Bayrou mwanasiasa wa mrengo wa kati anatumai kuwa baraza lake la jipya la mawaziri linalojumuisha mawaziri wa zamani na watumishi waandamazi wa serikali litasaidia kusimamia kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2025 na hivyo kuondoa mkwamo ambao ulikuwa unatishia kuzidisha mzozo ndani ya nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya.
Majina ya baraza jipya la mawaziri yalisomwa na mkuu wa wafanyikazi wa ikulu Alexis Kohler.
Macron amemteua aliyekuwa Waziri mkuu Elisabeth Borne mwenye umri wa miaka 63 kuwa Waziri wa elimu katika baraza jipya la mawaziri.
Soma pia: Rais Macron amteua Francois Bayrou kuwa Waziri Mkuu mpya
Waziri mkuu mwengine wa zamani Manuel Valls mwenye umri wa miaka 62, ameteuliwa kuwa Waziri wa maeneo ya nje yalio chini ya usimamizi wa Ufaransa huku aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani Gerald Darmanin akiteuliwa kuongoza wizara ya sheria.
Waziri wa ulinzi Sebastian Lecornu na Waziri wa mambo ya nje Jean-Noel Barrot walibaki katika nafasi zao mtawalia.
Lecornu, mwenye umri wa miaka 38 na mshirika wa karibu wa Macron, amehudumu katika kila serikali tangu Macron alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kama rais mnamo mwaka 2017.
Wachambuzi wanatabiri kuwa Bayrou atakumbwa na wakati mgumu
Waziri wa mambo ya ndani mhafidhina Bruno Retailleau, ambaye ameahidi kupambana na uhamiaji haramu na Waziri wa utamaduni mwenye kuegemea siasa za mrengo wa kulia Rachida Dati pia walibaki katika nafasi zao za uwaziri.
Kibarua kigumu kinaonekana kumuangukia Eric Lombard. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 66 ambaye ni mkuu wa taasisi ya uwekezaji wa sekta ya umma CDC, ameteuliwa kuongoza wizara ya fedha. Atafanya kazi sako kwa bako na Amelie de Montchalin aliyeteuliwa kama Waziri wa bajeti.
Soma pia: Wanasiasa wa Ufaransa wanakutana kujadili serikali mpya
Bayrou ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, “najivunia sana timu hii mpya tuliyoitangaza jioni hii.” Ameongeza kuwa, serikali yake yenye uzoefu inapania kurudisha tena imani.
Ujumuishaji wa mawaziri wakuu wawili wa zamani ndani ya baraza jipya la mawaziri kumetafsiriwa kama nia ya Macron ya kuwepo kwa serikali imara ambayo haitakumbwa na hatma kama iliyomkuta mtangulizi wa Bayrou, Michel Barnier, aliyeondolewa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye kufuatia mzozo kuhusu bajeti ya kubana matumizi.
Bayrou alitarajia kuwajumuisha wanasiasa kutoka mirengo yote ya kisiasa, kushoto, kulia na kati ili kuilinda serikali yake juu ya uwezekano wa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani nayo japo baraza lake la mawaziri halijumuishi mwanasiasa yeyote kutoka muungano wa mrengo wa kushoto wa New Popular Front ambao ulishinda viti vingi zaidi katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge.
Tangazo hilo la baraza jipya la mawaziri limetolewa wakati Ufaransa ikiomboleza wahanga wa kimbunga Chido kilichoipiga kisiwa cha Mayotte.