Sababu Ninja kuachana na FC Lupopo hii hapa

BEKI Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema sababu ya kuvunja mkataba wa miezi sita uliokuwa umebaki katika klabu aliyokuwa anaichezea ya FC Lupopo ya DR Congo ni maslahi.

Ninja alijiunga na klabu hiyo msimu huu akitokea Lubumbashi Sports ya nchini humo ambayo aliichezea kwa msimu mmoja kati ya miwili aliyokuwa amesaini ambapo sababu ya kuachana nayo ni changamoto ya mshahara.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga amesema ameachana na klabu hiyo kwa amani na amekatiwa tiketi ya ndege ya kurejea hapa nchini kesho, Jumatano baada ya kufikia makubaliano kutokana na maslahi kutokuwa mazuri.

“DR Congo ni kugumu kwa upande wangu. Maslahi imekuwa changamoto, hivyo sikuona sababu ya kuendelea nao katika miezi sita iliyobakia,” amesema Ninja.

“Unapocheza nje na umeacha familia Tanzania wanakuwa wanakutegemea uwatumie pesa. Sasa inapotokea kila mara unawapa kalenda inaleta changamoto.”

Alipoulizwa juu ya taarifa nyingine kwamba hakuwa na maelewano mazuri na kocha wa FC Lupopo, Ninja amejibu: “Kila kocha ana chaguo lake. Pia kazi ya soka ni ya mzunguko naweza kukutana naye popote, hivyo kazi yangu ni kujituma na mazoezi na siyo kuzungumzia makocha.”

Nini kinafuata baada ya kuachana na FC Lupopo, Ninja amesema tayari amepokea ofa za ndani na nje ya nchi lakini ni vigumu kuziweka wazi kabla dili halijatiki.

Mbali na Yanga timu nyingine ambazo amezichezea ni MFK Vyskov iliyomtoa kwa mkopo kwenda LA Galaxy ya Marekani, akarejea tena Yanga na baada ya kuachana na Wanajangwani akaenda DR Congo kujiunga na Lubumbashi Sports.

Related Posts