Kilio wanaopasua la saba kupangiwa shule za kata

Desemba 16, 2024, Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, alitangaza orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za Serikali mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, wanafunzi 974,332 walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2025.

Kati ya hao, ni 809 tu waliochaguliwa kwenye shule za bweni za vipaji maalum. Wengine wengi, wakiwemo wanafunzi wenye alama za juu kutoka shule binafsi, walipangiwa shule za kutwa za kata.

 Hata hivyo, uchaguzi huo umepokelewa kwa hisia hasi hususan kutoka kwa wazazi wa watoto waliofaulu vizuri kutoka shule binafsi.

 Kilio chao ni mshangao wa kuona wanafuzi waliofanya vizuri kutoka shule hizo wakikosa nafasi katika shule ama za vipaji maalum au zinazoelezwa kuwa na afadhali kubwa kitaaluma.

Matokeo yake ‘vipanga’ wengi kutoka shule hizo wamepangiwa shule za kata ambazo bado zinanyooshewa kidole kwa kutofanya vizuri kitaaluma.

Baada ya uchaguzi huo, mitandaoni hakukuwa shwari. Kulikuwa na mjadala mzito wa wazazi wa shule mbalimbali kuhusu vigezo vinavyotumika kupanga wanafunzi.

Kilio chao ni kushangaa watoto wao waliopata ufaulu wa daraja A kupangiwa shule za kata za hasa zilizo jirani na shule walizosoma watoto wao.

Mzazi, Clara Makame anayeishi jijini Dar es Salaam, anasimulia kwa masikitiko jinsi binti yake aliyepata alama A zote katika shule ya Bethel Mission alivyopangwa katika shule ya sekondari ya kata ya Yusuf Makamba.

“Mtoto wangu na wenzake wamefaulu kwa bidii. Bethel Mission ilihakikisha watoto wanaandaliwa vizuri kwa ajili ya mitihani. Tulijitahidi kama wazazi kuwalipia ada na kuhakikisha wanapata mazingira mazuri ya kujifunza. Lakini sasa, tunashangaa kwa nini wanapelekwa kwenye shule za kata, ambapo hata miundombinu ni changamoto kubwa,” anasema.

Mzazi mwingine, Gabriel Nyalali anayeishi mkoani Arusha anasema: “Mtoto wangu alisoma shule ya binafsi na kufaulu kwa kiwango cha juu, lakini bado amepelekwa shule ya kata iliyo na changamoto nyingi za miundombinu na walimu wasio na motisha. Hii ni njia ya wazi ya kuwakatisha watoto tamaa. Wazazi tunaona juhudi zetu zikififishwa na mfumo wa ovyo.”

Naye, Fatuma Mbasha kutoka Shinyanga anaongeza kusema: “Hii hali inakatisha tamaa. Mtoto aliyepata alama A zote anapangwa shule moja na yule aliyepata wastani wa C. Kwa nini tusijifunze kutoka nchi kama Ujerumani au Uingereza ambako wanafunzi wanapangiwa shule kulingana na uwezo wao na viwango vya ufaulu?”

Musa Kimario wa Dodoma anahoji: ‘’Inakuwaje mwanafunzi wa darasa la saba aliyepata A zote anapelekwa shule za kata zilizo na changamoto tele, ilhali shule bora za kitaifa kama Mzumbe na Kilakala zinaonekana kuwa chaguo la kipekee kwa watoto wa tabaka fulani?’’

Wazazi hawa na wengineo wanahoji kwa nini wanafunzi waliofaulu kwa alama za juu hawapangiwi shule bora za kitaifa kama Mzumbe, Kilakala, au Kibaha, ambazo zimekuwa na rekodi nzuri ya ufaulu kitaaluma.

Wakati wazazi wengi wakitamani watoto wao kupangiwa shule za umma zenye ahueni, Mwalimu mstaafu Bakari Kheri ana mtazamo tofauti..Anasema hoja ya wazazi hao ni mwendelezo wa alichokiita kubagua watoto wanaosoma shule za msingi za umma.

Anasema hata watoto wanaosoma shule za umma nao wana haki ya kusoma shule bora wanapoingia sekondari.

“Inashangaza mno na hii kwangu ni ishara ya ubinafsi. Ukishasema kila aliyefaulu vizuri aende shule bora, maana yake unasema watakaosoma huko watakuwa ni wanafunzi kutoka shule binafsi ambazo ndizo utaona darasa zima lina ufaulu wa daraja A. Sasa kwa nchi nzima inamaanisha shule bora za umma zitakuwa na watoto wanaotoka shule binafsi. Hawa wa shule zetu waende wapi? ” anahoji.

Anasema kama wazazi hao wanadai wanafunzi shule za binafsi wanatengwa katika uchaguzi, kinyume chake ikifanyika kwa wao kuchaguliwa shule bora, huo ndio ujenzi mbaya zaidi wa matabaka katika nchi.

“Halafu hawa wazazi wanaolalamika wanasimamia wapi, watoto wao wanapofika kidato cha nne kwenda cha tano, Serikali pia inawatenga? Huko mbona hatusikii kelele? ” anaeleza na kutaka Serikali iachwe kufanya kazi yake kwa kuwa inajua inachokifanya katika uchaguzi wa wanafunzi.

Tujifunze mataifa mengine

Mfumo wa elimu wa nchi nyingi za Magharibi, unasisitiza uwiano wa kipekee kati ya ufaulu na fursa.

Kwa mfano, nchini Finland, wanafunzi wenye ufaulu wa juu hupatiwa nafasi katika shule zenye mitalaa ya ubora wa juu zaidi, huku wale wenye changamoto wakisaidiwa zaidi ili kufikia viwango vinavyotakiwa. Mfumo kama huu unahakikisha kila mwanafunzi anapata fursa sawa kulingana na juhudi zake.

Nayo Uganda imeboresha mfumo wake wa upangaji kwa kuzingatia uwezo wa mwanafunzi na kuhakikisha kuwa shule zote za Serikali zinatoa elimu bora sawa.

‘’Hatua hii imepunguza mwanya kati ya shule za serikali na binafsi, na hivyo kuimarisha mshikamano wa kijamii, ‘’ anasema Dk Sarah Nkondo wa Uganda.

Dk Nkondo na Sarah Nkondo na Profesa Themba Ndaba wa Afrika

Kusini, wameeleza kuwa kutokuwepo kwa mfumo wa uwiano katika elimu, kunajenga tabaka la kijamii linalosababisha tofauti kubwa za kiuchumi na kiutamaduni miongoni mwa watu.

Kwa mfano, Afrika Kusini imeweza kuondoa sehemu kubwa ya matabaka haya kwa kuhakikisha kuwa shule zote, bila kujali mahali zilipo, zinapewa rasilimali sawa.

Hata hivyo, kwa Tanzania bado hali ni mbaya. Kinachoonekana ni kuwapo kwa jamii iliyogawanyika, ambapo wanafunzi wa shule za umma wanajikuta wakihangaika na changamoto za miundombinu duni, ukosefu wa walimu wa kutosha na vifaa vya kufundishia visivyokidhi mahitaji.

Kuibuka kwa shule za serikali zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, kumeongeza mwelekeo wa upendeleo kwa shule hizi, huku shule za umma zinazotumia Kiswahili zikionekana kuwa chaguo la mwisho.

Pamoja na Serikali ikijitahidi kuendeleza elimu ya msingi bila ada, tofauti kati ya shule za umma na zile za binafsi imeendelea kuwa kubwa.

Tamisemi imekuwa ikisisitiza kuwa wanafunzi wote wamepangwa kwa kuzingatia viwango vya

ufaulu na kwamba lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma. Hata hivyo, maelezo haya hayawaridhishi wazazi wengi.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Juma Kasekwa, anasema kuwa mfumo huu wa

upangaji unahitaji maboresho makubwa. “Kwa sasa, hatuwezi kusema kwamba tuna mfumo wa haki. Ufaulu wa juu unapaswa kuthaminiwa kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi kwenye shule zinazostahili. Bila hivyo, hatuwezi kuwahamasisha watoto wetu kusoma kwa bidii,” anasema.

Nao wadau wa elimu wanatoa mapendekezo kadhaa, ikiwamo Serikali kuweka mfumo wa wazi wa upangaji unaozingatia ufaulu wa mwanafunzi bila kujali shule alikotoka. Pili, wanasema shule za kata zinahitaji kuboreshwa ili ziweze kushindana kwa ubora na shule za binafsi.

Kwa sasa, wazazi wengi wanabaki na maswali mengi yasiyo na majibu. Lakini jambo moja ni wazi kuwa mfumo wa sasa wa upangaji wa wanafunzi wa sekondari unahitaji mabadiliko makubwa ili kuleta haki na usawa kwa kila mwanafunzi, bila kujali shule alikotoka.

Wadau wanaishauri Serikali kutafuta mbinu za kufanikisha usawa katika kugawa wanafunzi,

huku ikiimarisha shule za umma ili ziweze kushindana na zile za binafsi. Hii itasaidia kupunguza tofauti za kijamii na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts