Madenge aachiwa msala Biashara Utd

HALI imezidi kuwa mbaya zaidi kwa Biashara United ya mkoani Mara baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mussa Rashid kuondoka kutokana na ukata unaoikabili, ikiwa ni siku chache baada ya mastaa wengine wanne pia kutimka kikosini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mussa alisema kwa sasa amejiweka pembeni na timu hiyo na asingependa kuzungumzia jambo lolote huku akitaka waulizwe viongozi ndio wenye majibu, japo hana shida na mtu yeyote na amefurahia kufanya nao kazi.

“Nimeamua kwanza kupumzika hadi nitakapoamua vinginevyo, siwezi kusema moja kwa moja kama nimeondoka ila wakiulizwa viongozi naamini watakuwa na majibu sahihi juu ya jambo hilo, itoshe kusema nawaheshimu kutokana na ukarimu wao kwangu.”

Kaimu Mwenyekiti wa Biashara, Augustine Mgendi akizungumzia jambo hilo alisema ni kweli Mussa ameondoka bila ya kutoweka sababu wazi, huku akieleza kikosi hicho kwa sasa kiko chini ya aliyekuwa Kocha na Mkurugenzi wa ufundi, Omary Madenge.

Mussa ambaye ni kocha wa zamani wa timu za African Sports na Green Warriors alijiunga na timu hiyo akichukua nafasi ya Henry Mkanwa, huku kikosi hicho kikipambana kwa ajili ya kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2021-2022.

Related Posts