KATIKA kuhakikisha Mbeya Kwanza inafanya vizuri ili kutimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, mabosi wa timu hiyo wameanza kuimarisha kikosi hicho kwenye dirisha hili dogo la usajili, baada ya kupata saini ya nyota watatu wapya.
Nyota wapya waliosajiliwa na timu hiyo yenye makazi yake mkoani Mtwara ni beki wa kati, Hussein Abdullah kutokea Mbuni na mawinga, Jamal Mtegeta kutoka Pamba na Oscar Tarimo aliyekuwa anakichezea kikosi cha Maafande wa Polisi Tanzania.
Akizungumzia maingizo hayo Kocha wa Mbeya Kwanza, Emmanuel Masawe alisema wachezaji hao watakuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na uwezo wao, huku akiweka wazi wataendelea kuboresha maeneo mbalimbali kutokana na mahitaji yao.
“Ndiyo kwanza tumeanza na hao watatu lakini tutaendelea kuangalia uwezekano tena wa kuongeza wengine hususani eneo letu la ushambuliaji, lengo ni kutengeneza balansi ya timu katika maeneo yote ili kuendana na ushindani wa Ligi msimu huu.”
Masawe anapigania timu hiyo ili iweze kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushiriki msimu wa 2021-2022 kisha kushuka daraja, huku akikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Mtibwa Sugar, Geita Gold na Stand United zilizokuwa juu yake.