Desemba ya ajali, wengine 20 wafa Rombo, Tanga

Handeni. Unaweza kusema Desemba hii ni ya majonzi na simanzi kubwa kutokana na mfululizo wa ajali mbaya zilizotokea, zikiwamo zilizotokea jana wilayani Handeni Mkoa wa Tanga na nyingine iliyotokea leo Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro ambazo zimesababisha vifo vya watu 20.

Mwezi huu ambao kwa kawaida huwa wa shamrashamra za sikukuu za mwisho wa mwaka, umegeuka kuwa wa machozi na huzuni kwa baadhi ya familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na ajali za barabarani.

Ajali hizo zinatajwa na Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa baadhi zimesababishwa na uzembe wa kibinadamu na nyingine ni ubovu wa magari.

Hata hivyo, mamlaka zinazohusika zimeendelea kusisitiza madereva kuendesha magari kwa kufuata sheria za usalama barabarani.

Desemba 24, 2024 watu wanane walifariki dunia na wengine kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori na basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Kijiji cha Michungwani, Kata ya Segera wilayani Handeni.

Kabla ya machungu ya ajali hiyo hayajatoka, jana ilitokea ajali nyingine iliyosabisha vifo vya watu 11, huku 14 wakijeruhiwa. Ajali ilihusisha gari aina ya Toyota Coaster na lori wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Desemba 26, 2024 amesema ajali hiyo ilitokea jana, saa tatu usiku eneo la Kwenkwale, Kata ya Kitumbi, Wilaya ya Handeni.

Amesema magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni lori aina ya Fuso lililokuwa likitoka Lushoto kuelekea Dar es Salaam na basi dogo aina ya Toyota Coaster la abiria lililokuwa ikitoka Mkata kwenda Tanga mjini.

“Watu 11 wamefariki dunia, wakiwamo madereva wa magari yote mawili na majeruhi 14 wamepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni kupata matibabu. Hali ya majeruhi tisa bado si nzuri, madaktari wanaendelea kuwahudumia,” amesema Msando.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao.

Kuhusu chanzo cha ajali, Msando amesema uchunguzi unaendelea na mamlaka husika zitatoa majibu zitakapokamilisha uchunguzi.

Majeruhi asimulia ilivyotokea

Shukuru Msisi, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, amesema mashimo yaliyopo barabarani ndiyo chanzo cha ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Shukuru, Coaster aliyokuwa akisafiria ilijaribu kupishana na lori la mizigo, huku madereva wote wakitaka kulikwepa shimo kubwa barabarani.

Amesema walipolikaribia shimo hilo, dereva wa lori pia alikuwa akikaribia na juhudi za kupishana hazikufanikiwa, hivyo magari hayo kugongana uso kwa uso.

“Dereva wetu aliingia kwenye lile shimo, huku akisoma dua ya ‘La Ilaha Illallah’, lakini gari likaelekea moja kwa moja kwenye Fuso. Nilishangaa kujikuta nikiwa chini,” amesema Shukuru.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, amesema ameliona shimo hilo, lakini akasisitiza huenda lisiwe chanzo pekee cha ajali hiyo.

“Dereva wa Coaster alionekana kulifuata moja kwa moja Fuso akijaribu kulikwepa shimo. Hata hivyo, shimo hilo halikuwa kubwa kiasi cha kusababisha ajali hii, lakini labda ilikuwa ni hatima yao,” amesema Balozi Batilda.

Kwa upande wake, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma, amesema ajali hiyo imehusisha gari T497 DZW, aina ya Nissan Civilian, lililokuwa likiendeshwa na Salim Abeid Almas (45), mkazi wa Tanga na liliingia upande wa kulia wa barabara na kugongana uso kwa uso na gari T707 EBZ, aina ya Mitsubishi Fuso, lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye bado hajafahamika.

Amewataja waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Nissan Civilian, Salim Abeid Almas (45) na abiria wengine 10 ambao bado hawajatambuliwa.

Kamanda huyo amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni kushindwa kwa dereva wa gari la Nissan Civilian kulimudu gari lake baada ya kuingia kwenye shimo barabarani, hali iliyomlazimu kuhamia upande wa kulia ambako aligongana na lori hilo.

Katika ajali nyingine iliyotokea leo, watu tisa wamefariki dunia papo hapo wilayani Rombo, Kilimanjaro baada ya gari dogo kugongana uso kwa uso na basi la abiria la Kampuni ya Ngassere.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo na kwamba majeruhi mmoja aliyebaki katika ajali hiyo amepelekwa Hospitali ya Huruma kwa matibabu zaidi.

“Kwenye Noah tumetoa miili tisa na yote tumeihifadhi Hospitali ya Karume na majeruhi amepelekwa Hospitali ya Huruma,” amesema.

Mwangwala amesema chanzo cha ajali ni baada ya gari aina ya Noah iliyokuwa ikitokea Tarakea kulipita lori na kwenda kugongana uso kwa uso na basi la Ngassere lililokuwa likitokea Dodoma kwenda wilayani humo.

Kauli ya ‘Desemba ya ajali’ inakuja baada ya mfululizo wa ajali zilizoondoa uhai wa watu, huku wengine wakijeruhiwa.

Desemba 3, 2024 watu saba walifariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu, wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Desemba 6, 2024 wabunge 16, maofisa wawili wa Bunge na dereva wa basi la kampuni ya Shabiby, walijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Mbande, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye michezo ya Afrika Mashariki, Mombasa nchini Kenya, kugongana na lori lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Dodoma.

Desemba 18, 2024 watu 15 walifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Mikese mkoani Morogoro. Katika Ajali hiyo, gari aina Toyota Coaster liligongana na lori.

Desemba 20, 2024 abiria 44 wa basi la kampuni ya usafirishaji ya Kisire walijeruhiwa baada ya basi hilo kupata ajali iliyosababishwa na dereva alipojaribu kulipita gari la kampuni ya George Town bila kuchukua tahadhari katika eneo la Magu, mkoani Mwanza.

Pia, Desemba 20, 2024 watu sita wa familia moja waliokuwa wakisafiri na gari aina ya Toyota Harrier walinusurika kifo baada ya gari hilo kupinduka kwa kuacha njia na kuingia kwenye mtaro eneo la Kizumbi, katika Manispaa ya Shinyanga.

Ajali nyingine ni ile iliyokatisha uhai wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko na binti yake, Maureen Nnko na kujeruhi wanafamilia wanne, akiwemo mke na watoto watatu wa Nnko. Ajali hiyo illitokea Desemba 22, 2024.

Related Posts