Watatu wafa kipindupindu kikitajwa Mbeya

Mbeya. Watu watatu wakiwamo wawili wa familia moja wamefariki dunia wakihofiwa kuugua kipindupindu katika Mtaa wa Ilolo, Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Akizungumza Mwananchi leo Desemba 24, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo, Ezekiel Mwasandube amesema mmoja kati ya watu hao amezikwa.

“Wengine tunasubiri kibali kwa kuwa miili ipo hospitali, tunapaswa kila mmoja kuchukua tahadhari,” amesema.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Ambakisye Mzunguko (70), Laheri Mwashoholo (46) na mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Magreth.

Mwananchi ilifika nyumbani kwa familia iliyopoteza watu wawili na kukuta waombolezaji.

Mwenyekiti huyo wa mtaa akiwa na viongozi wenzake waliwataka waombolezaji kuondoka.

Ofisa Afya, Yondo Hamis na Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, David Mwanjonga walisimamia nyumba ya marehemu kufungwa milango wakanyunyiza dawa.

Mwanjonga amesema kwa sasa wanasubiri ripoti ya madaktari kubaini chanzo cha vifo hivyo wakati wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari.

“Tunasubiri ripoti ya madaktari kuthibitisha kama kweli ni kipindupindu wakati huohuo tutaendelea na elimu kupitia mkutano wa dharula kwa wananchi kuchukua tahadhari,” amesema mtendaji wa mtaa huo.

David Emanuel, mtoto wa marehemu Ambakisye, amesema kabla ya kifo cha mzazi wake alikuwa akitapika na kuharisha na alipofikishwa hospitali alifariki dunia.

“Tatizo lilianza siku moja kabla ya kifo chake, tukampeleka hospitalini ndipo umauti ukamkuta, kwa sasa tumebaki wanne na tunazingatia ushauri tuliopewa na wataalamu,” amesema.

Sungura Mzunguko, ambaye ni ndugu wa marehemu amesema wanaiachia Serikali ya mtaa kuamua kinachofaa kufanyika.

“Mimi kama msimamizi wa familia tunawaombea wapumzike kwa amani na hatuna cha kufanya zaidi ya kuiachia serikali ya mtaa itakayoamua nini kifanyike,” amesema Mzunguko.

Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema kuzungumzia taarifa za vifo hivyo amesema anafuatilia.

“Hivyo vifo ni wapi? Ngoja niende huko,” amesema Dk Elizabeth alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi.

Desemba 22, aliliambia Mwananchi kuwa hakuna taarifa ya uwapo wa kipindupindu akieleza anayetoa takwimu aulizwe.

Desemba 19, 2024 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila alilieleza Mwananchi kuhusu ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu idadi ikifikia kuwa 46 akiwaomba wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga.

Alisema kamati ya afya jijini humo inaendelea kuchukua hatua ikiwamo kutoa elimu kwa mama na baba lishe katika masoko na kusimamisha huduma kwa baadhi ya maeneo zikiwamo baa zisizo na ubora.

“Ongezeko hili linatishia na kuleta hofu, lazima tushirikiane na wananchi na wadau kukabiliana na ugonjwa huu, kamati ya afya kwa ushirikiano wa mkuu wa wilaya tunaendelea na elimu na kukagua visima na sehemu za baa na kuchukua hatua,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa alipotafutwa na Mwananchi kwa kupigiwa simu alielekeza atumiwe ujumbe, ambao baada ya kutumiwa hakuujibu.

Related Posts