Mchanja, Mfilipino kazi ipo KO ya Mama

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Yohana Mchanja na mpinzani wake Miel Farjado wa Ufilipino watakabiliana katika pambano la kimataifa la kuwania mkanda wa ubingwa wa WBO Global huku kila mmoja akitamba kumchakaza mpinzani wake.

Mabondia wamepima uzito leo katika Ufukwe wa Coco tayari kwa pambano hilo la Knockut ya Mama litakalofanyika kesho Alhamisi kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim.

Mara baada ya kupima Mchanja amesema amejipanga na amejiandaa vya kutosha kuhakikisha anabakisha mkanda wa ubingwa huo nchini ambao kwake utakuwa wa kwanza kupigania nchini katika daraja la kimataifa.

“Nimejiandaa vizuri kwa ajili ya KO ya Mama kesho. Najua ukubwa wa pambano na kile ambacho naenda kukifanya. Naomba Watanzania wanipe sapoti ya kutosha pamoja na dua zao ili niweze kuibuka na ushindi,” amesema.

Lakini, kwa upande wa mpinzani wake, Farjado amedai amekuja nchini kwa kazi ya kuhakikisha anaondoka na mkanda wa ubingwa huo mbele ya mpinzani wake.

Mabondia wengine watakaopanda ulingoni kesho ni Ibrahim Mafia ambaye atatetea mkanda wa ubingwa wa WBC Afrika dhidi ya Lusinzo Manzana wa Afrika Kusini, Said Chino atatetea mkanda wa ubingwa wa IBA International dhidi ya Malcolm Klassen wa Afrika Kusini sawa Kalolo Amiri ambaye atatetea ubingwa wa kimataifa wa PST dhidi ya Sihle wa Jelwana wa India ilhali Salmini Kasim atawania ubingwa wa IBF Intercontinental dhidi ya Adrian Lerasan wa Ufilipino.

Wengine watakaopigana ni Mfaume Mfaume na Paulus Amavila wa Namibia, Fadhili Majiha na John Zile wa  Ghana wakati Frank Shagembe na Asemahle Wellem wa Afrika Kusini, Said Bwanga vs Gurpreet Singh, Abbada Cadabra Ferooz atapigana na Latibu Muwonge, Joh Babai atazichapa na Manish wa India, Luckman Kimoko atapambana na Bismark Saah huku Leila Macho akifumuana na Agnes Mtimaukanena. 

Related Posts