Sikukuu ya Krismasi kwa mwaka huu imedondokea siku nzuri ya Jumatano. Hii ni makala ya Jumatano hii ya Krismasi.
Kwa mafundisho ya dini ya Kikristu tuliyopewa na huyu Masihi aliyezaliwa leo, Bwana wetu Yesu Kristu, aliulizwa amri kuu kuliko zote ni amri gani?
Yesu akajibu: “Mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote. Hii ni amri kuu ya kwanza, amri kuu ya pili inafanana na hii, mpende jirani yako kama nafsi yako.”
Na mimi naomba kuiongeza kidogo, upendo huo uwe ni upendo wa kweli na upendo wa dhati. Mpende Mungu, ipende nchi, wapende viongozi, mpende jirani yako kama nafsi yako. Akaulizwa tena, jirani ni nani? Ilifuata stori, nami nakuuliza wewe, je, unampenda jirani yako?
Japo Krismasi ni sikukuu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Masihi, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa sisi Wakristu, lakini sikukuu hii inaadhimishwa dunia nzima na watu wa dini zote na mataifa yote, hata nchi za Kiislamu, kwa kitu kinachoitwa Christmas Spirit is Giving, yaani dhima ya Krismasi ni kutoa, kujitoa, kukipelekea zawadi kichanga kilichozaliwa leo, lakini kwenye maisha yetu, siyo lazima kuwepo kichanga kilichozaliwa leo.
Hivyo, hiyo dhana ni ya kutoa kwa waliotuzunguka ukianzia kwenye familia yako, majirani waliokuzunguka, ndipo twende kwa ndugu, jamaa na marafiki hadi kwa wazazi wetu vijijini. Ni sikukuu ya kutoa na siyo sikukuu ya kupokea.
Tena ukitoa, toa kwa wote bila kujali ni dini gani, maana Krismasi ni sikukuu ya wote. Hata kwenye dini ya Kiislamu, wanamtambua Masihi, Bwana wetu Yesu Kristo, kama Nabii Issa Bin Maryam, ukisoma sifa za huyo Nabii Issa bin Maryam, utakubaliana na mimi mtu huyo ni Yesu Kristo, lakini kwa vile kila dini iko huru kuamini imani yake, kuna dini zinamkubali Yesu ndiye Nabii Issa, hivyo kuzaliwa kwake kunasherehekewa dunia nzima, ni sikukuu ya wote.
Hata simulizi za mwanzo wa ulimwengu kwa dini kuu mbili za Wakristo na Waislamu, sote tunakubaliana dunia iliumbwa na Mungu, mwanzo Mungu aliwaumba Adam na Eva (Kikristu) au Adam na Hawa, (Kiislamu), hivyo sisi binadamu wote ni watoto wa baba mmoja.
Adam, hata neno mwanadamu au binadamu, maana yake ni mwana wa Adamu au Bin Adam. Hata sisi nembo yetu ya Taifa yenye mwanamke na mwanamume, bibi na mwana, wale ni wazazi wetu, Adam na Hawa.
Kwa dini zote mbili kuu duniani, Wakristo na Waislamu, tunaamini kisa cha nabii Abraham (Kikristo) Ibrahimu, (Kiislamu) na mkewe Sara (Kikristu), Sarai (Kiislamu), waliishi muda mrefu kwenye ndoa yao bila kubahatika kupata mtoto.
Baada ya uzee kuwanyemelea na mkewe Sara siku zake kukoma, hivyo kutokuwa na uwezo tena wa kuzaa mtoto, ndipo akamtoa mjakazi wake wa Kimisri, Hagai (Kikristu), Hagir (Kiislamu), kushiriki na mumewe Ibrahim ili kupata mrithi.
Somo hapa ni familia ambazo hazikujaaliwa kupata watoto kutokana na tatizo la uzazi kwa mwanamke, wanawake msiwe wachoyo wa waume zenu kupata watoto! Ukijikuta wewe ni mwanamke, na una matatizo ya uzazi, huwezi kushika ujauzito na kuzaa mtoto, waruhusuni waume zenu kupata watoto kwa wanawake wengine.
Huu ndio upendo wa dhati. Hii ni endapo tatizo la uzazi ni kwa mwanamke, linapokuwa tatizo ni kwa mwanamume, hili mtanisamehe, bado sijajua utaratibu wake, kwa sababu hata kwenye vitabu vya dini, haijasemwa.
Huyo mjakazi akashika ujauzito, akamzaa mwana wa kwanza wa Ibrahimu akaitwa Ishmael (Kikristu) Ismail (Kiislamu), aliyemzaa na huyo mjakazi wake wa Kimisri. Familia nzima ilifurahi kupata mtoto, baba, mama na mjakazi.
Baadaye kwa muujiza wa Mungu, mke wa Ibrahimu, Sara, akiwa mzee wa umri wa miaka 80, alishika ujauzito na kumzaa mtoto aliyeitwa Isaka (Kikristu), Isihaka (Kiislamu). Ishmael ndio Baba wa Waislamu wote, na Isaka ndio baba wa Wakisto wote. Hivyo Wakristu na Waislamu ni watoto wa baba mmoja, Nabii Ibrahim. Ni katika ukoo huu ndipo alikuja kuzaliwa Nabii Musa, na aliyewakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri, na ndiye aliyepewa amri kuu za Mungu, ni zile zile amri alizopewa Musa, kupitia Torati, na hata Yesu alipokuja, bado amri za Mungu ni zilezile za Musa. Yesu hakuja kuitengua Torati bali alikuja kuikamilisha, hivyo Wakristu na Waislamu ni watoto wa baba mmoja, tusherehekee Krismasi pamoja.
Kwa vile Krismasi ni sikukuu ya kizungu, wenzetu wazungu wanaisherehekea kwa kitu kinachoitwa “The Christmas Spirit” ambacho ni kusherehekea by “Giving” and not “Receiving”, kumaanisha Krismasi ni sikukuu ya kutoa na sio kupokea.
Kuna Watanzania wengi wanajiandaa kwa mwaka mzima, ikiwemo kuweka akiba ya fedha za kutumia kula Krismasi na mwaka mpya, wanajikuta wanaisherehekea kinyume cha malengo, badala ya kutoa, wao ndio kwanza wanatumia kwa kujipenda, kufanya matumizi makubwa na sherehe, kula, kunywa, kusafiri, kustarehe, kununua vitu na kujipa zawadi wenyewe badala ya kuwapa zawadi wengine, hasa wahitaji. Amri kuu kuliko zote ni upendo, ukimpenda mtu kwa dhati, utamtakia heri, fanaka na mafanikio, natoa wito kwa sisi Watanzania, baada ya kumpenda Mungu, ni kumpenda jirani yako kama nafsi yako, jirani yako ni nani?
Kitaifa baada ya Mungu, nchi ndio jirani yako, tuipende nchi yetu, viongozi wetu ndio jirani zetu, tuwapende viongozi wetu, wananchi wengine wote ni jirani zetu, tupendane sisi kwa sisi kwa upendo wa dhati, viongozi pendaneni na wapendeni wenzenu hata wapinzani, ukiwa na upendo wa dhati toka moyoni mwako. Kwenye medani za siasa za vyama, CCM kama chama tawala, jirani zake ni Chadema, ACT Wazalendo, CUF, NCCR, wanaCCM wana wajibu wa kuwapenda vyama vingine kama wanavyojipenda wenyewe.
Nawatakia Krismasi njema.