AKILI ZA KIJIWENI: Siri ya watoto wa Morogoro ni hii

VIJANA wa Morogoro hivi sasa wamezikamata Simba na Yanga kutokana na viwango bora wanavyovionyesha katika vikosi vya timu hizo ambavyo vimewawezesha kupata namba vikosini.

Katika kikosi cha Yanga kuna Dickson Job, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari, Abuutwalib Mshery na Jonas Mkude ambaye hata hivyo yeye amekuwa hapati nafasi ya kucheza ila amedumu sana kwenye kiwango chake.

Pale Simba watoto wawili wa Morogoro ni miongoni mwa wazawa wachache wanaotamba kikosini ambao ni beki Abdulrazack Hamza na winga Ladack Chasambi.

Hata hivyo, pale Simba kama ilivyo kwa Mkude kule Yanga, kuna kipa Aishi Manula ambaye amekuwa pia hapati nafasi ya kucheza lakini amedaka kwa ubora wa hali ya juu katika kikosi cha Simba na Taifa Stars kwa muda mrefu.

Sasa kwa muda mrefu hapa kijiweni tumekuwa tukitamani kujua siri ya mafanikio ni nini kwa watoto wa Morogoro hadi wamekuwa wakifanikiwa kupata nafasi ya kucheza na kudumu kwa muda mrefu kwenye klabu kubwa.

Uchunguzi wetu umebaini mambo matatu ambayo yanawabeba sana watoto wa Morgoro kwenye soka letu kulinganisha na vijana wa Dar es Salaam au mikoa mingine hapa nchini.

Jambo la kwanza, watoto wa Morogoro wanacheza kwa kujituma sana pindi wawapo mazoezini na kwenye mechi lakini jambo la pili linalowapa ulaji kwenye timu ni nidhamu kwa benchi la ufundi, viongozi na hata mashabiki.

Mchezaji mwenye nidhamu na anayejituma ni rahisi kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi ya kucheza na anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuteka hisia za wapenzi na mashabiki wa timu yake.

Jambo la tatu ambalo nadhani linawabeba watoto wa Morogoro ni wengi kutokuwa na mambo mengi ya nje ya uwanja ambayo mara nyingi ndio huchangia idadi kubwa ya wachezaji kushuka viwango.

Related Posts