IOC yatoa tamko uchaguzi TOC

KAMATI ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) imetoa tamko la uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

IOC imeitaka TOC kufanya uchaguzi kabla ya Februari 28 mwakani, kinyume na hapo itajiingiza matatizoni.

Kwa mujibu wa taratibu za IOC, nchi wanachama zinapaswa kufanya uchaguzi ndani ya miezi sita baada ya michezo ya Olimpiki kumalizika, msimu huu michezo hiyo ilifikia tamati Agosti, 2024.

Awali, TOC ilipanga kufanya uchaguzi mkuu Desemba 28 kabla ya kufutwa katikati ya mchakato kwa kilichoelezwa na rais wake, Gulam Rashid kwamba walipokea barua kutoka kwa kaimu msajili wa vyama vya michezo Desemba 2, 2024 iliyoeleza kuufuta.

“Katika barua hiyo, kaimu msajili alidai mchakato wa uchaguzi ulianza kwa kutumia rasimu ya katiba ambayo ilikuwa haijapata ithibati ya msajili wa vyama na klabu za michezo,” alisema Gulam hivi karibuni.

Habari za ndani kutoka TOC zimeliambia Mwanaspoti kwamba, baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo uongozi wa Kamati ya Olimpiki ulikutana na Baraza la Michezo la Taifa katika kikao kilichofanyika wiki iliyopita kuweka mambo sawa.

Habari zaidi zilidai katika kikao hicho, kikubwa kilichojadiliwa ni katiba ya TOC ambayo upande wa Serikali ulitaka baadhi ya vipengele viboreshwe kabla ya kwenda kwenye uchaguzi ambao msajili alisema mchakato wake ulianza kabla ya katiba kuthibitishwa na msajili.

Inaelezwa, hitimisho la kikao hicho lilikuwa ni wanachama 39 wa TOC ndio wataamua hatma ya uchaguzi  kwenye mkutano mkuu wa wa kawaida Desemba 28.

Chanzo chetu kilikwenda mbali zaidi na kueleza kwamba wakati hayo yakiendelea,  tayari IOC imewaandikia barua TOC ikitaka hadi kufikia Februari 28, 2025 wawe wamefanya uchaguzi mkuu na kupata viongozi wapya.

“Kinyume na hapo itachukua hatua dhidi ya Tanzania,” kilisema chanzo kikibainisha kwamba, kwenye mkutano mkuu wa kawaida uongozi utalipeleka kwa wanachama ili waamue.

Itakumbukwa, wakati mchakato wa awali unafutwa, tayari wagombea 27 walikuwa wamejitosa kuwania uongozi ikiwamo wanne urais.

Wagombea hao ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Henry Tandau, Nasra Mohammed na Michael Washa huku nafasi ya makamu wa rais ikiwa na wagombe wawili wote kutoka Zanzibar na waliosalia wakichuana kuwania nafasi 10 za ujumbe.

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi hakukubali wala kukataa zaidi ya kusema kwamba kinachosubiriwa ni mkutano mkuu kuamua mbivu na mbichi za uchaguzi huo.

Related Posts