Ahoua apindua utawala wa Chama

Mashabiki wa Simba kwa sasa wanatembea vifua mbele kutokana na aina ya kikosi walicho nacho, huku wakiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 37.

Lakini, chama hilo pia linafanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika likishika nafasi ya tatu katika Kundi A, likiwa na pointi sita baada ya kucheza michezo mitatu wakiwa na matumaini ya kuvuka hatua hiyo kwenda robo fainali ambako sasa siyo habari mpya kwao, kwani wameshiriki mara tano kwenye mashindano ya kimataifa ya CAF.

Lakini, mashabiki hao wa Simba watafurahia zaidi wakisikia kwamba kiungo Jean Charles Ahoua ametumia mechi 14 tu kumfikia na kumuacha aliyekuwa kiungo fundi wa wekundu hao, Clatous Chama kwa namba za mabao na asisti ndani ya timu hiyo.

Msimu wa mwisho wa Chama akiwa na Simba kiungo huyo alifanikiwa kucheza mechi 23 akifunga mabao sita, akitengeneza asisti nne, akihusika kwenye ya mabao 10, kisha akatimkia zake Yanga msimu huu.

Baada ya hapo Simba ikamshusha Ahoua kuchukua nafasi yake ambapo kiungo huyo ndani ya mechi 14 amefunika namba hizo za Chama akifunga mabao saba, asisti sita akihusika kwenye mabao 11.

Ndani ya mabao hayo saba ya Ahoua amefunga mara tatu akitumia mashambulizi ya wazi, huku akiweka wavuni  penalti tatu na adhabu ndogo bao moja.

Chama katika mabao hayo alifunga penalti moja pekee na adhabu ndogo moja huku mabao mengine yakiwa kwa mashambulizi ya wazi.

Nyuma ya Ahoua yupo mshambuliaji Leonel Ateba aliyefunga mabao matano ambapo kati ya hayo ametupia wavuni penalti mbili huku akiwa hana asisti yoyote.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids akizungumzia namba hizo za Ahoua kwenye msimu wake wa kwanza amesema raia huyo wa Ivory Coast ameonyesha kiwango kizuri, lakini bado anahitaji kuongeza kasi ya kufanya vizuri zaidi.

Fadlu amesema Ahoua ananufaika na aina ya soka wanalocheza la kushambulia kwa nguvu ambapo kasi na akili yake ya kufanya uamuzi akiwa kwenye uso wa lango ni vitu vinavyombeba.

“Tunataka kucheza – timu icheze kwa kasi tukitengeneza mashambulizi mengi. Aina hii ya soka kama ukitulia unaweza kufunga zaidi. Ukiangalia Ahoua ana kasi na akili ya kufanya uamuzi akifika kwenye uso wa lango la wapinzani,” amesema Fadlu.

“(Ahoua) ni mchezaji mzuri na anafanya vizuri, lakini hizi takwimu  zinaweza kuwa bora zaidi kama atazidi kujituma.”

Related Posts