AKILI ZA KIJIWENI: Simkoko, Mwambusi na sasa Ahmad Ally

MIAKA ya 2000, mwanaume mmoja aliibuka akiwa na timu ya mkoani na kuzipasua kichwa timu mbili kongwe za Simba na Yanga na akafanikiwa kutwaa kombe la ligi mbele yao.

Ni kocha wa mpira, John Simkoko ambaye aliiongoza Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1999 na 2000 anabakia kuwa kocha wa mwisho tena mzawa kuipa timu ubingwa wa taji hilo ikitokea nje ya Dar es Salaam.

Na Simkoko alifanya hivyo akiwa na kikosi chenye wazawa tupu, kina Mecky Maxime, Kassim Mwabuda, Kassim Issa, Monja Liseki, Zuberi Katwila, Godfrey Kikumbizi, Abdallah Juma, Salhina Mjengwa na Abubakar Mkangwa.

Baada ya miaka kadhaa kupita, akaibuka kocha Juma Mwambusi na kikosi tishio cha Mbeya City ya Mbeya ambacho kikiwa na wachezaji kibao wazawa akazisumbua sana Yanga na Simba.

Ilikuwa Simba na Yanga zikikutana na Mbeya City ya Mwambusi ambayo ilikuwa na kina Deus Kaseke, Peter Mwalyanzi, Anthony Matogoro, Deo Julius, David Burhan, Paul Nonga, Saad Kipanga, Steven Mazanda na Mwigane Yeya zilikuwa na shughuli hasa.

Miaka kadhaa baada ya Mbeya City ile kupotea, sasa ameibuka kocha mwingine mzawa ambaye anaonekana kuwa na dalili za kuwa maumivu kwa hizo timu mbili kubwa nchini.

Kocha huyo ni Ahmad Ałły wa JKT Tanzania ambaye katika mechi mbili alizokutana na Yanga na Simba msimu huu ameziuliza maswali ya kutosha ambayo yamezilazimu timu hizo kutumia nguvu na akili kubwa kuzijibu.

Silaha kubwa ambayo Ahmad Ally amekuwa nayo ni uwezo wake wa kuzitazama timu pinzani na kuzifanyia tathmini kisha kuandaa mpango bora wa kukabiliana nazo jambo ambalo timu nyingi zinaonekana kulishindwa.

Ahmad Ally ameanza kutupa matumaini hapa kijiweni kwamba atakuwa mrithi mzuri wa baba zake waliozitesa Yanga na Simba ambao ni John Simkoko na Juma Mwambusi.

Related Posts