Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume mbili, ya kwanza itahusika na tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na ya pili itaangalia utekelezaji wa uhamaji wa hiari kutoka eneo la hifadhi hiyo.
Uundaji wa tume hizo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Desemba mosi, 2024 alipokutana na viongozi wa kimila wa jamii ya kimasai wanaoishi eneo la Hifadhi la Ngorongoro alitangaza uamuzi wa Serikali kuunda tume.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, leo Jumatatu, Desemba 23, 2024, tume ya masuala ya ardhi utakuwa na wajumbe tisa, huku ile inayotathmini uhamaji ikiwa na wajumbe wanane.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro itaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Gerald Ndika aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume hiyo.
Dk Ndika kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, atasaidiana na wajumbe tisa walioteuliwa akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo.
Wengine ni Zakia Meghji, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Jaji George Masaju ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mshauri wa Rais, Sheria.
Pia, Dk Richard Muyungi ambaye ni Mshauri wa Rais, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi ameteuliwa pamoja na Balozi Salome Sijaona ambaye ni Balozi na Katibu Mkuu mstaafu.
“Pia Rais amemteua, Profesa Wilbard Kombe ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Emmanuel Luoga kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mollel James Moringe Diwani na Katibu wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro na Moi Aprakwa Sikorei na Diwani na Mkazi wa Ngorongoro,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefanya uteuzi wa tume ya kutathmini uhamaji wa hiari wa wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Katika tume hiyo, Rais Samia amemteua Musa Iyombe ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu kuwa mwenyekiti wa tume hiyo.
Iyombe atasaidiwa na wajumbe wanane, akiwemo Sihaba Nkinga ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu, Alphayo Kidata ambaye ni wa Rais, Uwezeshaji Biashara na Masuala ya Kodi, Balozi Valentino Mlowola na Balozi Mstaafu na aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wengine Balozi mstaafu na aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Balozi Mohamed Mtonga, Balozi mstaafu, Balozi George Madafa, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Haruna Masebu.
“Wengine walioteuliwa Edward Maura Nduleti na Rehema Moisare ambaye ni Mwalimu na Mkazi wa Ngorongoro,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.