Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limeishushia rungu klabu ya CS Sfaxien ya Tunisia ikiitoza faini na kuzuia mashabiki wa timu hiyo katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika.
CAF imeikuta na hatia Sfaxien kutokana na vurugu za mashabiki wa timu hiyo katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa nyumbani dhidi ya CS Constantine ya Algeria.
Mashabiki wa Sfaxien walifanya vurugu nyingi wakati wa mchezo huo uliopigwa Novemba 27, timu hiyo ikilala kwa bao 1-0 nyumbani ikiwa ni mechi ya kwanza ya michuano hiyo.
Sfaxien, pia imelimwa faini ya Dola 50,000 (Tsh 119 Milioni) kwa vurugu hizo, huku ikipewa adhabu ya kutakiwa kucheza mechi mbili zinazofuta za nyumbani bila mashabiki.
Adhabu hiyo itazilainishia Simba itakapokutana na Sfaxien mchezo utakaopigwa Januari 5, 2025 kisha ule wa Januari 19 itakapoikaribisha Bravos ikiwa ni wa mwisho kwao katika Kundi A.
Sfaxien haijashinda mechi yoyote katika kundi hilo baada ya kupoteza michezo mitatu ikishika mkia bila pointi yoyote.
CS Constantine kwa sasa ndio vinara ikiwa na pointi sita sawa na ilizonazo Simba na Bravo ya Angola, japo zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, Sfaxien bado inakabiliwa pia na adhabu nyingine sambamba na Simba kutokana na vurugu zilizotokea katika pambano baina yao lililopigwa Desemba 15 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wenyeji wakishinda 2-1.