Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, akilenga kuunda kikosi imara cha kutekeleza malengo ya Serikali.
Kama ni mchezo wa soka, ungesema bado Rais Samia hajapata kikosi cha kwanza. Mwaka huu pekee, amefanya mabadiliko mara nne, hatua inayoonyesha juhudi zake za kuboresha uwajibikaji na utendaji wa viongozi katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Rais anayo mamlaka ya kuteua au kumuondoa waziri au naibu waziri kadri anavyoona inafaa.
Ametumia mamlaka hayo kuboresha utendaji wa Serikali, huku mabadiliko hayo yakihusishwa na haja ya kukabiliana na changamoto zilizopo na kuimarisha utekelezaji wa sera.
Wakati mabadiliko haya yakizua mjadala katika jamii na mitandao ya kijamii, wachambuzi wa masuala ya siasa wanatoa mitazamo tofauti kuhusu athari zake kwa utawala na utendaji wa Serikali.
Ni mtazamo wa jamii kwamba, mabadiliko hayo yanaimarisha uwajibikaji wa mawaziri katika sekta mbalimbali ili kukidhi matarajio ya wananchi kwa huduma bora.
Julai 2, 2024 Rais aliwahamisha wizara mawaziri mawili, alimteua Dk Selemani Jafo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Pia alimteua Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), awali alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Siku 19 baadaye, Julai 21, 2024, Rais Samia alifanya mabadiliko mengine akitengua uteuzi wa Nape Nnauye, January Makamba na Stephen Byabato.
Nape alikuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na January alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Byabato alikuwa naibu wa January.
Nafasi ya Nape ilichukuliwa na Jerry Silaa, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Nafasi ya Makamba ilichukuliwa na Balozi Mahmoud Kombo, ambaye aliteuliwa kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.
Dennis Londo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki akichukua nafasi ya Byabato.
Pia katika mabadiliko hayo, Rais alimteua Deogratius Ndejembi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Awali, Ndejembi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) nafasi ambayo ilichukuliwa na Ridhiwani Kikwete.
Kabla ya uteuzi huo, Ridhiwani alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mabadiliko hayo pia yalimwingiza Cosato Chumi aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Chumi alichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye ilielezwa angepangiwa kituo cha kazi.
Katika mabadiliko hayo, kuachwa kwa January na Nape kuliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.
January kuachwa kwake kulihusishwa na utendaji ndani ya wizara, huku Nape akihusishwa na kauli aliyoitoa Julai 15, 2024 akiwa mkoani Kagera.
Nape alionekana kwenye video iliyosambaa akisema: “Matokeo ya uchaguzi siyo lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe.”
Kauli hiyo ilizua mjadala mitandaoni, huku ikijitenga nayo, kuwa si msimamo wa chama hicho.
Mabadiliko kati ya Dk Jafo na Dk Kijaji yalihusishwa na mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo uliosambaa katika baadhi ya maeneo nchini, huku kukiwa na malalamiko kuhusu unayanyasaji katika ulipaji wa kodi.
Hicho ndio kipindi kilichomwondoa Angellah Kairuki, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye Baraza, akiteuliwa kuwa Mshauri wa Rais.
Siku 24 baadaye, Agosti 14, 2024 Rais Samia alifanya mabadiliko mengine yaliyoshuhudiwa yakiwarejesha kwenye Baraza la Mawaziri, Profesa Palamagamba Kabudi na William Lukuvi.
Profesa Kabudi aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi aliyowahi kuhudumu mwaka 2017-2019, huku Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), nafasi aliyowahi kuhudumu.
Profesa Kabudi na Lukuvi kwa pamoja waliachwa katika baraza jipya la mawaziri la Rais Samia lililotangazwa Januari 8, 2022.
Hata hivyo, Rais Samia Januari 10, 2022 akiwaapisha viongozi wateule, alieleza wawili hao watapangiwa kazi maalumu. Lukuvi wakati akichwa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Nina kaka zangu wawili, William Lukuvi na Palamagamba Kabudi ukiwatazama hao umri wao ni kama wangu na niliowateua hamfanani kabisa, kwa hiyo kaka zangu hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisimamie kuwasimamia ninyi kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye ile orodha hapo wote ni wadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri.
“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee na kazi hiyo, ila kazi yake kwa sababu haipo kwenye muundo haitangazwi, mashirika yote kazi zote zitakazoingia ubia na Serikali yeye ataongoza hiyo timu kwa hiyo yeye ni baba mikataba,” alisema Rais Samia.
“Kaka yangu Lukuvi yeye ana kazi na mimi mtaisikia baadaye lakini ninamvuta Ikulu kazi yetu ni kuwasimamia nyie, kwa sababu nikiwatazama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili, wengine mna safari ndefu mimi na wale tulishastaafu kwa hiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu.”
“Nimeona meseji nyingi wengine wanasema afadhali Lukuvi katoka, hajatoka yupo, wengine wameanza kumletea meseji za ajabu wakijua atagombania uspika, hatagombania ana kazi na mimi msianze kumchafua ametumikia Taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu muacheni aende na mimi tumalizie kazi atakayopangiwa,” alisema Rais Samia.
Ni katika mabadiliko hayo ya Agosti 14, uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ulitenguliwa na nafasi yake kujazwa na Jenista Mhagama aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).
Mbali ya uteuzi wa mawaziri na naibu mawaziri pia aliwahamisha wizara wengine.
Siku 116 baadaye, Desemba 8 Rais Samia amefanya mabadiliko mengine akihamisha majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Profesa Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku Jerry Silaa akiteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mabadiliko pia yamewagusa Dk Damas Ndumbaro ambaye anakuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Dk Kijaji safari hii ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, huku Innocent Bashungwa akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Mohamed Bakari akizungumza na Mwananchi kuhusu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni alisema:
“Kama ni mabadiliko yatakuwa madogo sana ya kiutendaji lakini hakuna mabadiliko ya mfumo, kama hakuna mabadiliko ya mfumo hatuwezi kutegemea mabadiliko ya uwajibikaji maana mfumo ni uleule na bado kuna kiwango kikubwa cha kutowajibika hata kwa wale wanaofanya makosa.” Ametoa mfano wa matukio ya watu kupotea na wengine kupatikana wameuawa akisema hayo yamechangiwa na uwajibikaji kushuka.
Dk Denis Muchunguzi, mchambuzi wa masuala ya siasa amesema mabadiliko yanayofanyika katika Baraza la Mawaziri yamekuwa na matokeo kulingana na mahitaji ya Rais.
“Tangu ameingia Ikulu Rais Samia amebadilisha viongozi kwa kiwango kikubwa na kumekuwa na matokeo, kila sekta aliyogusa kumeonekana tija, ameongeza wizara na zinafanya vizuri,” amesema.
Akizungumzia mabadiliko hayo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Loisulie amesema manufaa yake hutafsiriwa na kiongozi mkuu wa nchi mwenye mamlaka ya kufanya uteuzi na utenguzi wa viongozi aliowateua.
Amesema uteuzi na utenguzi faida yake ni kuwakumbusha watu kuwa uteuzi ni dhamana na anayepewa mamlaka anapaswa kuwa mnyenyekevu.
“Faida nyingine ni kuimarisha maeneo fulani ya kiutendaji, wale wanaoteuliwa na hakuna matokeo wanaondolewa wale wanaoletwa wapya wanaongeza nguvu, japo kuteua na kuondoa hakuleti utulivu kwenye utendaji, watu wanakosa uhakika wa kufanya kazi kwa uweledi,” amesema.
Hoja hiyo inaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya siasa Dk Richard Mbunda, anayesema yapo mambo hutokea kwa hamasa ya kisiasa.
“Mtu hafanyi kulingana na maelekezo ya mamlaka ya uteuzi sasa ukiangalia katika teuzi nyingi zilizofanyika zina mrengo mkubwa wa kisiasa kuliko utendaji, hivyo ni mara chache kuangalia utendaji, wapo waliofanya vizuri kwenye nafasi zao lakini waliondolewa,” amesema.
Dk Mbunda amesema ni ngumu kufanya tathmini ya matokeo ya utendaji ya wateule katika nafasi mbalimbali za uteuzi kutokana na kutodumu kwenye nafasi hizo.