Eneo la soko Kurasini lauzwa kinyemela

Dar es Salaam. Soko la Kurasini lililopo Mtaa wa Shimo la Udongo, wilayani Temeke limeuzwa, mwananchi limefahamishwa.

Soko hilo lenye eneo la mita za mraba 400 awali ilikanushwa kuuzwa kwa mwekezaji na uongozi wa wafanyabiashara sokoni hapo.

Mwananchi limebaini vibanda vilivyokuwapo sokoni hapo vimebomolewa na kumezungushwa uzio wa mabati.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Jomary Satura, ameliambia Mwananchi amesikia taarifa za kuuzwa eneo la soko hilo.

Anasema baada ya kuona mwekezaji ameweka uzio wamebandika tangazo la zuio la kutofanyika shughuli zozote za uendelezaji, akieleza halmashauri haikushirikishwa.

Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa tangazo la zuio lilibanduliwa baada ya kubandikwa.

Mwananchi liliripoti kuhusu mpango wa kuuzwa soko hilo uliothibitishwa na katibu wa soko, Bendickson Bazale.

Wakati huo baadhi ya wafanyabiashara walilalamika kwamba hawakushirikishwa katika mchakato wa uuzaji ulioelezwa ulikuwa umekamilika, na kilichokuwa kikisubiriwa ni kuingizwa fedha kwenye akaunti ya soko ili wagawane.

“Fedha zimechelewa kwa sababu kuna mambo yamejitokeza yanayofanyiwa kazi na halmashauri, lakini kwa upande wetu tumemaliza kila kitu,” alisema katibu huyo.

Agosti Mosi, 2024 baada ya Mwananchi kuripoti taarifa hiyo, halmashauri kupitia kitengo cha mawasiliano ilitoa taarifa yenye kichwa cha habari ‘Ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa juu ya uuzwaji wa soko la Kurasini lililopo mtaa wa Shimo la Udongo.’

Katika taarifa hiyo ilisema: “Halmashauri imeshangazwa na taarifa iliyochapishwa na chombo cha habari ‘Mwananchi’ kupitia ukurasa wake wa Instagram ‘mwananchi official’ ikieleza kuwa viongozi wa soko la Kurasini lililopo Shimo la Udongo barabara ya GSM kuwa wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuuza soko hilo. Tunapenda kuufahamisha umma kwamba soko la Kurasini ni mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na siyo mali ya mtu au watu binafsi.

“Manispaa ya Temeke haijapokea ombi lolote kutoka kwa mtu, watu au taasisi yoyote kuhusu kuuziwa, kukodishwa au kupangishwa kwa soko hilo.

“Manispaa ya Temeke kupitia vikao vyake vya kisheria haijawahi kujadili wala kuidhinisha hoja juu ya kuuzwa soko la Kurasini,” ilielezwa kwenye taarifa hiyo.

Halmashauri katika taarifa hiyo iliwatoa wasiwasi wafanyabiashara na wananchi ikiwahimiza waendelee kupata mahitaji yao muhimu katika soko hilo na iwapo watapata changamoto yoyote watembelee ofisi za halmashauri kupata maelezo zaidi.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa akifanya shughuli za mama lishe sokoni hapo, Lucy Trax anasema waliitwa kulipwa fidia katika hoteli iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Anadai shughuli hiyo ilifanywa Agosti, 2024 na viongozi wao wa soko,  na yeye kwa kuwa alikuwa mpangaji alipata Sh500,000.

Anaeleza wengine ambao ni wamiliki wa vizimba, waanzilishi na wafanyabiashara wa zamani walilipwa kati ya Sh1.2 milioni hadi Sh3.6 milioni.

Akizungumzia namna walivyolipwa anadai walikuwa wakipigiwa simu kwa awamu kwenda hotelini na kwamba malipo yalichukua siku mbili kukamilika wakatangaziwa kubomoa vibanda na kuondoka.

Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Alice, anasema wamiliki wa vizimba walikuwa wakiwapa notisi wapangaji ya kuhama.

“Aliyekupangisha ameshakuambia uondoke anataka kuchukua mabati na mbao zake, wewe utang’ang’ania kukaa hapo unasubiri nini, hivyo licha ya hela ya fidia kuwa ndogo lakini ilibidi tuichukue kishingo upande,” anasema.

Alipotafutwa aliyekuwa katibu wa soko hilo, Bazale anasema kwa sasa hana mamlaka ya kuzungumzia eneo hilo kwa kuwa wameshaondoka.

Alipoulizwa iwapo wamemalizana na mwekezaji, hakutaka kujibu bali aliuliza, “kwani kuna mfanyabiashara yeyote Mwananchi imemsikia akilalamika kuhusu kuondoka sokoni hapo?.

“Kuhusu kuuzwa kwa soko hilo naomba ukaulize taasisi na mamlaka zinazohusika ikiwemo halmashauri kwa kuwa mimi kwa sasa sina mamlaka tena ya kuzungumzia eneo lile kwa kuwa siyo kiongozi tena na wala sipo pale.”

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Satura anasema eneo hilo ni mali ya halmashauri hiyo, lakini wafanyabiashara waling’ang’ania kuwa ni la kwao.

Sababu wao kufanya hivyo walieleza miaka ya kati ya 70 na 80 walihamishiwa hapo hivyo wanadai ni mali yao. Lakini ukiwauliza walilipa fidia au walinunua ukweli ni kwamba hakuna hata kimoja walichofanya.

Anasema kisheria serikali ya mtaa ikikupa eneo imefanya hivyo badala ya halmashauri kwa kuwa serikali za mitaa zipo chini yake, hivyo kwa namna yoyote wasingeweza kukwepa kuwa soko hilo ni mali ya halmashauri.

“Halmashauri ni muunganiko wa watu na mali zake kwa hivyo hata ikiwa katika ngazi ya mtaa au kijiji, hiyo ndiyo halmashauri na kilichofanywa ndiyo uwakilishi wa halmashauri.

‘Ndiyo maana hata kwenye ramani ya uendelezaji eneo la Kurasini bado soko hilo limetambuliwa uwepo wake,” anasema.

Anasema wakati wa uthamini wa uendelezaji wa bandari kavu katika eneo hilo ili watu wanaoishi hapo  walipwe fidia, eneo la soko halikufanyiwa uthamini kwa sababu ni mali ya halmashauri.

“Sasa kwa kutumia historia ya wafanyabiashara waliokuwepo hapo miaka ya nyuma, waka- lobby (shawishi) mtu kuwa ni mali yao binafsi ili walipwe fidia.

“Na nimesikia wamelipwa Sh300 milioni na watu waliojiorodhesha ni zaidi ya 70 wakaingiziwa fedha kwenye akaunti yao. Lakini ukweli ni kwamba mwekezaji akitaka kibali cha kupaendeleza ni lazima apitie halmashauri, hivyo nasi tukaweka pingamizi kwa waziri mwenye dhamani ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, tukipinga kuwa wale watu walikuwa ni watumiaji na siyo wamiliki.”

“Hivyo ndivyo tulivyozuia wizara isitoe umiliki kwa sababu sisi pamoja na kutoa huduma pia tunafanya shughuli za kiuchumi na kama ni suala la mtu kama anahitaji eneo aje aombe ridhaa kwetu, ili halmashauri iridhie kummilikisha au kumpangisha mtu mwingine,” anasema.

Anasema baada ya kuona mwekezaji aliyepanunua amezungushia uzio, ndipo watu wa halmashauri wakaenda kuweka zuio na kwamba, hadi sasa mwekezaji hajajitokeza kwao.

Alipoulizwa kama kuna hatua wanazowachukulia waliouza eneo hilo, anasema wameona wamzuie aliyetaka kupachukua kwa kuwa hayo mauzo kati yake na wafanyabiashara hawajahusika wala kushuhudia yakifanyika.

Related Posts