Arusha. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko na binti yake Maureen Nnko, waliofariki dunia kwa ajali ya gari watazikwa Jumamosi, Desemba 28, 2024.
Amos na binti yake wa kwanza walifariki dunia katika ajali iliyotokea maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro juzi mchana Desemba 22, 2024.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Desemba 24, 2024, mmoja wa wanafamilia Obilio Mbise amesema familia hiyo kwa kushirikaina na Ofisi ya Msajili wa Hazina, wamekubaliana maziko yafanyike Jumamosi kijijini kwake Seela wilayani Arumeru mkoani Arusha, Desemba 28,2024.
Akizungumzia hali za majeruhi, Mbise amesema bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Tumeshakaa vikao na tumekubaliana Jumamosi wataagwa na maziko yatafanyika Kijiji cha Seela, Kata ya Seela Sing’isi wilayani Arumeru,” amesema Mbise.
Katika ajali hiyo waliojeruhiwa ni mke wa marehemu, Agnes Nnko, watoto wengine ni Marilyn, Melvin na mwanafamilia mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Saylvana.
Jana Mbise amesema miili ya Amos na Maureen iliyokuwa imehifadhiwa wilayani Same, ilifuatwa kwa ajili ya kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mt.Meru.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu ilieleza kuwa mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na familia ya marehemu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina.