Polisi timamu kwa ulinzi Krismasi, Mwaka Mpya

Dar/Mikoani. Wakati Watanzania wakisherehekea sikukuu ya Krismasi leo Desemba 25, 2024, Jeshi la Polisi limewahakikishia usalama likiwataka wananchi kuchukua tahadhari, hasa kuwalinda watoto.

Msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, matukio ya uhalifu yamekuwa yakiongezeka katika maeneo tofauti nchini, kutokana na watu wengi kuwa kwenye mikesha na sherehe wakiacha nyumba bila uangalizi.

Pia, baadhi ya watu katika kusherehekea, hunywa pombe kupita kiasi wakisababisha ugomvi kwenye baa na wengine kupata ajali wakiendesha vyombo vya moto kutokana na ulevi.

Wezi na vibaka hutumia fursa hiyo kutekeleza uhalifu kwenye baa, majumbani na hata kwenye magari ya watu, matukio yanayowarudisha nyuma kimaendeleo wananchi na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Kutokana na uzoefu wa sikukuu zilizopita, Jeshi la Polisi limetoa angalizo kwa jamii kuzingatia mambo manne ikiwemo kutoweka mali au fedha kwenye mazingira hatarishi.

Mambo mengine yanayopendekezwa na jeshi hilo ni kuacha nyumba bila uangalizi, kutumia vilevi kupindukia, kuacha watoto wakizurura ovyo bila uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu.

Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Desemba 24, 2024 na msemaji wa Jeshi hilo, David Misime inaeleza namna walivyojipanga kuimarisha usalama wakati wa sikukuu hizo.

“Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuimarisha usalama katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa kushirikiana na wananchi, viongozi wa nyumba za ibada, kamati za usalama za nyumba za ibada ambako zitafanyika na viongozi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha kila mmoja anasherehekea kwa amani na utulivu,” inaeleza taarifa hiyo.

Misime katika taarifa hiyo ametoa wito kwa kila mmoja kusherehekea na kufanya shughuli zake katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.

Amesisitiza kwamba: “Usalama unaanza na wewe mwenyewe kwa kujiepusha na vitendo vitakavyohatarisha usalama wako, mali zako na familia yako.

“Vitendo kama vile kuacha nyumba bila uangalizi, kutumia vilevi kupindukia, kuacha watoto wakizurura ovyo bila uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu. Tuepuke kuweka mali au fedha katika hali hatarishi.”

Misime amesema watachukua hatua kuzuia ajali ikiwemo ukamataji kwa wanaovunja sheria za usalama barabarani na utoaji elimu.

Polisi imesisitiza raia kukemea papo kwa hapo na kutoa taarifa pale wanapoona mtu yeyote akifanya vitendo vya kuhatarisha usalama barabarani.

“Baadhi ya ajali zilizotokea ukisikiliza mashuhuda inaonyesha wazi tungekuwa na utamaduni na uthubutu wa kukemeana zingeepukika hata kwa yale magari yaliyokuwa yanatumiwa na familia na mengineyo,” inaeleza taarifa ya Polisi.

Makamanda wa Polisi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wamesema usalama na doria umeimarishwa kuhakikisha sikukuu zinaisha kwa amani.

“Watu wasiache nyumba wazi. Haiwezekani wote wanaenda kusherehekea, kwenye mkesha wanaacha nyumba zote zipo wazi… ukiacha nyumba wazi ni kishawishi kwa mhalifu. Tutalinda, tutaimarisha doria lakini hatuwezi kusema tutalinda nyumba moja baada ya nyingine,” amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda.

Amepiga marufuku ‘disko toto’ akisema maeneo linakofanyika husababisha maafa kwa watoto kwa kuwa waendeshaji wake huangalia fedha zaidi badala ya idadi ya watoto wanaoingia kwenye kumbi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo pia amepiga marufuku disko toto na wanaokwenda kuogelea maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria, akisema siyo salama. Amesema polisi watakuwa wakifanya doria kwenye maeneo yote.

Amewatahadharisha wazazi kutowaacha watoto watoke wenyewe nyumbani na kwenda kutembea kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu na barabarani kwa kuwa ni hatarishi, hivyo amewaasa wanapotoka wawe na mwangalizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wao ili kuepuka madhara yanayoweza kuwakuta wakati wa sikukuu hasa katika maeneo yao.

“Hatutaki kusikia maafa yoyote yametokea kwenye mkoa wetu, hivyo wazazi na walezi tunawataka wawe makini katika kuwasimamia watoto. Sisi Jeshi la Polisi tumejiandaa kwa ulinzi lakini peke yetu hatuwezi ni lazima kuwepo ushirikiano,” amesema.

Ulinzi kwa watoto ni suala ambalo pia limesisitizwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akizungumzia usalama wa watoto, amesema kutokana na baadhi ya wazazi kuwa na tabia ya kwenda na watoto kwenye kumbi na maeneo ya starehe ili kufurahia sikukuu, ni jambo lisilo jema kwa kuwa wanajifunza mambo mabaya yanayofanyika huko.

Jijini Mwanza leo ulinzi umeimarishwa ikiwamo kwenye vituo vya daladala ambako kuna askari wa usalama barabarani.

“Leo madereva wanaendesha kistaarabu sana maana hawajui nini kitawakuta mbeleni, kila eneo leo askari wapo tofauti na siku nyingine wanakuwa wanajua sehemu gani waendeshe rafu na wapi niendeshe vizuri kuna askari,” amesema Hamduni Juma, mkazi wa Jiji la Mwanza.

“Yanayoelekezwa ni kwa faida yetu, kuna faida gani baada ya sikukuu unaishia kulazwa au hata kufa kwa kufanya matendo ambayo yanahatarisha usalama wako na wa wengine, mfano mtu unakunywa pombe kupitiliza kisha unaanza kuendesha gari au pikipiki,” amesema Emmanuel Mirigo, mkazi wa Musoma mkoani Mara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe amewataka wananchi kuchukua tahadhari hasa wanapokuwa barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matumizi ya vilevi wanapoendesha vyombo vya moto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema wamejipanga kuzuia uhalifu, akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Ameonya vitendo vya kulipua baruti, kuchoma matairi na kufanya fujo katika sikukuu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Morogoro, Shabani Marugujo amesema wamefanya ukaguzi kwenye baa na maeneo mengine ya michezo ya watoto,  kwa lengo la kuangalia hali ya usalama na namna yanavyoweza kutoa huduma kwa watu bila kuleta madhara au majanga.

“Maeneo hayo ni pamoja na hoteli zenye mabwawa ya kuongelea, kikubwa tunaangalia kina cha maji kwenye mabwawa hayo, lakini pia tumetoa elimu kwa wasimamizi wa mabwawa haya na kutoa onyo la kutoruhusu mtoto kuogelea kwenye bwawa la watu wazima. Pia kutoruhusu mtu kuogelea akiwa amelewa,” amesema.

Amesema wametoa elimu kwa madereva na abiria namna ya kutumia namba ya dharura ya 114 endapo watapata majanga wakati wa safari na kuhitaji huduma ya uokozi.

Kamanda Marugujo amewataka wananchi kuhakikisha wanazima vyombo vyote vya umeme wakitoka kwenye nyumba zao kwenda kusherehekea sikukuu ili kuepuka majanga ya moto yanayoweza kutokea.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa (Dar), Saada Amir (Mwanza), Beldina Nyakeke (Mara), Ananias Khalula (Kagera), Seif Jumanne (Njombe), Iddi Mumba (Katavi) na Hamida Sharif (Morogoro).

Related Posts