Watoto 200 Dar, Pwani Washerehekea Kikapu 

ZAIDI ya watoto 200 kutoka mkoani Pwani na Dar es Salaam wameshiriki maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mpira wa Kikapu.

Maadhimisho hayo yalidhaminiwa na Basketball For Good Foundation yalifanyika katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Shalom kilichopo Kibaha, Pwani.

Balozi wa Basketball For Good nchini, Bahati Mgunda alisema makocha 15 walitoa mafunzo kwa watoto hao ambao walionekana kuufurahia mchezo huo.

Mgunda ambaye pia ni mratibu wa kituo cha michezo cha JMK Youth Park, alisema watoto walijifunza pia stadi za maisha pamoja na kutambulishwa mchezo huo.

“Watoto walifurahi kutokana na jinsi walivyokuwa wanatambulishwa mchezo huo mpya kwao,” alisema Mgunda.

Alieleza kuwa wakiwa katika kituo cha Shalom  walitoa magoli mawili ya mchezo wa kikapu ili kuwawezesha watoto kuendelea kujifunza na kucheza kikapu kwa ajili ya kujiweka fiti.

Baada ya hapo, watoto waliendelea kupatiwa mafunzo zaidi ya stadi za maisha katika Kituo cha Filbert Bayi Olympic Africa Center.

Related Posts