Clara: Mbona ni kawaida yangu

MSHAMBULIAJI wa timu ya wanawake ya Al Nassr inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake  Saudia, Clara Luvanga amesema imekuwa kawaida kwake kufunga kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Al Hilal ikiwa miongoni mwa michezo yenye msisimko nchini humo.

Mchezo huo ulipigwa wikiendi iliyopita na chama hilo la Clara likiondoka na ushindi wa mabao 4-0, huku mawili yakifungwa na nyota huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Luvanga amesema kwake ni fahari kubwa kuifunga timu kubwa kama Al Hilal ambao ni mafahari wakubwa nchini humo.

Ameongeza kuwa sio mara ya kwanza kuifunga kwani msimu uliopita alifanya hivyo, lakini huu ukiwa tofauti kwa kuwa ametupia nyavuni mabao mawili.

“Naweza kusema ninawafahamu kwani hii ni mara ya pili tangu tumekutana naifunga Al Hilal, lakini kwangu ni furaha na fahari kubwa kufunga mabao hayo kwenye mchezo wa dabi,” amesema Luvanga.

Mabao hayo yanamfanya Luvanga afikishe matano kwenye mechi nane akiwa kwenye 10 bora ya vinara wa ufungaji Saudia.

Ikiwa katika raundi ya nane Ligi ya Kuu ya Wanawake Saudia, watetezi hao wako kileleni na pointi 24 ikiwa timu ya kwanza ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa.

Desemba 27 Nassr itashuka Uwanja wa Prince Saud bin Jalawi kwenye mchezo wa raundi ya tisa dhidi ya Al Taraji iliyopo mkiani mwa msimamo ikiwa haijashinda mchezo wowote.

Related Posts