STAMICO yarejesha tabasamu kwa wenye mahitaji maalum kijiji cha Samaria Hombolo

Na Mwandishi wetu Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Staki Senyamule kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wametembelea na kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalum katika kijiji cha Samaria kilichombo Hombolo mkoani Dodoma.

RC Senyamule ameahidi kutoa kiasi cha Shilingi laki tano kwa Kaya zote 23 zilizopo katika eneo hilo ambalo limekuwa eneo wanaloishi watu wenye ukoma.

Akizungumza katika eneo hilo, RC Senyamule amesema kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linayo haki ya kuendelea kuchukua tuzo mbalimbali za ushindi kwa sababu ni Shirika la kipekee linalogusa maisha ya watu.

Ameipongeza STAMICO kwa kuwaweka hadharani watu wa Kijiji cha Samaria ili wadau wengine waone na waguswe akisisitiza kuwa yeye pia atakuwa sehemu ya maendeleo ya Wanasamaria.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa jitihada zote hizo ni kwa kusudi la kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inatumia Nishati safi ya kupikia pamoja na kuwainua wananchi Kiuchumi .

Aidha Dkt. Mwasse ameahidi kuwapa Wananchi hao wa Kijiji hicho Uwakala wa usambazaji Mkaa mbadala (Coal Briquette) unaozalishwa na STAMICO kuanzia January 2025 hivyo kujipatia kipato na kuendeleza Kampeni ya Nishati safi ya kupikia mkoani humo.

Vile vile Dkt. Mwasse ametumia fursa hiyo kuahidi kuwa sehemu ya furaha kwa wana Samaria kwa kuendelea kuwasaidia vitu mbalimbali ambapo moja ya mambo aliyoahidi kuyatekeleza kwa haraka ni pamoja na swala la umeme,maji na kurasimisha kundi lao la kwaya ili waweze kuendeleza Sanaa zao.






Related Posts