Yanga haipoi, yaendeleza moto Ligi Kuu

YANGA leo imeendeleza moto katika Ligi Kuu Bara baada ya kuifumua Dodoma Jiji kwa mabao 4-0, huku Prince Dube akiendelea alipoachia tangu alipoinasa ‘code’ ya mabao kwa kufikisha mechi ya nne mfululizo akifikisha mabao sita.

Dube alianza kufunga bao la kwanza dhidi yaTP Mazembe wakati aikiipa Yanga sare ya 1-1 ugenini kabla ya kufunga mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara na kumfanya afikishe matano akilingana na Clement Mzize ambaye leo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma alitakata kwa kufunga mabao mawili katkika mchezo huo.

Huo ulikuwa pia ni ushindi wa saba mfululizo wa Yanga kwa mechi za ugenini katika Ligi Kuu ya msimu huu, huku akifunga mabao 12 bila wenyewe kuruhusu bao lolote, lakiki ukiwa ni wa tisa kati ya 10 dhidi ya Dodoma tangu timu hiyo ilipopanda daraja mwaka 2020.

Matokeo ya leo yameifanya Yanga kufikisha pointi 36, moja pungufu na ilizonazo Siomba inayoongoza msimamo wa ligi hiyo kila moja ikicheza michezo 14 kwa sasa, lakini ukiwa ni ushindi wa 12 kwa kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Sead Ramovic.

Mzize aliyekuwa nyota wa mchezo huo ndiye alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 19 akimalizia mpira wa kona ya Pacome Zouzoua, likiwa la nne kwake msimu huu kabla ya kuongeza jingine dakika ya 38 akimalizia pasi tamu ya Mudathir na kumfanya afikishe matano kama aliyonayo Dube.

Dodoma iliyoanza langoni na kipa Mohammed Hussein ‘Mudi Kala’, ilishindwa kabisa kuhimili kasi ya Yanga iliyowaanzisha washambuliaji hao wawili (Dube na Mzize) mbali na viungo washambuliaji Mudathir Yahya, Pacome, Stephane Aziz Ki, aliyeifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 29.

Penalti hiyo iliyotokana na kipa Mudi Kala kuonekana kama amemuangusha Dube, japo marudio ya Azam TV ilionekana wazi hakuguswa, ila mshambuliaji huyo Mzimbabwe alipoteza balanzi mwenyewe kabla ya kuanguka.

Wakati Dodoma ikijiuliza imekuwaje ikajikuta inajitengenezea mazingira ya kupigwa bao la tatu baada ya beki na kipa wa timu hiyo kushindwa kumiliki mpira vizuri dakika ya 38 na Mzize kupokea pasi ya Mudathir na kufunga katika lango lililokuwa wazi baada ya Mudi Kala kuchelewa kurudi alipookoa mpira.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko kadhaa ambayo ni kama yaliipunguzia kasi timu hiyo, japo Dodoma iliendelea kucheza bila utulivu na Prince Dube akafanya yake kwa kufunga bao la nne dakika ya 63 akimalizia pasi ya Mudathir.

Hilo lilikuwa bao la tano katika ligi kupitia mechi tatu za Ligi Kuu, lakini likiwa la sita katika mechi nne ikiwamo moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza gundu lililokuwa likimuandama kwa kushindwa kufunga kwa muda mrefu kiasi cha kuonekana kukimbilia kanisani kufanyiwa maombi ambayo ni kama yamejibu kwa sasa.

Ushirikiano wa Dube na Mzize katika safu ya ushambuliaji ya Yanga imekuwa balaa kwani wawili hao wamefunga jumla ya mabao 10, kila mmoja akiwa na tano wakiwa ndio vinara wa timu hiyo, huku wakifuatiwa na Ibrahim Bacca mwenye manne, ilihali Maxi Nzengeli akiwa na matatu na Kennedy Musonda akiwa na mawili.

Licha ya Yanga kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo sambamba na mabao hayo manne lakini haijawaacha bure Dodoma baada ya kuwaachia fedha ndefu kufuatia uwanja huo kujaa mashabiki ambazo zitawafuta jasho wenyeji.

Ushindi huo wa leo utampa raha kocha Sead Ramovic ambaye sasa anafikisha mechi nne za Ligi Kuu akishinda mfululizo tangu alipoanza kuinyoa Namungo kwa mabao 2-0 ikiwa ugenini, kisha kushinda mbili za nyumbani dhidi ya Mashuja (3-2) na Tanzania Prisons (4-0) na huo wa leo ambao umeifanya Dodoma kushuka hadi nafasi ya 11 ikiwa na pointi 16, baada ya Namungo mapema mchana kushinda mabao 2-1 dhidi ya Fountain Gate itakayovaana na Yanga katika mechi ijayo ya ligi hiyo itakayopigwa Jumapili.

Katika mechi hiyo ya mapema, iliyopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara Namungo ilipata mabao yake kupitia kwa Pius Buswita na Geofrey Luzendaze, huku Salum Kihimbwa akiifungia wenyeji bao la kufutia machozi, ilihali Nicholas Gyan wa Fountain akikosa penalti baada ya kipa wa Namungo Jonathan Nahimana kuidaka.

Related Posts