Vikundi saba vyawezeshwa kilimo cha mwani

Unguja. Ili kupata mwani bora, wakulima Zanzibar wamepewa mashine za kusagia na kukaushia zao hilo, hatua inayotajwa itaongeza uzalishaji, hususani kipindi cha mvua.

Vikundi saba vya ukulima wa mwani vya Unguja vimekabidhiwa kamba 120 na taitai 80 kwa kila kikundi. Pia kumetolewa kaushio la mwani moja na mashine ya kusagia yenye uwezo wa kusaga kilo 10 kwa saa.

Vifaa hivyo vimetolewa kupitia mradi wa Bahari Maisha ulioanza kwa majaribio, ukitarajia kuanza rasmi mwakani.

Mradi huo utadumu kwa miaka mitano ukifadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa kugawa vifaa hivyo mjini Unguja, jana Jumanne, Desemba 24, 2024 Ofisa Mkuu wa Uvuvi, Mohammed Soud amesema licha ya changamoto inayowakabili wajasiriamali wa mazao ya baharini kuhusu upatikanaji wa elimu ya ufugaji na ukulima wa mwani kisasa, Serikali inaendelea na jitihada za kuwawezesha.

“Mradi wa bahari maisha umekuja wakati muafaka kutokana na Zanzibar inatekeleza ya sera ya uchumi wa buluu kupitia bandari, utalii, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji, ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vya uchumi wa buluu nchini,” amesema.

Ofisa Mkuu wa Uvuvi Zanzibar akiwakabidhi wakulima wa mwani zana za kilimo hicho ili walime kwa tija katika mradi wa bahari maisha

Amesema mradi huo utasaidia uzalishaji wa mwani kutosheleza mahitaji ya kiwanda cha kuchakata zao hilo ambacho kinahitaji tani 30 kwa mwaka, mahitaji hayo bado hayajafikiwa.

Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Mwanza, Profesa Juvenal Nkonoki amewataka wakulima wa mwani kutumia vifaa walivyokabidhiwa kwa lengo lililokusudiwa.

Mratibu msaidizi wa mradi huo, Christopher Mdoe kutoka Chuo cha Mipango Mwanza, amesema mradi huu upo katika maeneo ya Tanga, Pemba, Unguja na Bagamoyo ambao umelenga kutatua changamoto za wakulima wa mwani na wafugaji wa mazao ya baharini, ili kuwakomboa kiuchumi.

Related Posts