Dar es Salaam. Wakristo wametakiwa kutafakari na kutenda yaliyo mema ili kuyaweka maisha yao na Taifa lao katika nuru, wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Krismas.
Imeelezwa kuwa, nuru huongoza maisha ya mtu, huleta furaha, amani na upendo na kwamba Taifa lenye nuru hujawa mafanikio.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Desemba 24, 2024 na Msaidizi wa Askofu Kanisa Kuu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) jijini Dar es Salaam, Chediel Lwiza wakati akiongoza ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi katika Kanisa la Azania Front.
Amesema maneno hayo, alipokuwa akihubiri kutoka kitabu cha Mathayo Mtakatifu sura ya kwanza kinachoelezea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
“Tunapokumbuka namna Yesu Kristo alivyozaliwa alileta nuru. Hii tuitafakari na tukumbuke nuru inaliongoza Taifa na kuleta furaha kwenye Taifa, haina tofauti na kipindi ambacho tunafurahia mavuno kwa sababu yapo mambo mengi anayotutendea,” amesema.
Lwiza amesema katika Taifa ambalo hakuna matendo mema, badala ya kuona nuru huona mauti, “badala ya kuona uhai wanaona mauti, badala ya kuona uzima wanaona mauti, badala ya kuona amani na furaha wanaona mauti.”
“Lakini ndani yao kuna giza limeingia. Tunataka nuru kuu kwenye maisha yetu, kazi zetu na amani yetu,” amesema.
Akitafakari neno hilo, amesema katika lugha ya malaika imesema,”nuru kuu atakaa na wewe Emanuel,” akifafanua kwamba hiyo ni lugha ya Kimungu.
“Lugha hii ni ya Kimungu inaweza ikakuchanganya sana ukitumia maarifa yako mwenyewe, ukaiweka imani pembeni unaweza ukachanganyikiwa.
“Katika kitabu cha Mathayo ameeleza vizuri kwamba Yusuf alikuwa amelala usingizi mstari wa 24 alipoamka katika usingizi, akafanya kama malaika wa bwana alivyomwagiza,” amesema Lwiza.
Misa hiyo imetumika kuwakumbusha Wakristo hao namna Yesu alivyozaliwa kwa igizo la dakika 45.
Misa hii pia imehudhuriwa na Askofu Alex Malasusa.