Unguja. Wakati Mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mji Mkongwe ikisitisha kwa muda mchezo wa makachu Forodhani, vijana na wadau wanaojihusisha na mchezo huo wameeleza athari za kiuchumi na kwenye sekta ya utalii.
Hata hivyo, mamlaka hiyo imetangaza kuwa itasainisha mikataba maalumu na wale watakaokubaliana na masharti ndiyo watakaoruhusiwa kurejea na watakaoshindwa, hawataruhusiwa tena kushiriki mchezo huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 22, 2024 na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe, Ali Abubakar marufuku hiyo imetokana na ukiukwaji wa sheria na miongozo, ikiwa ni pamoja na mavazi yasiyozingatia utamaduni, uharibifu wa mifereji na miundombinu, pamoja na matumizi yasiyofaa ya debe za taka katika michezo ya vichekesho.
Taarifa hiyo imesema kuwa marufuku hiyo itaendelea hadi utaratibu mpya wa kuimarisha usimamizi utakapowekwa.
Serikali inatambua mchango wa mchezo wa makachu katika kutangaza utalii, lakini hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya wale watakaobainika kukiuka sheria.
Baadhi ya vijana waliozungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati taofauti wamesema marufuku hiyo imeathiri vyanzo vyao vya kipato. Ali Shaib, maarufu Kibu amesema wataendelea kufuata maelekezo hadi watakaporuhusiwa tena.
“Inatuathiri ila hakuna namna,” amesema Kibu.
Naye Albaiya Mussa amesisitiza umuhimu wa kufuata utaratibu na kuwa mabalozi wazuri wa eneo hilo.
Amesema kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha taratibu zinafuatwa na watahakikisha miongozo yote inazingatiwa baada ya kufunguliwa.
Taarifa zilitolewa na baadhi ya vijana hao zimedai walikaa na uongozi wa mamlaka Jumapili Desemba 22, 2024 wakaambiwa wamezuia kwa siku tatu na Desemba 26, 2024 wataruhusiwa kuendelea.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo amesema hakuna muda maalumu uliowekwa kwa marufuku hiyo, kwa sababu utaratibu maalumu wa kusaini mikataba na vigezo vya usimamizi bado unaandaliwa.
Amesema kurejea kwa washiriki kutafanyika kwa awamu baada ya kusaini mikataba na wale watakaoshindwa kutimiza masharti hawataruhusiwa tena.
“Kwa sasa ichukuliwe hivyo kama tulivyotoa taarifa yetu, ila tunaweka utarataibu maalumu, tutawasainisha mikataba maalumu ya kurudi hapo. Kwa sasa hatutaruhusu kurejea kundi lote kwa pamoja, kila mmoja atakuwa anarejea kwa muda wake baada ya kusaini mkataba, atakayeshindwa masharti, huyo hatapata nafasi tena,” amesema.
Mdau wa michezo, Sadif Haji amesema eneo hilo ni kivutio kikubwa cha utalii kwa Zanzibar na ni muhimu utaratibu mpya uwekwe haraka ili kuepusha athari zaidi kwenye sekta ya utalii.
Makachu ni mchezo unaohusisha vijana kujirusha baharini, ambao umekuwa kivutio kikubwa kwa wageni na wenyeji na unatoa mchango mkubwa kwa utalii na ajira kwa vijana wa Zanzibar.