Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza Januari 2025 kuanza utaratibu wa kufanya biashara kwa saa 24 eneo la Kariakoo, wafanyabiashara wametaja mambo matano ambayo yakifanyika mchakato huo utafanikiwa.
Mambo hayo ni ulinzi na usalama, changamoto za chemba za maji taka zifanyiwe kazi, umeme wa uhakika, benki kuongeza muda wa kutoa huduma na njia zilizopo maeneo ya Kariakoo jijini hapa kupitika kwa urahisi.
Jana Jumatatu Desemba 23, 2024 akitoa salamu za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema jiji linajiandaa kufanya biashara kwa saa 24 na kamati maalumu imeshaundwa kusimamia jambo hilo.
“Kuanzia Januari 2025 tutafanya sherehe kubwa ya kuzindua rasmi utaratibu wa kufanya biashara kwa saa 24. Tutawataka kila mkuu wa wilaya na mkurugenzi kuainisha eneo litakalofanya biashara saa 24.
“Upande wa Kariakoo tumeanza mchakato wa kununua kamera na tutaanza mchakato wa kununua baadhi ya vifaa vitakavyosaidia ikiwemo taa. Tayari tumeshakaa na wamiliki wa benki na taasisi nyingine ili suala la kufungua biashara saa 24 liwe rasmi,” amesema.
Chalamila amesema kuna baadhi ya sheria zinakinzana, akieleza katika Jiji la Dar es Salaam, zipo zinazoeleza baadhi ya biashara zifungwe saa sita usiku.
“Sasa utaratibu huo kwa Dar es Salaam tunaanza kukomesha taratibu kwa sababu mkoa huu una miundombinu inayoruhusu kufanya biashara saa 24,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 24, 2025 kuhusu uamuzi huo wa Serikali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi amesema wamejiandaa na hatua hiyo kwa sababu itaongeza mzunguko wa fedha.
“Tunachoomba kifanyiwe kazi ni umeme ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara hasa mchana, tungependa kupata uhakika kutoka Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kuhusu nishati hii.
“Pia Dawasa (Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam) wawe na timu maalumu ya kushughulikia changamoto za chemba eneo la Kariakoo. Jambo lingine, njia ziwe wazi zifunguke ili kutoa urahisi wa watu kupita bila usumbufu hasa usiku,” amesema Mushi.
Amewaomba wenye benki kuongeza muda wa kutoa huduma tofauti na sasa, kwani baadhi zinafunga kati ya saa 10 jioni na saa moja usiku.
Mushi amesema kwa hatua ya mwanzo wafanyabiashara watatoa huduma hadi saa tano au sita usiku, badala ya saa moja usiku.
“Kwa kuwa tutafanya kazi hadi usiku, basi benki nazo zisogeze muda kidogo, lakini pia Jeshi la Polisi liongeze doria ili kuimarisha usalama muda wote kwa ushirikiano na Serikali za mitaa ya Kariakoo,” amesema.
Kuhusu ulinzi na usalama, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne ameliambia Mwananchi kuwa limeshajiandaa tangu mwaka 2023.
“Siku nyingi tumejipanga ndiyo maana unaona Kariakoo ipo shwari, polisi imeshajipanga kuimarisha ulinzi na usalama kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tumeshaandaa mazingira na kufanya maandalizi kuhusu suala hili,” amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary amesema wamejipanga kutoa ulinzi na usalama kwa kuimarisha vikosi vya ulinzi shirikishi kwa ushirikiano na wafanyabiashara ili kuleta ustawi.
“Tutakaa pia na wafanyabiashara kuangalia namna bora ya kubadilisha fedha kwa mitandao badala ya kutumia taslimu. Tumeshaanza kufanya nao kikao, baada ya wao kutoka kwenye kikao cha mkuu wa mkoa,” amesema.