Mkosa, Mushi waondoka na simulizi Kenya

BAADA ya kurejea nchini wakitokea Kenya, nyota timu ya Dar City, Amin Mkosa na Jonas Mushi anayeichezea ABC wameondoka na simulizi katika mashindano ya kikapu ya Afrika Mashariki na Kati yaliyomalizika hivi karibuni.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti wachezaji hayo nyota wa kikapu nchini walisema kuna mambo mazito na tena ya maana waliyojifunza ambayo watapambana kuyaendeleza katika michuano mbalimbali watakayoshiriki.

Mkosa alisema katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati alijifunza utofauti wa uchezaji na uwezo wa  kila mchezaji katika mchezo huo baada ya kuwaona wachezaji mbalimbali wakicheza kulingana na timu wanazocheza nazo.

Alisema uchezaji wa nyota kutoka nchi tofauti  ulimpa funzo la kuusoma vyema mchezo wa wapinzani wakati ukiendelea ili kuwa na majibu murua yatakayoisaidia timu yake kupata ushindi.

“Usitegeme leo mchezaji atacheza hivi katika mashindano hayo na kesho atacheza hivyo,” alisema Mkosa.

Akizungumzia kuhusiana na nafasi ya pili waliyopata, alisema Dar City ingekuwa bingwa wa mashindano hayo endapo ingepata muda wa kupumzika kwa siku moja.

“Tulicheza michezo mfululizo bila kupumzika hali iliyofanya tuchoke na kufanya mchezo wetu wa mwisho tufungwe na Remesha ya Burundi kwa pointi 77-58,” alisema.

Hata hivyo, mchezaji huyo anayeichezea Mchenga Star katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL),  kutokana na mkataba wa miaka miwili alionao, alisema ataendelea kuichezea.

“Nina mkataba na Mchenga Star wa miaka miwili, nimebakiwa na mwaka mmoja. Kama Dar City wakinihitaji itawapasa wavunje mkataba wa mwaka mmoja katika timu yangu,” alisema Mkosa.

Naye fundi wa kutupia katika mchezo wa kikapu nchini, Mushi alisema kilichomfurahisha katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ni kufunga pointi mbele ya wachezaji wazoefu waliokuwepo katika michuano hiyo.

Katika mashindano hayo nyota huyo alichaguliwa kuwa mfungaji bora, huku Remesha ikiwa bingwa.

Akizungumzia wachezaji wa timu pinzani, alisema  walikuwa na uwezo mkubwa wa kupambana naye akisisitiza, ” walikuwa na uwezo kunizuia nisifunge kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao.”

Alimtaja mmoja wa wachezaji hao kuwa ni Steve Nsumizi wa Remesha ambaye katika mashindano hayo  alichaguliwa kuwa mzuiaji bora.

Wachezaji wengine ni Landry Ndikumana, Gilbert Nijimbere wanaokipiga Remesha na Salim Kisiu wa KPA.

Wakati akielezea hayo, nyota huyo alisema mchezo  anaoukumbuka uliokuwa mkali dhidi yao ni ule waliokabiliana na KPA ya Kenya ambao Wakenya hao walishinda kwa pointi 85-82.

“Mchezo huo ulikuwa mkali na wa kusisimua. Makosa madogo ndiyo yaliyofanya tushidwe kwenye mchezo huo,” alisema Mushi.

Akizungumzia kuhusiana na mashindano hayo, alisema   yalikuwa ya kwanza kwake kucheza.

Related Posts