MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube ameonekana kufanya vizuri zaidi katika kipindi cha muda mfupi chini ya kocha Sead Ramovic tofauti na ilivyokuwa wakati wa Miguel Gamondi.
Dube aliyetua Yanga msimu huu akitokea Azam, takwimu zinaonyesha amehusika kwenye mabao mengi zaidi akicheza mechi chache chini ya Ramovic baada ya kupita kipindi kirefu bila ya kufunga.
Ramovic ambaye alitambulishwa ndani ya Yanga Novemba 15 mwaka huu kuchukua nafasi ya Gamondi, ameiongoza timu hiyo kucheza mechi sita za michuano tofauti akishinda tatu za Ligi Kuu, sare moja na kupoteza mbili zote zikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Gamondi aliiongoza Yanga kucheza mechi kumi za ligi, mbili Ngao ya Jamii na nne Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kitendo cha Dube kufunga mabao manne kwenye ligi katika mechi mbili zilizopita ikiwamo hat trick, yamewafanya mashabiki wa timu hiyo kuanza kuona straika wao hivi sasa amejipata. Si kufunga tu, hata kutoa asisti yupo vizuri.
Tangu awe chini ya Ramovic, Dube ameonekana kufanya vizuri zaidi tofauti na wakati wa Miguel Gamondi.
Takwimu za kwenye ligi zinaonyesha kwamba, Dube chini ya Gamondi alicheza mechi tisa bila ya kufunga bao zaidi ya kutoa asisti moja katika mchezo wa mwisho ambao Gamondi aliisimamia timu hiyo.
Ukiweka kando Ligi Kuu, Dube alifunga bao moja na asisti moja katika michuano ya Ngao ya Jamii akiiwezesha timu yake kubeba ubingwa.
Kimataifa wakati wa Gamondi, Dube alifunga mabao matatu yote hatua ya awali na asisti mbili, hivyo kumfanya kuwa na jumla ya mabao manne na asisti nne chini ya Gamondi kwenye mechi 15 za mashindano tofauti.
Katika mechi sita za Ramovic, Dube amehusika kwenye mabao sita akiwa na wastani wa kuhusika na mabao kila mechi kutokana na kufunga matano na asisti moja huku akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu kupiga hat trick.
Takwimu za jumla zinaonyesha kwamba, Dube amecheza mechi 21 kati ya 22 za michuano yote tangu atue Yanga msimu huu akitokea Azam akifanikiwa kufunga mabao manane na asisti tano. Katika mabao hayo manane, matano kipindi cha Ramovic na matatu wakati wa Gamondi.
Kimataifa amecheza mechi zote saba tangu hatua ya awali kwa dakika 306. Upande wa ligi, dakika zake ni 626 akicheza mechi 12 kati ya 13, amekosa moja pekee dhidi ya JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic alisema Dube amerudisha hali ya kujiamini ambayo ilipotea hapo awali.
Ramovic alisema yeye pamoja na wenzake wa benchi la ufundi walichukua hatua za kumsaidia kisaikolojia nyota huyo Mzibabwe kwa kuzungumza naye mara kwa mara hadi kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
“Dube ni mshambuliaji mzuri ndio maana tupo naye hapa, tangu nimefika alikuwa hajafunga bao kwenye ligi lakini ilikuwa inaumiza kumuona kwa kuwa anapambana sana akiwa mazoezini na hata uwanjani ,” alisema Ramovic.
“Kuna nyakati tulilazimika kukaa naye na kumjenga kisaikolojia tukimsihi asikate tamaa kwani kwenye soka kwa washambuliaji ukame kama huu wa mabao unatokea lakini haitakiwi kukata tamaa. Tulipambana kuiweka sawa saikolojia yake na sasa anaendelea sawa.
Ramovic alisema anavutiwa na ushirikiano wa wachezaji wote kwenye kikosi hatua ambayo itaendelea kuzalisha mabao mengi zaidi endapo watatulia na kutumia nafasi wanazotengeneza.
“Tunatakiwa kuendelea kucheza kama timu kama hivi, unaona namna wachezaji wanavyoshirikiana, unaweza kuona Dube anamtengenezea nafasi mwenzake na Clement (Mzize) anamtengenezea nafasi mwenzake, kitu muhimu hapa ni kuiweka timu mbele.
“Tunaweza kufunga mabao mengi zaidi kama hali ya namna hii ikiendelea hivi, tunatakiwa kuendelea kutumia nafasi kwa wingi kwenye kila mchezo,” alisema Ramovic.
Wakati Ramovic akiyasema hayo, hivi karibuni zilisambaa picha katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha Dube akiombewa na mmoja wa wachungaji ambapo siku chache baadaye akamaliza ukame wa mabao kwa kufunga dhidi ya TP Mazembe kabla ya kupiga hat trick dhidi ya Mashujaa.
Ukilinganisha kipindi cha Gamondi na Ramovic ndani ya ligi, utaona namna ambavyo timu imekuwa na mabadiliko makubwa sana ya kiuchezaji licha ya kwamba hapo awali ilionekana ni kama haichezi kitimu.
Gamondi ambaye alitamba na kikosi chake kwenye mechi za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufunga mabao 17 katika mechi nne na kufuzu makundi bila ya kuruhusu bao, hali ilibadilika kwenye ligi.
Hadi anaondoka Yanga, Gamondi aliiongoza timu hiyo katika mechi kumi ikishinda nane na kupoteza mbili huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne.
Ramovic katika mechi tatu za ligi, timu hiyo imefunga mabao tisa ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi.
Ramovic alianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo ugenini, kisha akashinda 3-2 nyumbani dhidi ya Mashujaa na akaichapa Tanzania Prisons 4-0.
Ukilinganisha na Gamondi, mechi tatu za kwanza msimu huu kwenye ligi naye alishinda zote, lakini mabao yalikuwa machache akifunga manne huku nyavu zake zikiwa hazijatikiswa wakati tayari Ramovic kikosi chake kimeruhusu mabao mawili.
Wakati wa Gamondi, ilionekana baadhi ya wachezaji ndiyo wenye uhakika wa kucheza huku wengine wakitupwa nje.
Wachezaji kama Farid Mussa, Kibwana Shomari na Aboutwalib Mshery hawakuwa wakipewa nafasi lakini sasa wanacheza.
Ramovic anachofanya ni kutoa nafasi kwa kila mmoja ambaye yupo fiti kuonyesha uwezo jambo ambalo mtu akishindwa ni juu ya mchezaji mwenyewe.
Katika mechi tatu za ligi alianza kwa kumpa nafasi Khomeiny Abubakar dhidi ya Namungo ambaye ulikuwa ni mchezo wa pili kucheza msimu huu baada ya kuikabili Coastal Union. Lakini pia Khomeiny akadaka dhidi ya Mashujaa.
Katika mchezo wa Mashujaa, pia ilikuwa ni mara ya kwanza kumshuhudia Kibwana Shomari akicheza msimu huu mechi yake ya kwanza tena akitumika kwa dakika 79 kabla ya juzi dhidi ya Tanzania Prisons kumaliza zote 90.
Farid Mussa naye alirejea uwanjani mara ya kwanza dhidi ya Mashujaa akiingia dakika ya 79 huku juzi dhidi ya Tanzania Prisons akianza kikosi cha kwanza na kucheza kwa dakika 65. Katika mchezo huo Mshery alidaka mara ya kwanza msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kibwana alisema anafurahi kupata nafasi nyingine ya kuitumikia Yanga baada ya kukaa nje kwa muda mrefu huku akiweka wazi kuwa bado anajitafuta kujiweka kwenye hali ya utimamu na ataendelea kuipambania nafasi hiyo bila kuchoka.
“Kuaminiwa kwa kucheza dakika nyingi mchezo wa kwanza baada ya kukaa nje kwa muda mrefu sio rahisi, nashukuru Mungu nimepokewa na kuaminiwa. Naomba hili liendelee ili kunijengea kujiamini zaidi,” alisema.