Same. Watu watatu waliofariki dunia baada ya kuangukiwa na gema wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wamezikwa, huku Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni, akiwataka wananchi wanaoishi maeneo ya milimani kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua.
Mvua zilizonyesha kuanzia Desemba 20 hadi 22 mwaka huu katika Wilaya ya Same zilisababisha vifo vya watu sita na wengine wanne kujeruhiwa baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kuangukiwa na gema usiku wakiwa wamelala.
Kasilda amehudhuria ibada ya maziko ya familia iliyofiwa na watu wawili ambao ni Joyce Elifuraha (57) na mume wake Elifuraha Elienea (59) wa kijiji cha Mjema, Kata ya Bombo, pamoja na Eliakunda Mrutu wa kijiji cha Duma, Kata ya Msindo.
Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika leo Jumanne Desemba 24, 2024, Kasilda amesema baadhi ya wananchi wamejenga nyumba kwenye vilele vya milima bila kufuata tahadhari za kimazingira, na hali hiyo inahatarisha maisha yao hasa wakati huu wa mvua kubwa.
“Tumepoteza watu sita kipindi hiki cha mvua. Tuko kwenye huzuni kubwa, lakini ni lazima tuchukue tahadhari. Wale wanaoishi kwenye maeneo hatarishi wahame ili kuepusha maafa zaidi,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Aidha, amesema ukataji miti hovyo na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya milimani umechangia pia kutokea kwa maafa hayo.
Hivyo, amesisitiza kuwa jiwe linapokosa mizizi ya miti ya kulishikilia, linakuwa katika hatari ya kuanguka wakati wa mvua ni vema wakachukua tahadhari bila kupuuza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, amesema kuna maeneo ambayo watalazimika kuwahamisha wananchi kwa muda hadi msimu wa mvua upite.
Lakini pia amesema maeneo mengine yatazuiliwa kujengwa makazi ya kudumu kutokana na hatari za kimazingira.
“Huku milimani si mafuriko, bali ni maporomoko ya gema za udongo ambazo husababisha nyumba kuangukiwa. Tutachukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wanahama maeneo hatarishi,” amesema Mapande.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mjema, Jeremia Mjema amekumbusha kuwa maafa kama haya yalitokea pia mwaka 2023, lakini hali ya mwaka huu imekuwa mbaya zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya maafa ya wilaya, kata zilizoathirika zaidi ni Msindo, Vuje, Bombo, Mtii, na Maore. Mbali na vifo, mvua hizo pia zimesababisha nyumba 25 kubomoka, kuharibu miundombinu ya barabara na mazao mashambani.
Wananchi wamehimizwa kushirikiana na mamlaka za wilaya ili kuhakikisha usalama wao wakati huu wa msimu wa mvua kubwa.