Mwenyekiti mpya Coastal ayakataa makundi

BAADA ya Hassan Muhsin kuchaguliwa na wajumbe zaidi ya 235 kuwa mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, ameitaja falsafa yake kuwa ni umoja ikiwa ni kipaumbele chake kikubwa itakayosaidia kuvutia wawekezaji na wadhamini watakaoiwezesha kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu na michuano mingine.

Kiongozi huyo alichaguliwa katika Mkutano Mkuu wa Coastal Union uliowapata viongozi wapya.

Muhsin aliwataka wanachama kuvunja makundi na kuimariaha umoja na mshikamano ili kufikia malengo ambayo watayaweka pamoja kwa maslahi ya klabu.

“Tutajitahidi kuwekeza katika wafadhili. Tunaamini kuwa wafadhili hawawezi kwenda sehemu ambayo haijatulia, hivyo lazima tuwe na umoja. Tukitulia tunao uwezo wa kupata wafadhili.

“Ukiangalia miaka zaidi ya 10 iliyopita Coastal Union hatukuwa na mfadhili hata mmoja, lakini sasa hivi angalau tuna wawili watatu. Tutajipanga kwa pamoja ili kuimarisha ushirikiano na wawekezaji na kutafuta vyanzo vingine vya mapato,” alisema Muhsin.

Alisema atahakikisha anaendelea kulisimamia soka la vijana jukumu ambalo alikuwa nalo tangu akiwa makamu mwenyekiti ambapo wamewaibua wachezaji wanaofanya vizuri kwenye ligi wakiwa na timu mbaalimbali akiwemo Bakari Mwanyeto anayecheza Yanga, Charles Semfuko na Ramadhani Chuma wanaoitumikia Coastal Union.

“Tumekuwa tukitegemea sana vijana ambao tunawaibua sisi wenyewe. Hii ni sehemu ambayo nilikuwa naishughulikia mwenyewe zaidi ya miaka sita nilikuwa ni mlezi. Kwa kuanzia tumejipanga pia na timu ya wanawake ambayo ni kama tulikuwa tumeiacha. Hatukuwa na kipaumbele nayo,” aliongeza.

Alisema Coastal Union inahitaji wanachama wengi zaidi ya waliopo sasa kulinganisha na ukubwa ilionao ambao kwa kulipia ada za uanchama watachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya klabu.

“Tuna tatizo la kuwa na wanachama hai wachache. Katika kumbukumbu zetu tuna wanachama zaidi ya 700, lakini waliopo hai ni 300 tunataka tuliboreshe hili tuweke utaratibu mzuri wa kuwafanya watu waipende klabu yao. Tunakwenda pia kuongeza wanachama nje ya nchi yetu,” alisema.

Mwenyekiti aliyemaliza muda, Steven Mguto aliutaka uongozi mpya kuhakikisha hautoi mwanya kwa wanachama wasiolipa ada kuwapasua vichwa pale wanapohitaji kupiga hatua jambo ambalo linazitesa klabu nyingi zenye wanachama.

“Klabu zinazotegemea wanachama zina shida nyingi na sio kwa Coastal Union pekee hata kwa Simba na Yanga wapo wanachama hawalipi ada wala kufuatilia mambo ya klabu. Sasa tunataka uongozi unaokuja ukomeshe mtindo wa wanachama kulipiwa ada zao na ndio hao wenye maneno ya kudhoofisha klabu,” alisema Mguto.

Muhsin alitangazwa mwenyekiti akiwa ndiye mgombea pekee aliyekidhi vigezo huku wajumbe saba wa Mkutano Mkuu wakichaguliwa. Wajumbe saba waliochaguliwa katika uchaguzi huo kati ya 15 waliowania nafasi hiyo ni Nasoro Mohammed akipata kura 171, Ally Shechonge (169), Bakari Mohammed (142), Abdallah Zuberi (136), Hussein Abdallah (133), Bakari Fumbwe (112) na Emmanuel Mchechu (140).

Wakati huohuo, Muhsin kwa mamlaka aliyopewa kikatiba aliwateua Dk Fungo Ali Fungo, Abdrahaman Fumbwe, Mohammed Kiruasha na Saida Said Bawaziri kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji. Pia alimteua Dk Fungo kuwa makamu mwenyekiti wa klabu.

Related Posts