Dar/ Mikoani. Wakati Watanzania wakiungana na Wakristo duniani kote kuadhimisha Sikukuu ya Krismasi hali ya amani imetawala nchini jana, huku tukio la mauaji ya mfugaji na mkazi wa Lubungo wa Mvomero mkoani Morogoro, Elisha Lengai (20) likitia doa.
Lengai anadaiwa kuchomwa kisu na Sikonye Kipondo (22) baada ya kutokea ugomvi ambao chanzo chake bado hakijafahamika.
Akithibitisha tukio hilo leo Desemba 26, 2024 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kijana huyo aliuawa jana Desemba 25, 2024 saa tatu asubuhi.
“Huyu marehemu, mtuhumiwa na vijana wengine walikuwa wamekaa mahali wakizungumza, ghafla ukazuka ugomvi kati ya vijana hawa wawili na kama inavyofahamika hawa wafugaji huwa wanatembea na visu na silaha nyingine.
“Hivyo, mtuhumiwa alichomoa kisu na kumchoma mwenzake sehemu ya nyonga karibu na kibofu na kusababisha kifo chake,” amesema kamanda Mkama.
Amesema baada ya kufanya mauaji hayo mtuhumiwa alikimbia, hivyo wanaendelea kumsaka ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Mpaka sasa hatujafahamu chanzo cha ugomvi uliopelekea (uliosababisha) mauaji hayo, hivyo polisi tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo,” amesema kamanda Mkama.
Wakati huohuo, askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo waliweka kambi maeneo yenye michezo ya watoto na starehe kwa lengo la kuimarisha usalama.
Kamanda wa jeshi hilo Mororgoro, Shabani Marugujo amesema ukaguzi huo ulianza Desemba 24 2024 na utaendelea hadi msimu huu wa siku kuu utakapomaliza.
Amesema lengo la kufanya ukaguzi huo ni kuwaweka salama watoto pamoja na wazazi wanaokwenda maeneo mbalimbali ya kumbi za starehe kusherekea Sikukuu ya Krismasi pamoja na mwaka mpya 2025.
Amewataka wananchi kutumia simu ya dharura ya 114 kwa msaada wa uokozi endapo wataona majanga mbalimbali.
Wauawa kwa kushambuliwa na mamba
Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, watu wawili wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa na mamba walipokuwa wakioga ndani ya Ziwa Victoria siku ya Krismasi.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Senyi Nganga amewataja watu hao alipozungumza na Mwananchi leo Desemba 26, kuwa pamoja na Sostenes Petro (58) anayetoka Kata ya Kasenyi, aliuawa na mamba jana Desemba 25, 2024 saa 11 jioni alipokwenda kuoga ziwani.
Amemtaja pia mtu aliyetambulika kwa jina moja la Msafari mkazi wa Kata ya Buhama Halmashauri ya Buchosa aliyeshambuliwa na mamba leo Desemba 26, 2024 saa 8.00 mchana katika eneo la Kambi ya Uvuvi ya mchangani alipokuwa akioga.
“Tumetoa elimu mara kwa mara juu watu kujikinga na madhara ya kushambuliwa na mamba wanapofanya shughuli za kibinadamu ndani ya Ziwa Victoria, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuchukuwa tahadhari,” amesema Ngaga.
Hadi sasa mabaki ya miili ya watu hao haijapatikana na wananchi wanaendelea kuwatafuta.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Buhama, Matias Mgasa ameseme ili matukio ya watu kushambuliwa na mamba yakome, Serikali haina budi kupeleka huduma ya maji ya bomba kwenye maeneo yote yaliko kandokando mwa Ziwa Victoria.
Askari aliyegongwa na gari kuzikwa
Mkoani Manyara, askari polisi wa Kituo cha Polisi Kibaya wilayani Kiteto, George Mwakambonjo (50) aliyefariki dunia kwa kugongwa na lori atazikwa Mjini Babati kesho Desemba 27.
Mwakambonjo alifariki dunia Desemba 24, 2024 aligongwa na gari aina ya Scania akiwa amepakizwa kwenye pikipiki ya kubebea abiria (bodaboda).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema Mwakambojo atazikwa Ijumaa ya Desemba 27 huko Babati.
Awali, akielezea ajali hiyo Kamanda Makarani amesema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori aina ya Scania lililokuwa nyuma ya pikipiki.
“Ajali ilitokea baada ya lori hilo lililokuwa nyuma ya pikipiki hiyo kuigonga na kusababisha kifo cha askari polisi huyo,” amesema kamanda Makarani.
Amesema baada ya ajali hiyo dereva wa lori alikimbia na dereva wa pikipiki (bodaboda) naye alikimbia.
Licha ya kuwapo matukio hayo, hali ya amani imetawala katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa sherehe za Krismasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema licha ya kutokuwepo kwa tukio la uhalifu katika maadhimisho hayo, lakini wanaendelea kuimarisha kuimarisha ulinzi kuelekea mwaka mpya.
Amesema sherehe za Krismasi wilaya za Bunda, Musoma, Serengeti na Butiama zimefanyika kwa amani na utulivu, huku akiwapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kutii sheria bila shuruti.
Jijini Mbeya, Jeshi la Polisi limesema Sikukuu ya Krimasi imesherehekewa kwa amani na salama kutokana na kutopokea taarifa yoyote ya uvunjifu wa amani.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 26, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema hadi leo Desemba 26 hawajapata taarifa ya tukio lenye viashria vya uvunjifu wa amani.
Amesema kwa kuwa sherehe inaendelea hadi leo, wanaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya mkoa kuhakikisha sherehe zinaisha kwa amani.
“Doria zimesaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuwa tuliweka askari maeneo mengi kulinda raia na mali zao, bado sherehe zinaendelea ila kwa jana hatujapata taarifa yoyote uvunjifu wa amani,” amesema Kuzaga.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewataka wananchi kuendelea kuzingatia maelezo yaliyotolewa na wataalamu wa usalama ikiwamo wapohitaji kuondoka nyumbani lazima abaki mtu.
Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro ametoa rai hiyo wakati akitoa tathimini ya hali ya usalama katika Sikukuu ya Krismasi.
Akizungumza na Mwananchi leo, Muliro amesema jana kulitokea tukio moja la moto eneo la ufukwe wa Coco na kudhibitiwa mapema na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
“Kwenye maeneo mengine ni salama, watu wamesherekea vizuri, walifanya ibada kwa utulivu isipokuwa kuna mambo machache yalijitokeza ikiwamo moto kuteketeza baadhi ya vibanda pale Coco Beach lakini ulidhibitiwa,” amesema kamanda Muliro.
Hata hivyo, ametoa tahadhari akisisitiza ni muhimu kwa wananchi kuzingatia nyumba inakuwa na mtu muda wote.
“Familia zinapoondoka zisiache nyumba yenyewe hii ni kwa ajili ya kudhibiti viashiria vyovyote vya kiusalama vinavyoweza kujitokeza kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na wamiliki wa baa kufuata sheria katika biashara zao.
“Watoto tusiwaache wakitembea wenyewe kwani wanaweza kupotea au kupata madhara mengine, wawapo baharini kama mtu hajawahi kuogelea asijaribu,”amesema kamanda Muliro
Imeandikwa na Beldina Nyakeke, Hamida Shariff, Tuzo Mapunda, Saddam Sadick, Joseph Lyimo na Imani Makongoro