Dodoma. Mdundo maarufu uliosikika kwenye taarifa za habari za redio ya Taifa (Radio Tanzania Dar es Salaam-RTD) ulikuwa ni wa kipekee.
Mdundo huo uliokuwa ukianza kwa ‘kududundu, kudu kudu kudu kudundundu, halafu ti ti tiii’, uliashiria muda wa taarifa za habari.
Ni mdundo uliotokana na ngoma 17 zilizopigwa kwa wakati mmoja na Mzee Morris Nyunyusa, mlemavu wa macho ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kwa kipaji chake cha kipekee.
Nyunyusa hakuwa mtu wa kawaida, licha ya ulemavu wake wa macho, alithibitisha kwamba vipaji havina mipaka.
Alianza safari yake ya sanaa kwa kupiga ngoma saba, lakini kila mwaka alivunja rekodi yake mwenyewe kwa kuongeza idadi ya ngoma alizokuwa akipiga kwa wakati mmoja. Hatimaye, alifikia idadi ya kushangaza ya ngoma 17.
Midundo yake ilisikika kwa umahiri wa hali ya juu kiasi kwamba yeyote aliyeisikia hata kwa mbali alitambua ni muda wa taarifa ya habari.
Umahiri wa Mzee Nyunyusa haukuishia tu katika kutambulisha taarifa ya habari. Alijulikana ndani na nje ya nchi, na kazi yake ilimpa heshima kubwa.
Moja ya mafanikio yake makubwa yalikuwa ni kuiwakilisha Tanzania kwenye tamasha la kimataifa la Expo 70, lililofanyika Osaka, Japan.
Katika tukio hilo, picha yake ilichapishwa kwenye stempu za Shirika la Posta la Tanzania, ishara ya heshima kubwa kwa mchango wake kwenye sanaa na utamaduni wa taifa.
Ziara ya Japan ilifungua milango mipya kwa Mzee Nyunyusa, na sifa zake zilisambaa kote ulimwenguni.
Miongoni mwa watu waliovutiwa na kipaji chake ni mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe.
Mbaraka alitunga wimbo maarufu uitwao “Expo 70,” ambapo alimkumbuka na kumpongeza Mzee Nyunyusa kwa kipaji chake.
Katika kipande cha wimbo huo, Mbaraka aliimba:
“Maonyesho Japan yalifana sana, Likembe, Mahoka na ngoma za Taifa, wacheza midimu na wachezea nyoka, Mzee Morris na ngoma zake kumi oyeee.”
Kwa kweli, Mzee Morris Nyunyusa alikuwa kivutio cha aina yake. Wageni kutoka mabara mbalimbali walipozuru Tanzania, walitamani kukutana naye na kushuhudia uwezo wake wa kipekee.
Midundo yake haikuwa tu burudani, bali pia iliwakilisha utamaduni wa Kitanzania na ngoma za asili.
Ngoma zake zilijulikana kama ‘msoma,’ aina ya ngoma ya asili kutoka Mkoa wa Ruvuma, ambayo ilishinda umaarufu wa aina nyingine za ngoma kama lizombe.
Mdundo wa ngoma ya ‘msoma’ ulijulikana kwa sauti za ‘mkabe rungu mkabe rungu mkabe rungu,’ zikimaanisha ‘mpige rungu mpige rungu.’
Katika kipindi chake cha uhai, Mzee Nyunyusa alionyesha uvumilivu, ubunifu, na nidhamu ya hali ya juu katika kazi yake.
Alikuwa mfano wa kuigwa, si kwa wasanii wa ngoma pekee, bali pia kwa yeyote anayepigania ndoto zake licha ya changamoto alizonazo.
Alipokuwa akiishi kwenye nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Mtoni kwa Kombo, Temeke, aliendelea kuvutia watu wengi kwa kipaji chake.
Kazi yake ilihamasisha hata vizazi vilivyofuata, akiwamo mwanawe, Siddy Morris, maarufu kama “Super Konga.”
Siddy Morris aliendeleza urithi wa baba yake kwa kuwa mpiga tumba hodari na maarufu hapa nchini.
Alitamba na bendi maarufu kama Maquis du Zaire, Bicco Stars na MK Group wana Ngulupa.
Umaarufu wa Siddy ulithibitisha kwamba kipaji ni urithi unaoweza kuendelezwa kizazi hadi kizazi.
Mzee Nyunyusa alifariki dunia mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, iliyokuwa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Alizikwa katika makaburi ya Wailes, Temeke, karibu na Uwanja wa Taifa, ambao sasa unajulikana kama Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kifo chake kiliacha pengo kubwa, lakini alama yake katika sanaa ya ngoma itaendelea kuishi milele.
Historia ya Mzee Morris Nyunyusa ni ushuhuda wa jinsi sanaa na utamaduni vinavyoweza kuunganisha watu na kuipa nchi hadhi ya kipekee duniani.
Alikuwa tunu ya taifa ambaye kipaji chake kilivuka mipaka ya kawaida na kuifanya Tanzania kujivunia.
Midundo yake ilikuwa siyo tu sehemu ya taarifa ya habari bali pia alama ya urithi wa kiutamaduni unaostahili kuhifadhiwa kwa vizazi vijavyo.
Kwa kuzingatia mchango wake mkubwa, ni muhimu kwa Serikali na wadau wa sanaa nchini kuhakikisha kuwa historia ya watu kama Mzee Nyunyusa haipotei.
Inaweza kuwa kupitia kuanzisha makumbusho au programu za mafunzo kwa vijana wenye vipaji ili waendeleze urithi huu.
Urithi wa Mzee Nyunyusa ni kumbukumbu ya nguvu ya sanaa na nafasi yake katika kujenga utambulisho wa Taifa.
Leo hii, tunapokumbuka maisha na kazi ya Mzee Morris Nyunyusa, tunapaswa pia kutambua jukumu letu la kuhifadhi na kukuza utamaduni wa Tanzania.
Urithi wake unapaswa kuwa mwanga unaotuongoza katika kuthamini vipaji vya ndani na kuhakikisha kuwa vinaendelezwa kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa hakika, historia ya Mzee Morris Nyunyusa ni hadithi ya ushindi wa ubunifu dhidi ya vikwazo na urithi usio na kifani katika utamaduni wa Tanzania.