Usiyojua kuhusu Buza kwa Mpalange, Mama Kibonge

Dar es Salaam. Majina ya Buza kwa Mama Kibonge, Kwa Lulenge na Kwa Mpalange si mageni jijini Dar es Salaam kutokana na umaarufu uliojizolea.

Umaarufu wake unakuja kutokana na waanzilishi wake, tafsiri hasi ya majina hayo sambamba na aina ya maisha wanayoishi wenyeji wa maeneo hayo yaliyomo katika Kata ya Buza, Wilaya ya Temeke.

 Ukienda Buza, hutaacha kuona namna wafanyabiashara ndogondogo walivyojipanga barabarani wakiuza supu za kongoro, samaki aina ya ‘dagaa mchele’, matunda, vyakula, vijiwe vya kahawa, wauza kachori kwa mchuzi wa pweza na vijiwe kadhaa vya bodaboda.

Baadhi ya wenyeji wanaeleza namna jina Kwa Mpalange lilipoanzia, huku baadhi yao wakichukizwa na kitendo cha baadhi ya watu kulipa tafsiri mbaya neno hilo.

Imeelezwa zamani eneo hilo kulikuwa na bonde lililokuwa likijaa tope kiasi cha kuwaletea changamoto wapita njia, kuteleza na wakati mwingine kuzama.

Akisimulia hilo, Adam Yusuph, mwenyeji wa Buza kwa Mpalange anasema walioanzisha eneo hilo ni watu wa kabila la Wandengereko walioishi hapo kuanzia miaka ya 1986.

Yusuph anasema kuna ukoo wa kina Mlanzi ndio waanzilishi wa eneo hilo lililokuwa na bonde ambalo kulikuwa na tope jingi ambalo watu walikuwa wakipita miguu inazama.

 “Barabara haikuwa nzuri, watu hata waliokuwa wakitembea kwa mguu walikuwa wakiteleza, hivyo umaarufu ukaanzia hapo,” anasema Yusuph.

Kuhusu jina Kwa Mpalange, simulizi zinaeleza kuwa Wandengereko, tope kwao wanaita mpalange, hivyo kwa changamoto hiyo ya tope, eneo hilo likapachikwa jina la Kwa Mpalange kwa maana ya eneo lenye tope.

Salum Mlanzi, mwenyeji wa eneo hilo kuanzia mwaka 1995 ambaye ni mtoto wa mzee Mlanzi aliyekuwa mmoja wa waanzilishi wa eneo hilo, anasema watu wanapaswa kuachana na tafsiri kwamba kwa Mpalange kuna biashara chafu za ufuska.

“Hakuna hivyo vitu huku na tunaomba Serikali iwachukulie hatua watu wanaopadharau na kupachafua huku na kuona kuna dada poa na madanguro.

“Kuna baadhi ya maeneo kuna watu wameenda mbali zaidi na kuandika matangazo ya mabango kwamba ukitupa taka hapa faini yako ni Kwa Mpalange, inasikitisha sana, ila nawashukuru waandishi wa habari kwa kutoa elimu.”

 Mwenyeji mwingine, Said Naeka, maarufu kama Said Masilinda au Mkongwe anasema kutokana na tope kuwa jingi waendesha bodaboda wakawa hawatamani kwenda eneo hilo wakiepuka kadhia ya kukwama.

Kuhusu umaarufu wa eneo hilo, anasema umetokana zaidi na hatua ya baadhi ya watu kuwa na tafsiri tofauti na maana ya tope.

“Huku hakuna wanawake wanaofanya baishara ya kuuza miili wala hakuna madanguro, lakini mtu unakuta anasema Kwa Mpalange kuna aina hiyo ya biashara, ninachotaka kusema hakuna hivi vitu huku,” anasimulia. Mkongwe huyo anasema Kwa Mpalange ni sehemu wanayoishi watu wenye heshima zao tofauti na picha iliyojengwa.

Akizungumzia urahisi wa maisha ya hapo, anasema kwa upande wa vyakula hakuna ubishi ukiwa na Sh1,000 unapata chakula cha kushiba kama alivyokutwa na Mwananchi  akila maharage chai na chapati kwa Sh1,000.

Mjukuu wa mama Kibonge, Rashid Mfaume au Mchina anasema kilichompa umaarufu bibi yake ni unene aliokuwa nao yeye pamoja na mume wake.

Mchina, ambaye ameanza kuishi eneo hilo mwaka 1989 anasema asili ya jina la mama Kibonge linaanzia kwa mumewe aliyekuwa akifanya kazi za hotelini mjini kwa Wahindi ambaye baadaye alipata unene. Anasema kutokana na unene wa mumewe ambaye alipewa jina hilo kazini, baadaye lilihamia kwa mkewe na kuanza kuitwa mama Kibonge.

“Bibi alikuwa mnene na babu naye alikuwa ana mwili, hivyo kutokana na kuwa nyumba ilikuwa barabarani, basi watu wakawa wanasema nishushe kwa mama Kibonge,” anasema mjukuu huyo.

 “Hadi barabara za lami zinakuja kuwekwa jina lilikuwa tayari limeshakuwa kubwa, magari yalikuwa yanaishia hapa kituoni ndio maana pakaitwa hivyo,” anaongeza.

Mwenyeji mwingine wa mama Kibonge anasema unene aliokuwa nao mama huyo ulimsababishia akawa anashinda nje, huku chakula na shughuli nyingine akizifanya hapohapo.

“Alikuwa mnene, akitoka asubuhi anashinda nje hadi jioni ananyanyuliwa anaingizwa ndani, alikuwa mnene sana,” anasimulia mwenyeji huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe.

 Wakazi wenyeji wa eneo la Buza kwa Lulenge wanasema jina hilo linatokana na mzee aliyekuwa anaitwa Ramadhan Lulenge aliyeishi hapo na kuwaachia urithi watoto wake.

Ramadhan Salum, mmoja wa wajukuu wa mzee huyo anasema baba yake aitwaye Salum Lulenge alianzisha duka kati ya mwaka 1998 na 1999 na daladala zilikuwa zikija hadi dukani.

 “Duka la vyakula la marehemu mzee likawa maarufu na kukawa kunaitwa dukani na daladala zikawa zinageuzia hapa, lakini baadaye walivyojua mwenye duka anaitwa Salum Lulenge, basi wakawa makonda wanasema shusha kwa Lulenge,” anabainisha.

Anasema daladala zikaongeza safari hadi mbele kunapoitwa Buza Kanisani, ambapo zamani kabla ya jina hilo palikuwa panaitwa Soweto, kabla ya kanisa kujengwa.

Anasema watu waliendelea kupaita kwa Lulenge hadi mji ulipozidi kuchangamka.

 “Baba yangu alizaliwa na wenzake wawili, hivyo walikuwa watatu, yeye akajiwekeza hapa sokoni ambapo sisi watoto tunapaendeleza,” anasema Ramadhan.

Related Posts