NIKWAMBIE MAMA: Mipaka ya utawala na dosari zake

Ngonjera, mabango, vitabu na historia nzima ya Tanzania imejaa sifa ya amani na utulivu. Zamani misafara ya wafanyabiashara, watafiti na wamisionari waliopita hapa, ilikuwa na kila sababu ya kuimezea mate nchi hii iliyojaaliwa bahari, mito, maziwa, milima na mabonde ya kuvutia. Kama vile haitoshi, ardhi yenye rutuba na madini pamoja na misitu iliyojaa wanyama wa kila aina vilizidi kuifanya nchi kuwa kama Paradiso.

Mbega aliponzwa na uzuri wake, hivyo utamu wa nchi hii ulimfanya kila mgeni aitamani kuwa mtoto wake. Wakoloni wenye nguvu walishindwa kujizuia, wakaamua kuivamia. Wakaitawala kwa mabavu, wakazipoka rasilimali zetu na kuwafanya wazee wetu watumwa wao.

Lakini wakati ulipofika wenye nchi tukaamka na kudai uhuru. Tofauti na wenzetu, sisi tulipata uhuru wetu kwa njia ya amani. Tangu tukio hilo la mwaka 1961 hatukuacha kuwaenzi wazee wetu na kuamini kuwa amani ni suluhisho la matatizo. Kwa silika za kibinadamu, hakuna maisha bila kugongana kimawazo au kwa namna nyingine. Hata hivyo, sisi hatukufikia hatua ya kutoana ngeu, na tuliyamaliza matatizo yetu kwa amani.

Nchi yetu ikawa kimbilio la wapigania uhuru wa bara zima la Afrika. Na ukweli ni kwamba hatungeweza kuwa huru wakati jirani na marafiki zetu wakiwa utumwani. Unapokuwa rafiki wa mnyonge nawe unageuka kuwa mnyonge, hivyo kwa pamoja inabidi mumng’oe mvamizi. Hii ililazimisha nchi yetu ya amani kuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa bara la Afrika

Ukiacha wenzetu waliokuwa bado kujikomboa kutoka kwenye makucha ya ukoloni, kulikuwa na waliokuwa huru, lakini wakagombana wenyewe kwa wenyewe. Nao walikimbilia huku kwenye utulivu kupata ahueni wakati nchi zao ziliponuka damu. Walipatiwa suluhisho na kurudi makwao. Hapo ndipo Tanzania ilipojulikana duniani kote kama “Kisiwa cha Amani”. Ilikuwa mfano wa pepo inayopokea viumbe walio matatizoni.

Lakini kama nilivyodokeza, silaha kubwa kwetu ilikuwa amani. Hapana mahala panapokosekana matatizo, lakini kwa kuwaenzi wahenga tuliyafuta mapungufu yetu kwa maridhiano. Changamoto ni sehemu ya maisha ya binadamu. Kama hisabati haziongopi na zinasema kuna hasi na chanya, hatuwezi kupata vyote bila kukosa vichache maishani. Kuna ukweli kwamba dawa ya moto ni moto, lakini sumu ya moto ni maji.

Hata hivyo, kuna usemi wa “Shibe mwana malevya”. Mtu anaweza kutafuta chakula kwa jasho jingi, lakini akishiba analewa na si ajabu akaipiga teke sahani yake ya chakula iliyomshibisha. Uswahilini kuna watu wanaofanya kazi za shuruba kutwa nzima, lakini wakilipwa huenda kuteketeza kipato chote kwa anasa, zikiwemo ulevi na uzinzi. Hawakumbuki adha waliyozipitia katika kupata fedha hizo. Hali hii ndiyo iliyoibuka Tanzania, ikajijenga na sasa imeota mizizi.

Tofauti na wazee wetu, hivi sasa tumeacha kutatua matatizo ila tunayazalisha. Tukiwa bado tunasumbuliwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, ni hivi juzi tu tumezalisha changamoto ya mipaka ya utawala kwenye mikoa, wilaya, kata na vitongoji. Jana usiku wenyeji waliingia vitandani wakiwa kwenye eneo lao walilolipatia jina la asili yao, asubuhi wanatangaziwa kuwa sasa wanasomeka kwenye kata au tarafa ya jirani.

Wachambuzi wa mambo wanaiona changamoto hii mpya kuwa imezalishwa ili kuleta utata wa kisiasa. Kwenye kipindi hiki tunapoelekea kwenye chaguzi, kila upande una mbinu zake za ushindi. Tatizo ni uhalali wa mbinu za wanasiasa. Pengine lawama zinakuja kwa sababu changamoto hizi hazikujitokeza kabla ya hekaheka za uandikishwaji wa wapigakura. Kutokana na hilo, baadhi ya wananchi wenye haki ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wametishia kususia zoezi hilo.

Dosari hii inaweza kuacha muhuri wa uchaguzi usio huru pamoja na kusimamiwa na chombo kinachojulikana kama “Tume Huru ya Uchaguzi”. Chini ya tume hii, baadhi ya vituo vimelalamikiwa kukiuka kanuni za uboreshaji na uadikishaji kwenye madaftari ya makazi na lile la wapigakura. Kule Chunya, Handeni na Pangani ni mifano hai ya jinsi wananchi walivyotishia kugomea zoezi la kujiandikisha wakilalamika vitongoji vyao kuhamishiwa kwenye majimbo mengine.

Inawezekana wananchi hawa wana fikra potofu. Lakini kama tatizo si la lazima, kwa nini lizalishwe? Na ni kwa nini iwe wakati huu? Kuna wakati tunaahirisha sherehe za nyumbani kupisha misiba ya jirani; hivyo iwapo ilikuwa ni lazima sana, Serikali ingeweza kusubiri uchaguzi upite ili kuepusha taharuki zinazoepukika. Mzozo wa kodi ya pango unaweza kuahirishwa kupisha msiba wa mpangaji.

Changamoto ya mipaka ya utawala inatokea wakati bado hatujasuluhisha migogoro ya mipaka tuliyonayo. Ieleweke kwamba hata kama ardhi ni kubwa na binadamu hajamiliki hata robo yake, maandiko yanasema tutagombania hata inchi moja ya ardhi iliyo halali. Haya yalianza zamani pale Wafaransa walipogombana na Wabelgiji, Waingereza wakafyatuana na Wajerumani na kadhalika.

Tanzania ilishatunishiana misuli kwenye mizozo ya mipaka dhidi ya Kenya na Malawi. Kama tunataka amani ya kweli, tushughulikie matatizo yaliyopo vitongojini badala ya kuanzisha changamoto ya mipaka ya utawala.

Related Posts