Kocha Serengeti afichua siri ya mafanikio

KOCHA wa timu ya taifa la Tanzania kwa vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’,  Aggrey Morris, amefichua siri ya mafanikio ya timu yake kufuzu kwa mashindano ya Afcon U17 2025, kwenye Kanda ya Cecafa baada ya kuifunga Sudan Kusini na kutinga fainali huko Uganda.

Tanzania na Uganda zimejihakikishia nafasi ya kuwakilisha Kanda ya Cecafa kwenye fainali hizo ambazo zitafanyika huko Morocco.

Kocha huyo alisema: “Nashukuru kwa juhudi kubwa za wachezaji wangu. Tumefanya kazi ya ziada katika mazoezi na kuwa na umoja mkubwa, jambo ambalo limezaa matunda. Kilichotufanya tufuzu ni nidhamu ya wachezaji wangu na maandalizi mazuri.”

Morris aliongeza kwa kusema, “ushindi huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya wachezaji, benchi la ufundi, na shirikisho letu la soka. Ni hatua kubwa kwa timu yetu, lakini hatuwezi kupumzika na kuona kama imemalizika kwa sababu tuna mchezo mmoja wa fainali, lengo ni kufuzu ila kuchukua ubingwa litakuwa jambo jema zaidi kwetu.”

Timu hizo mbili zilikata tiketi ya kufuzu baada ya kupata ushindi katika mechi za nusu fainali zilizochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Nakivubo Hamz, Kampala. Katika mchezo wa kwanza, Tanzania ilionyesha ufanisi mkubwa mbele ya Sudan Kusini. Ilianza kwa kasi ikiongoza 3-0 kwenye kipindi cha kwanza kupitia mabao ya Hussein Mbegu, Ng’habi Zamu na Abel Josiah Samson.

Baada ya mapumziko Sudan Kusini walijaribu kupigania kurudi kwenye mchezo, lakini walishindwa kumiliki mpira mbele ya wachezaji wa Tanzania. Juma Abushiri, aliyeingia kutokea benchi, alifunga bao la nne dakika ya 52 na kuifanya Tanzania kuongoza 4-0.

Sudan Kusini walipata penati dakika ya 67, lakini kipa wa Tanzania, Abrahman Massoro, alifanikiwa kuokoa mkwaju wa penati kutoka kwa Lazarus Peter George Laku, na hivyo kuzidi kuimarisha matumaini ya Tanzania kufuzu kwa Afcon.

Katika mechi ya pili, wenyeji Uganda waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Somalia.

Mechi ya fainali kati ya Tanzania na Uganda pamoja na mechi ya mashindi wa tatu na nne kati ya Sudan Kusini na Somalia zitachezwa Desemba 27, 2024.

Related Posts