji wa kuanzisha kwenye mchezo.
“JKT Tanzania ni timu ngumu wameonyesha uwezo mkubwa katika ulinzi na hivyo tunajua itakuwa mechi ya changamoto,” alisema Fadlu.
“Lengo letu ni kushinda ili kuendelea kujivunia kilele cha msimamo wa ligi. Tunahitaji kuendelea kuwa imara kwenye ushambuliaji, lakini pia kuhakikisha kuwa tunatunza umakini kwenye ulinzi wetu. Tumewaandaa wachezaji vizuri na tunataka kuwatia furaha mashabiki wetu kwa ushindi wa Krismasi.”
Rekodi zinaonyesha kuwa Simba imeshinda mechi nne mfululizo dhidi ya JKT Tanzania katika misimu miwili iliyopita. Msimu uliopita, Simba ilishinda mechi zote mbili dhidi ya JKT Tanzania bila kuruhusu bao, ambapo ilishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza na 2-0 katika mchezo mwingine. Hata hivyo, JKT Tanzania imeshinda mara moja tu dhidi ya Simba, na ushindi wao wa pekee dhidi ya Mnyama ulifanyika Februari 7, 2020, kwa bao 1-0 lililofungwa na Adam Adam, ambaye sasa anachezea Azam FC.