Wenye simu hizi kupotea WhatsApp mwaka mpya

Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa simu za Android za matoleo ya zamani na unahitaji kuendelea kutumia WhatsApp huna budi kuandaa bajeti ya pesa kununua simu nyingine kwa kuwa mtandao huo uko mbioni kuacha kufanya kazi kwenye simu hizo.

WhatsApp itaacha kufanya kazi kuanzia Januari mosi 2025 kwa sababu simu hizo zenye mfumo wa uendeshaji wa KitKat hazina uwezo wa kupokea matoleo mapya ikiwamo kuboresha usalama na matumizi ya mtumiaji.

Mfumo wa KitKat katika simu za Android ni ule wa toleo kuanzia 4.4 unaohusisha Uendeshaji wa Google (OS)  na unapatikana kwenye simu zilizo na RAM ya MB 512.

Miongoni mwa simu hizo za zamani zilizo na mifumo ya uendeshaji iliyopitwa na wakati ni matoleo ya Samsung, Motorola, HTC, LG na Sony kama zilivyotajwa kwenye tovuti za Oneindia, Business Standard, GSM Arena na Republic World.

 “Samsung;  Galaxy S3, Galaxy Note 2, Galaxy Ace 3, Galaxy S4 Mini. Motorola: Moto G (1st Gen) Razr HD Moto E 2014. HTC: One X One X+ Desire 500 Desire 601 LG: Optimus G Nexus 4 G2 Mini L90. Sony: Xperia Z Xperia SP Xperia T Xperia V These phones,” zimetajwa katika tovuti hizo.

Imeelezwa kuwa, mabadiliko hayo yataathiri watumiaji wenye simu hizo ambazo nyingi zilizotolewa miaka tisa hadi kumi iliyopita.

Kwa mujibu wa kampuni mama ya WhatsApp, (Meta) uamuzi huo ni sehemu ya jitihada za kudumisha usalama na utendaji kazi.

Aidha, kutokana na teknolojia kuzidi kukua na kuendelea, vifaa vya zamani haviwezi tena kuunga mkono vipengele vipya vya programu au kulinda data nyeti kwa ufanisi.

Vilevile, bila kuwa na vipengele vya usalama kwa vifaa hivyo, vinakuwa katika hatari kubwa zaidi ya uhalifu mtandaoni. Kwa hiyo, kampuni imechagua kuendelea na vifaa vinavyoweza kuendesha programu za kisasa.

Hata hivyo, kwa upande wa watumiaji wa iPhone wenyewe watakuwa na muda hadi Mei 5, 2025 kwa zile zinazoendeshwa na iOS 15.1 au chini na zenyewe hazitapata tena WhatsApp.

Related Posts