Viongozi wa dini watoa angalizo uchaguzi mkuu 2025

Dar/Mikoani. Viongozi mbalimbali wa dini ya Kikristo nchini wametumia mkesha na sikukuu ya Krismasi kuiasa jamii ya Watanzania kuhusu mwelekeo wa uchaguzi mkuu mwakani, wakirejea yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.

Kwa nyakati tofauti katika mkesha wa Krismasi Desemba 24 na ibada za sikukuu hiyo Desemba 25, viongozi hao pia wamezungumzia matukio ya utekaji na umuhimu wa jamii kutenda mema, kudumisha amani na mshikamano.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa akihubiri leo Desemba 25, katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam amesema uchaguzi wa serikali za mitaa uligubikwa na viashiria vya uvunjifu wa amani, hivyo endapo hatua hazitachuliliwa dhidi ya vitendo alivyoviona, vitavuruga Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa kulikuwa na viashiria vingi ambavyo nimeviona kabisa vinaweza kuharibu amani kwenye uchaguzi ujao, ni lazima waombaji tuombe,” amesema.

Amesema ni muhimu wapigakura, wasimamizi wa uchaguzi na watia nia kuingia kwenye maombi kwani ili nchi iwe na amani ni lazima kumgeukia bwana wa amani.

Uchaguzi wa serikali za mitaa uliibua malalamiko kuhusu changamoto zilizojitokeza kuanzia uandikishaji wapigakura, uteuzi hadi utangazaji matokeo.

Waumini wa kanisa la St. Joseph wakiwa katika ibada ya mkesha wa Krismasi, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Maelfu ya wagombea wa upinzani walienguliwa kwa sababu mbalimbali, yakiwemo makosa madogo-madogo ya kukosea majina, herufi, anuani au kutokuwa na udhamini wa chama ngazi ya chini. Hata walipokata rufaa, wengi wao zilitupwa.

Pamoja na hayo , Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostenes amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu mwakani kwa kugombea nafasi mbalimbali, akiwaonya kutokubali kununuliwa haki zao na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.

Amesema nchi inahitaji viongozi wazalendo ili waongoze kwa kutanguliza mbele masilahi ya Taifa na si kwa kuzingatia matakwa yao.

Akisoma waraka wa askofu huyo kwa waumini kwenye ibada ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam, Kanoni Jacob Kahemele amesema kwa kutambua umuhimu wa kupata viongozi bora, ni lazima wananchi wahamasishane washiriki kikamilifu.

“Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Taifa letu,kwa ajili ya urais, wabunge na madiwani ni muhimu kuliombea Taifa livuke salama na uchaguzi ufanyike kwa amani na haki.

“Ni muhimu waumini kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kushiriki na miongoni mwetu mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali na kupiga kura. Tusipuuze na wala tusikubali kununuliwa haki zetu na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu,” amesema.

“Lazima tutambue masilahi ya Taifa ni muhimu zaidi kuliko itikadi au masilahi ya mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wachache, siasa njema ni muhimu,” amesema.

Pia amewataka Watanzania kuepuka siasa za chuki, ubinafsi na zinazolenga kuwagawanya kwa kuzingatia itikadi za udini na hata ukabila.

“Malumbano yenye kujenga chuki na yenye kuchochea fujo hayatufai katika kulinda amani ya nchi yetu. Tanzania ina thamani kubwa, ni muhimu kudumisha kwa kuwa na siasa safi na salama,” amesema na kuongeza kuwa uchaguzi ni jambo la msimu litapita lakini maisha ni jambo linalodumu wakati wote, vizazi kwa vizazi.

Naye amerejea uchaguzi wa serikali za mitaa akieleza ulikuwa na kasoro zinazotakiwa kufanyiwa kazi ili uchaguzi mkuu ufanyike kwa haki.

“Mwaka 2024 tulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa tunashukuru uliisha salama yamkini kulikuwa na changamoto zilizojitokeza ni muhimu kwa mamlaka zifanyie kazi kwa kuboresha ili uchaguzi mkuu unaokuja ufanyike katika mazingira mazuri,” amesema.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa Anglikana Achidikonary ya Kibaha, mkoani Pwani, Exavia Mpambichile yeye amewataka waumini kuombea uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza amani na utulivu katika uchaguzi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kwenye ibada ya mkesha kwenye Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Gabriel, Kibaha amesema: “Mwaka ujao tutashuhudia uchaguzi mkuu wa viongozi wa Serikali, ambao ni muhimu sana. Kwa hiyo, sote tunapaswa kuanza kuombea uchaguzi huu sasa, ili uwe wa amani.”

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao amesema kuna viashiria vya kutotenda haki licha ya watu kunyamaza, hivyo viongozi wana wajibu wa kuheshimu utawala wa sheria, kwa kuwa bila haki hakuna amani ya kweli.

Alihubiri katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph Minara Miwili, Zanzibar askofu huyo amegusia uchaguzi wa serikali za mitaa akisema yaliyofanyika hayaashirii mema mbeleni.

“Tunaona katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika kule bara, watu wanapata wasiwasi, je, katika uchaguzi mkuu ujao itakuwaje, watawala wana wajibu wa kutambua kuwa watu kunyamaza siyo kiashiria cha amani, mambo haya yanajenga chuki,” amesema.

Askofu Shao amesema: “Fimbo ya kutoa amani imeshikwa na wachache, lakini tusichoke kusema, sisi ndio mdomo, sisi ndio jicho katika kutoa haki.”

Amewakumbusha wananchi akisema: “Tunapaswa kuwaeleza viongozi wa juu kuheshimu utawala wa sheria na kuondoa chuki na vinyongo.”

Mwingine aliyezungumzia hilo ni Askofu wa Kanisa la FCG Zanzibar, Dk Charles Kiyengo katika ujumbe wake, amewasihi wananchi kuendelea kutunza amani, hususani katika kipindi ambacho Taifa linaelekea uchaguzi mkuu.

“Ujumbe wangu katika sikukuu hii, tunajua kwamba tunaelekea katika uchaguzi mkuu, tunahitaji amani, tuendelee kutunza amani, imekuwa ikiibuka migongano lakini hatuna budi kuwa kitu kimoja na kuwachagua viongozi ambao wataongoza Taifa hili.

 “Tujenge Taifa lenye hofu ya Mungu ili mataifa mengine yaje kuiga mfano kwetu, mtu akija Tanzania ajisikie kweli kuna amani,” amesema.

Askofu Malasusa akizungumzia matukio ya utekaji yanayoripotiwa nchini, amesema Watanzania wamepitia kipindi kigumu, akisema tangu azaliwe hajawahi kusikia watu wakitekwa.

“Ndugu zangu Watanzania tumepita katika kipindi kigumu, Mungu amekiondoa kipindi hicho. Tangu kuzaliwa kwangu sijawahi kusikia watu wakitekwa, lugha ya kutekwa inaleta hofu, hata mtu akikusogelea kukusalimia.

“Juzi (Desemba 23) alikuja askofu mmoja akanishika kwenye gari saa moja hivi, nikashtuka akaniambia shiii… nikamwambia vipi askofu,” amesema.

Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stephano Musomba.

Askofu Malasusa amesema kubwa sasa ni Watanzania kumuomba Mungu ili hali hiyo ikome.

Kuhusu hilo, Askofu Mkuu wa Kanisa la AGGCI, Asumwisye Mwaisabila amesema matukio ya aina hiyo yanawapa hofu hata wao kwa kuwa hayachagui mtu.

“Mtu anakamatwa hadharani, tena mchana watu wanaona, hii inatupa hata sisi hofu. Lazima tuzungumze kwani tofauti na hapo hata sisi tunaweza kutekwa, watekaji wote wasakwe wakachukuliwe hatua,” amesema.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yudathadeus Ruwa’ichi amewataka waamini kutumia sikukuu ya Krismasi kuziombea amani nchi zinazosumbuliwa na vita kama Sudan Kusini, Ukraine na Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, amewataka waamini wakati wakiomba amani nao wawe wajumbe wa amani, kweli, haki na upatanisho.

Amesema hayo kwenye mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.

“Katika kuadhimisha furaha ya tumaini jipya ni vyema kukumbuka kuwa Krismasi inapoadhimishwa ni sherehe ya amani lakini kwa bahati mbaya duniani kuna maeneo kadhaa ambayo yana majereha,” amesema.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Stephano Musomba katika misa ya mkesha iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro, amesema amani ndiyo chachu ya upatanishi miongoni mwa watu. Amesema kuliko kuhubiri ugomvi na chuki, ni vema watu watangaze amani katika ngazi zote.

“Palipo na amani, pana upendo na ushirikiano na hivyo panakuwa na upatanisho na uvumilivu baina ya sisi kwa sisi,” amesema.

Amesisitiza watu hawapaswi kununiana badala yake wawe na amani, kusameheana na kuvumiliana wakati wote.

Akihubiri leo Desemba 25, katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Denis Wigira amewataka waamini kuishi kwa mshikamano, kwa kujaliana na kuhurumiana.

“Ndugu zangu furaha inajidhihirisha katika mwonekano wa Mungu, kwa hiyo mtu unamuona anatabasamu, muulize kwa nini unatabasamu na kucheka majibu yake atakwambia kwa sababu nina furaha,” amesema.

Chediel Lwiza, msaidizi wa askofu wa KKKT akihubiri wakati wa mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Azania Front, amesema Wakristo wanatakiwa kutafakari na kutenda yaliyo mema ili kuyaweka maisha yao na Taifa lao katika nuru.

Amesema nuru huongoza maisha ya mtu, huleta furaha, amani na upendo na kwamba, Taifa lenye nuru hujawa mafanikio.

Mchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Center, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako, amesema kuzaliwa kwa Kristo kunaakisi maendeleo kwa wanadamu.

Akihubiri kwenye mkesha wa Krismasi kanisani hapo, Ubungo jijini Dar es Salaam, amesisitiza jamii kufanya kazi kwa bidii pamoja na kufanya maombi.

Amesema Yesu Kristo ni muasisi wa maendeleo duniani, akieleza kufurahishwa na waliojituma wakapata maendeleo ikiwemo umiliki wa nyumba au magari.

Askofu wa Jimbo la Morogoro la Kanisa Katoliki, Lazarus Msimbe amesema kutokana na watu kusonga mbele katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, binadamu amekuwa kiumbe anayerudi nyuma katika imani, akisahau maarifa anayopata yanatokana na uwepo wa muumba.

Amesema pamoja na maendeleo ya sayansi kanisa linaomba dunia iijalie imani thabiti kwani bila dini sayansi ni kiwete na sayansi bila dini ni kipofu.

Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa wa Kanisa la Inuka Uangaze, katika ibada ya Krismasi leo amewataka watu kusheherekea Krisimasi kiroho zaidi kuliko kimwili.

Mwamposa akihubiri katika ibada iliyofanyika Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam amesema kusheherekea kiroho kutamfanya mtu kuona matokeo zaidi ya kiroho na kimwili.

“Kwa bahati mbaya inachoonekana kwa sasa watu wamekimbilia kusheherekea sikukuu hiyo kimwili zaidi wakiangalia kuvaa nguo mpya, kula, kunywa na wengine kuzindua nyumba zao. Hii inanikumbusha zamani bila kuvaa nguo au viatu vipya haujasheherekea Krisimasi, tena zingine zinanunuliwa kuanzia mwezi wa 10.

“Hata mimi nakumbuka nilinunuliwa viatu, vikawa vidogo lakini nilikivaa vivyo hivyo mpaka kikajikunja na nikatembea kikiwa kimevimba mbele, lakini nilikivaa sababu ni Krisimasi,” amesema.

Krisantus Assenga, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu, Mirerani, wilayani Simanjiro amewataka vijana kujishughulisha na kazi halali ili wapate mahitaji yao.

Amesema vijana wanapaswa kujitambua wao ni kina nani, hivyo watumie fursa ya nguvu walizonazo kujipambania kimaisha.

Assenga amesema vijana wanapaswa kutambua Taifa na jamii kwa ujumla inawategemea, hivyo wajipange kufanya kazi kwa bidii.

Askofu wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel akitoa salamu za Krismasi katika Usharika wa Arusha Mjini, amesema wazazi na walezi wanapaswa kutumia vizuri vipato walivyonavyo na kutokufanya matanuzi ya sikukuu ili kuhakikisha Januari watoto wanapata mahitaji muhimu ya shule Januari 13, 2025.

Amesema wakati wa kusheherekea sikukuu ni muhimu kukumbuka jukumu la malezi na kuhakikisha watoto wanapata mahitaji ya muhimu na kuendelea na masomo.

“Kwa hiyo tule na tunywe tukikumbuka Januari 13, tusisahau kwani kabla hujaenda kwenye matumizi ya sikukuu tenga kwanza ada, hizo zinazokabaki kamalizie zote,” amesema.

Askofu wa kanisa hilo, Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema Yesu Kristo hahitaji msaada wa maji, chumvi wala udongo bali yeye anatosha.

Akihubiri wakati wa mkesha wa Krismasi katika Usharika wa Kayanga amesisitiza kuwa wokovu na ukombozi unapatikana kwa Yesu.

“Watu wanahangaika mara mafuta ya upako, mara chumvi, mara maji, mara vitambaa, mara nywele, mara nguo za ndani na nje, hayo yote ni mahangaiko kama walivyokuwa wana wa Israel lakini hawakuweza mpaka Yesu alipokuja kwa ajili ya kuokoa watu wake na dhambi zao,” amesema.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Full Gospel Bible Felloship, Hellen Kakobe amesema Wakristo wanapaswa kutambua Krismasi siyo kula, kupamba mapambo, kuvaa vizuri, kutembelea ndugu, kufanya uzizi, kunywa pombe na kukaa vibarazani kuongea maneno machafu, bali ni kutafakari neno na kufanya mambo yanayompendeza  Mungu.

“Kuzaliwa kwa Yesu kuna uhusiano upi na maisha yetu tunaangalia Mungu alikuwa na malengo yapi, hivyo binadamu tunatakiwa tubadilike, tumkiri ili atuongoze vizuri kwenda njia salama,” amesema.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya amewataka Wakristo kuchunga ndimi zao kwa sababu dunia imekuwa ikipata tabu kutokana na maneno ya uongo na ya ovyo.

“Dunia ingekuwa na amani zaidi kama kabla ya kutoa neno katika midomo yetu tungefikiri mara mbili. Mara ngapi tunakosana kwa sababu ya maneno ya ovyoovyo, mara ngapi familia zinakwenda mrama kwa sababu katokea mtu kaokota neno huko kalileta,” amehoji.

“Eti nimemkuta kasimamaa na fulani. Wanaanza kuvimbiana kumbe maneno ni ya uongo. Mara ngapi tumekosana kwa sababu ya maneno ya umbeya na ya kuokoteza. Maneno, mdomo unaumba,” amesema.

Salamu za Samia, Dk Mpango

Rais Samia Suluhu Haasan kupitia mtandao wa X (zamani twitter) amewatakia Watanzania kheri ya Krismasi akitaka isherehekewe kwa kujumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa furaha na upendo.

“Historia ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo itupe pia tafakari juu ya mwanzo mpya katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku, juu ya upendo kwa ndugu na jirani, juu ya uzalendo kwa Taifa letu, juu ya kuishi katika kweli, juu ya unyenyekevu tunapojaaliwa nafasi za kuwatumikia wenzetu, na juu ya shukrani. Tuungane pia kuiombea nchi yetu iendelee kudumu katika amani, umoja na utulivu,” amesema.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na mkewe Mbonimpaye Mpango walisali katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege, mkoani Dodoma.

Akitoa salamu za Krismasi leo, Dk Mpango amewasihi Watanzania kusheherekea kwa amani na utulivu pamoja na kujitoa kusaidia wale wasio na uwezo. Pia kutafakari juu ya malezi ya watoto majumbani kwa kuwaepusha na vitendo vya ukatili wanavyopitia.

“Ni vema kutafakari nafasi ya watoto katika Taifa kwa kuwapelekea tumaini, amani, upendo na furaha,” amesema.

Related Posts