Handeni. Ikiwa ni siku chache tangu wafariki dunia watu wanane, kutokana na ajali ya gari wilayani Handeni mkoani Tanga, jana usiku Desemba 25, 2024 wengine 11 wamefariki huku 13 wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha Coaster na Fuso wilayani humo.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amethibitisha kutokea ajali hiyo jana saa tatu usiku katika eneo la Kwenkwale, Kata ya Kitumbi, Wilaya ya Handeni.
Ametaja magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo kuwa ni gari aina ya Fuso iliyokuwa inatoka Lushoto kuelekea Dar es Salaam na basi dogo aina ya Coaster ya abiria iliyokuwa inatoka Mkata kwenda Tanga mjini.
“Watu 11 wamefariki dunia wakiwemo madereva wa magari yote mawili na majeruhi 13 walipelekwa kupata matibabu Hospitali ya Wilaya ya Handeni ambapo hali ya majeruhi tisa bado siyo nzuri na madaktari wanaendelea kuwahudumia,” amesema Msando.
Ameongeza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kutambuliwa na taratibu nyingine za kuanza kusafirishwa na ndugu zao.
Kuhusu chanzo cha ajali Msando amesema uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea na mamlaka husika zitatoa majibu watakapokamilisha uchunguzi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.