Dar es Salaam. Baada ya vigogo wanne wa Chadema kuchukua fomu kuwania uenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, mchuano sasa umeanza kupamba moto kwenye nafasi za mabaraza ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Nafasi hizo ni katika Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Baraza la Vijana (Bavicha) na Baraza la Wanawake (Bawacha). Baadhi ya makada wameonyesha nia kuchukua fomu kuwania uenyekiti, katibu, naibu katibu na mweka hazina.
Kibarua kingine kizito kitakuwa kwenye ujumbe wa kamati kuu katika nafasi tano kwa Tanzania Bara, zinazowaniwa.
Tayari makada watano wakiwemo wanaotetea nyadhifa hizo wamechukua fomu, wengine wakionyesha nia kuwania nafasi hizo.
Mchuamo huo unaanza kukolea huku vigogo wa juu wa Chadema – Freeman Mbowe (mwenyekiti) na Tundu Lissu (makamu mwenyekiti-Bara) wakiwa tayari wamechukua na kurejesha fomu kuwania uenyekiti.
Hatua ya wawili hao kuwania nafasi hiyo imezidisha joto kwa kambo zinazowaunga mkono zinazopambana kupata idadi nzuri ya wajumbe wa mkutano mkuu utakaofanyika Januari 21, 2025.
Mbali na hao, wengine waliochukua fomu kuwania uenyekiti wa taifa ni Romanus Mapunda na Charles Odero, aliyechukua fomu leo Jumanne Desemba 24, 2024.
Odero ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria la Cilao, amekabidhiwa fomu na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa.
Katika nafasi za uenyekiti wa Bavicha, waliochukua fomu ni Deogratius Mahinyila na Masoud Mambo.
Mambo aliwahi kuwa kiongozi wa Chadema wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, vya Kati na Sekondari (Chaso), tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mahinyila ambaye ni wakili wa kujitegemea, aliwahi kuwania udiwani Kata ya Berege wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Hivi sasa ni mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Dodoma aliyechaguliwa hivi karibuni.
Wawili hao walionyesha ndio wanaopewa nafasi kubwa ya mmoja wao kuibuka kidedea katika uchaguzi utakaofanyika Januari 13, 2025, ukienda sambamba na ule wa Bazecha.
Kwenye Baraza la Wazee (Bazecha) Casmir Mabina, aliyewahi kuwa mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani ndiye hadi sasa aliyechukua fomu kuwania uenyekiti ingawa pia anatajwa Suzan Lyimo, Spika wa Bunge la Wananchi la Chadema na mbunge wa zamani wa viti maalumu.
Kwa upande wa Bawacha, aliyetangaza nia kuwania uenyekiti wa baraza hilo ni Celestina Simba na wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Suzan Kiwanga na Sharifa Suleiman, ambao hata hivyo hawajachukua fomu wala kutangaza nia.
Simba aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Wananchi la Chadema ametangaza nia kuwania nafasi hiyo leo Jumanne Desemba 24, 2024.
Akitangaza nia hiyo amesema yupo tayari kukabiliana na mpinzani yeyote na wajumbe ndio watapima ubora wa sera.
“Maono yangu ni makubwa juu ya chama hiki katika kuimarisha mchango wa wanawake kupitia uongozi na moja ya dhamira yangu, kwanza kwenda kuishauri kamati kuu ya chama kuweka ukomo kwenye viti maalumu vya ubunge na udiwani ili kutoa fursa na hamasa kwa wanawake wengi kushiriki siasa za uchaguzi,” amesema.
Kiwanga ni mjumbe wa kamati kuu na amewahi kuhudumu nafasi ya ubunge wa jimbo na viti maalumu kwa miaka 10.
Sharifa amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa baraza hilo na hivi sasa ndiye kaimu mwenyekiti wa Bawacha, akichukua nafasi ya Halima Mdee aliyevuliwa uanachama.
Kwa upande wa katibu wa baraza hilo, Catherine Ruge aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu inaelezwa atatetea nafasi hiyo, huku Pamela Massay (mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki) na Ester Dafi aliyewahi kuwa ofisa mwandamizi wa makao makuu ya Chadema kitengo cha sheria, wakitajwa pia kuitaka nafasi hiyo.
Nafasi ya naibu katibu wa Bawacha Bara inatajwa kuwaniwa na Neema Mhanuzi, Groly Tausi na Nuru Ndosi ambaye anaitetea.
Mbali ya uongozi katika mabaraza, nafasi nyingine inayotolewa macho ni ujumbe wa kamati kuu.
Ahobokile Mwaitenda na Patrick Ole Sosopi inaelezwa wameshachukua fomu kutetea nafasi ya ujumbe wa kamati kuu.
Mbali ya hao, wengine waliotangaza nia ni Dorcas Francis, Daniel Ngogo na William Mungai ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa.