Mtandao wa EFD kilio cha wafanyabishara Zanzibar

Unguja. Wakati wafanyabiashara wakieleza changamoto ya kukosekana mtandao kwa muda katika mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD), Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imesema zinaweza kutumika bila mtandao kwa saa kadhaa.

Hayo yameelezwa jana Jumanne, Desemba 24, 2024 wakati ZRA ilipowatembelea wafanyabiashara kusikiliza changamoto zao, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya furaha kwa walipakodi yanayofanyika Desemba kila mwaka.

Licha ya wafanyabiashara kueleza kwa sasa changamoto nyingi zimepungua kutoka kwa mamlaka hiyo, wamesema tatizo kubwa ni mashine hizo kukosa mtandao.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara, kuna wakati mteja hulazimika kusubiri ili kupatiwa risiti.

Mfanyabiashara wa vyombo vya umeme eneo la Mlandege, Salum Khamis Omar amesema wanakabiliwa na tatizo la mashine kugoma kwa wakati fulani, jambo linalosababisha malalamiko kutoka kwa wateja wanaolazimika kusubiri.

“Changamoto iliyopo ni mashine kukata network (mtandao) kwa hiyo unalazimika kusubiri, japo wateja wakati mwingine hawapendi kusubiri kwa muda mrefu,” amesema.

Changamoto kama hiyo pia imetolewa na mfanyabaishara Othman Nadir, anayesema mtandao kuna wakati hukatika hata kwa saa moja, hivyo huwalazimu kuwaeleza wateja waende kisha watarejea baada ya muda.

“Wateja wameshakuwa waelewa, hawapendi kuacha risiti kwa hiyo inakuwa shida kidogo,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Saleh Ashor Khamis ameeleza changamoto ya kodi inayotozwa kampuni akieleza ni kubwa, hivyo kuomba iangaliwe upya na kupunguzwa.

Amesema licha ya kupunguzwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 15, vivyo hivyo wapunguziwe na kodi kwa ajili ya kampuni.

“Tumehamasishwa kulipa kodi na tunapenda kutoa risiti, ila hii kodi ni kubwa mno kukatwa asilimia 30 bado inatuumiza, kwa hiyo tunaomba iangaliwe upya, ipunguzwe kama ilivyopunguzwa VAT kutoka asilimia 18 hadi 15,” amesema.

Amesema changamoto nyingine ni wanaponunua bidhaa Tanzania Bara wanalipa kodi ya asilimia 18, lakini Zanzibar wanalipa asilimia 15, hivyo ni vema kuangalia namna ya kuweka usawa.

Akijibu hoja za wafanyabiashara hao, Kamishna wa Mapato ya Ndani ZRA, Ali Adnan amesema hata mashine zikizima mtandao, bado zina uwezo wa kuendelea kufanya kazi kama kawaida na kutoa risiti.

“Hizi mashine zikizima mtandao zinaendelea kutoa risiti kama kawaida kikubwa ziwe na chaji,” amesema.

Hata hivyo, amesema iwapo mtandao ukikata, unaporejea wanatakiwa kujaza taarifa zote za mauzo kwenye mashine, wasiruhusu bidhaa yoyote kuuzwa bila kuingizwa kwenye mfumo, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za kodi. 

Kuhusu kununua bidhaa Tanzania Bara na kwenda kuuzwa Zanzibar katika makato ya mifumo miwili ya punguzo la asilimia 18 kwa 15, Kamisha Adnan amesema iwapo wakifuata taratibu zote zilizowekwa, wanaomba na kurejeshewa asilimia inayozidi.

“Ukifuata taratibu zote unaomba kisha unarejeshewa, kikubwa kufuata taratibu,” amesema.

Kuhusu punguzo la kodi ya kampuni, amesema hilo wamelichukua na watalifikisha katika ngazi husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi, zaidi kodi hiyo inakatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Related Posts