Wakristo duniani washerehekea sikukuu ya Krismasi – DW – 25.12.2024

Wakristo duniani kote wanaadhimisha siku kuu ya Krismasi. Kulingana na imani ya Kikristo, Krismasi ni siku aliyozaliwa Yesu Kristo katika mji mtakatifu wa Bethlehem nchini Israel.

Wakristo wanaamini kuzaliwa kwa Yesu kuliwaletea ukombozi. Mamia ya watu walikusanyika katika kanisa la Uzawa katika mji mtakatifu kwa Wakristo wa Bethlehem Jumanne kuadhimisha Krismasi nyingine iliyogubikwa na vita katika Ukanda wa Gaza.

Vilivyokosekana kwa mwaka wa pili mfululizo ni pamoja na mapambo ya Krismasi, huku idadi ya wageni ikizidi kuwa ndogo ikilinganishwa na hapo zamani.

Bethlehem iliadhimisha Krismasi katika hali ya huzuni chini ya kivuli cha vita vinavyoendelea kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza. 

Katika Uwanja wa Manger, katikati ya mji huo wa Wapalestina unaojulikana kwa kanisa takatifu linaloaminika kuwa eneo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kundi la maskauti lilifanya maandamano madogo yaliyovunja ukimya wa asubuhi. 

Soma pia: Mashambulizi ya Israel yaua 100 katika mmoja ya usiku mbaya zaidi wa vita Gaza

“Watoto wetu wanataka kucheza na kucheka,” lilisomeka bango lililobebwa na mmoja wa skauti hao, huku wenzake wakipiga filimbi na kushangilia. 

Vita vya Gaza — eneo lililokatwa kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israeli — vilianza baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka jana. 

Shambulio hilo, lililosababisha maafa makubwa zaidi katika historia ya Israel, liliua watu 1,208, kulingana na takwimu rasmi za Israeli. 

Vita vya kiasi vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha vifo vya watu 45,338, kulingana na wizara ya afya ya eneo linaloendeshwa na Hamas, takwimu ambazo Umoja wa Mataifa unazichukulia kuwa za kuaminika. 

Maeneo ya Palestina 2024 | Maandamano ya Krismasi katika Kanisa la Kuzaliwa
Patriarki wa Kilatini wa Yerusalemu, Pierbattista Pizzaballa (katikati), akiongoza misa ya Krismasi katika Kanisa la Kuzaliwa mjini Bethlehem katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, tarehe 24 Desemba 2024.Picha: Hazem Bader/AFP

Kihistoria, Bethlehem huangazwa na mti mkubwa wa Krismasi katika Uwanja wa Manger, lakini kwa mwaka wa pili mfululizo, mamlaka za eneo hilo zilichagua kutoandaa sherehe kubwa. 

“Mwaka huu tumepunguza furaha yetu,” alisema Anton Salman, meya wa Bethlehemu, alipokuwa akizungumza na AFP. 

Maombi, pamoja na ibada maarufu ya usiku wa manane ya kanisa hilo, bado yatafanyika kwa uwepo wa Patriarki wa Kilatini wa Kanisa Katoliki, lakini sherehe zitakuwa za kidini zaidi. 

Licha ya hali ya huzuni, baadhi ya Wakristo katika eneo hilo takatifu – takriban 185,000 nchini Israel na 47,000 katika maeneo ya Palestina – walikuwa wakitafuta faraja katika maombi. 

“Krismasi ni sikukuu ya imani… Tutaomba na kumwomba Mungu aondoe mateso yetu,” alisema Salman. 

Katika ujumbe kwa Wakristo ulimwenguni kote, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliwashukuru kwa kuunga mkono mapambano ya Israel dhidi ya “nguvu za uovu.” 

“Mmekuwa upande wetu kwa uthabiti, wakati wote na kwa nguvu wakati Israel inatetea ustaarabu wetu dhidi ya unyama,” alisema. 

Matukio mengine ya Mashariki ya Kati 

Mahali pengine katika kanda ya Mashariki ya Kati, mamia ya watu walijitokeza mitaani katika maeneo ya Kikristo ya mji mkuu wa Syria kupinga uchomaji wa mti wa Krismasi. 

Tukio hilo lilitokea katika mji wenye Wakristo wengi wa Suqaylabiyah katikati mwa Syria, wiki mbili baada ya waasi wanaoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham kuongoza mapambano yaliomng’oa madarakani rais Bashar al-Assad. 

Kwa mujibu wa shirika la ufuatiliaji wa haki za binadamu la Syria la “Observatory for Human Rights”, wapiganaji waliouteketeza mti huo walikuwa wageni. 

Mmoja wa waandamanaji mjini Damascus aliyejitambulisha kama Georges aliambia AFP kwamba alikuwa akipinga “dhuluma dhidi ya Wakristo.” 

“Ikiwa hatutaruhusiwa kuishi imani yetu ya Kikristo katika nchi yetu, kama tulivyokuwa tukifanya zamani, basi hatustahili kuwa hapa tena,” alisema. 

Syria - Maandamano ya kupinga uchomaji wa Mti wa Krismasi.
Watu wakihudhuria maandamano kupinga uchomaji wa mti wa Krismasi huko Hama, Damascus, Syria, tarehe 24 Desemba 2024.Picha: REUTERS

Watawala wapya wa Syria wameahidi kulinda wachache wa kidini nchini humo, wakiwemo Wakristo. 

Lakini baadhi ya Wakristo wa Syria, wakiwemo wapinzani wa muda mrefu wa kisekula kwa utawala wa Assad, wana hofu kwamba itikadi ya Kiislamu ya uongozi mpya itamaanisha matarajio ya jamii yao na wachache wengine hayatazingatiwa katika mabadiliko hayo. 

Krismasi nchini Ujerumani

Nchini Ujerumani, Krismasi ilifunikwa na kivuli cha shambulio la maafa katika soko la Krismas, na kumfanya Rais Frank-Walter Steinmeier kutoa ujumbe wa uponyaji. 

“Chuki na vurugu hazipaswi kuwa na neno la mwisho. Tusikubali kugawanyika,” alisema. 

Papa Francis atasherehekea usiku wa Krismasi Jumanne kwa ibada maalum ya kuzindua Jubilee ya 2025, mwaka wa sherehe za Kikatoliki unaotarajiwa kuvutia zaidi ya mahujaji milioni 30 kwenda Roma. 

Kauli mbiu ya Jubilee ni “Mahujaji wa Matumaini,” na Papa Francis kutoka Argentina anatarajiwa kurudia wito wake wa amani katika dunia inayogawanyika kwa migogoro, hasa Mashariki ya Kati. 

Miongoni mwa makundi yaliyosajiliwa kushiriki katika Jubilee ni kikundi cha LGBTQ cha Kiitaliano La Tenda di Gionata, ikionyesha wito wa Papa kwa Kanisa kuwa wazi kwa wote. 

Ujerumani | Kampeni ya AfD Magdeburg
Watu wakiwa wamebeba mishumaa kwenye kampeni ya uchaguzi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD mbele ya kanisa kuu mjini Magdeburg.Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Baba Mtakatifu aunga mkono kuundwa kwa dola huru la Wapalestina

Bila shaka, kulikuwa na nyakati za furaha katika Krismasi, ambapo familia katika nchi nyingi ulimwenguni zilikusanyika kwa ajili ya milo na kugawana zawadi. 

Santa Claus ahakikishiwa usalama wake

Wakati desturi ya kila mwaka ya “kumfuatilia” Santa Claus ikianza, jenerali wa Jeshi la Anga la Marekani alisema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwamba matukio ya hivi karibuni ya droni zisizojulikana yanaweza kuathiri usafirishaji. 

Uhakikisho huo wa Jenerali Gregory Guillot ulikuja wakati ambapo Kamandi ya Ulinzi wa Anga ya Pamoja kati ya Marekani na Canada, NORAD ikiripoti kuwa Santa na Punda wake walikuwa wakitua kote barani Asia, ikiwa ni pamoja na Japani na Korea Kaskazini. 

“Bila shaka tunahofia kuhusu droni na vitu vingine angani” kamanda huyo wa NORAD Guillot alikimbia kituo cha Fox News. “Lakini sioni tatizo lolote la droni kwa Santa mwaka huu.” 

Shamrashamra za msimu wa likizo Berlin

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Na huko Paris, waumini walikusanyika katika kanisa kuu la Notre Dame kwa misa ya Krismasi ya kwanza tangu kufunguliwa tena kufuatia moto mkubwa wa mwaka 2019. 

“Tulifika hapa mapema kuhudhuria misa ya saa 10:00 jioni na kupata nafasi nzuri. Ni jengo zuri sana,” alisema Julien Violle, mhandisi mwenye umri wa miaka 40 aliyesafiri hadi Paris kutoka Uswisi akiwa na watoto wake wawili. 

Notre Dame ilifunguliwa rasmi tarehe 7 Desemba katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa dunia, akiwemo Rais Mteule wa Marekani Donald Trump. 

Chanzo: AFP

Related Posts