KAMA kuna kitu ambacho kinafanywa na Simba katika Ligi Kuu Bara, basi ni mateso makubwa kwa timu pinzania inazokutana nazo, ikiwa imeshafumania nyavu za timu pinzani mara 29 katika michezo 14 iliyocheza.
Lakini kama hiyo haitoshi imeruhusu mabao matatu tu kuingia katika nyavu zake, huku ikirejesha pira ililokuwa ikianza kurejea taratibu kucheza kama enzi zile za ubora wake misimu michache iliyopita ilipokuwa moto wa kuotea mbali kwa timu za ndani na nje ya nchi.
Nyuma ya hayo yote, kocha wa kikosi hicho, Fadlu David ni kama anataka kukomoa baada ya kusema kinachoendelea kufanywa na timu hiyo bado kabisa, huku akiweka bayana kuwa roho ya upambanaji ndio nguzo kuu ya mafanikio ya kikosi hicho.
Fadlu alisema kwa Simba ya sasa hata kama itakuwa nyuma kwa mabao 2-0, bado inaweza kupambana kurudisha na kinachofanyika ni mwanzo mzuri, kwani bado anaendelea kutengeneza kikosi cha ushindani.
Simba kwa sasa inaongoza kwa pointi 37 katika Ligi Kuu baada ya mechi 14, huku Fadlu akisisitiza mchezaji asiye na roho ya kupambana hatakuwa na nafasi kwenye kikosi hicho ikitokana na imani na mahitaji ya timu.
“Kwa kweli niwapongeze wachezaji. Tumefanya kazi ya ziada dhidi ya JKT Tanzania tukapambana kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, na licha ya kuwa na nafasi nyingi za kufunga kipa wa wapinzani alikuwa makini. Hii ni roho tunayoijenga na tunahitaji mashabiki waendelee kutusapoti,” amesema Fadlu.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto za michezo ya kimataifa, Simba inaendelea kutafuta ushindi kwa kila hatua akisisitiza kwamba timu itabaki imara kupigania alama tatu kila mara na haijaridhika ilipo kwani mambo bado kabisa Msimbazi.
Simba ilionyesha roho ya upambanaji pia katika mchezo wa ligi dhidi ya Mashujaa ambapo walipata bao la dakika za jioni ambalo lilifungwa na Steven Mukwala sekunde chache kabla ya mchezo huo kumalizika.
Mazingira ya namna hiyo pia yalijitokeza katika mchezo wa wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CS Sfaxien kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Kwa upande wa kiungo mshambuliaji chipukizi, Ladack Chasambi, amesema timu iko katika hali nzuri na kwamba wanapigania kwa kila sekunde na kuhusu msimamo wa Fadlu juu ya kupambana hadi mwisho.
“Kocha anataka kuona kila mchezaji akipambana mpaka dakika ya mwisho. Hii ni roho yetu. Hatutakubali kushindwa, hata kama tunaonekana kushindwa hadi. Tumefanya kazi ya ziada katika kila mchezo, na tunajua tutafanikiwa kwa kuendelea kupigana,” amesema.
Ladack aliongeza kuwa licha ya kupata changamoto nyingi kutoka kwa wapinzani, hasa mechi CS Sfaxien, morali ya timu ilikuwa juu na walijua lazima wafanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo.
“Mechi dhidi ya CS Sfaxien ilikuwa ngumu sana, lakini tulijua tunahitaji kupambana hadi mwishoni. Hii ni roho ya Simba, hiyo ndiyo tunayoijenga kwa sasa. Mashabiki wetu wanahitaji kutuamini, tutasonga mbele,” amesema.
Naye Valentino Mashaka ambaye alipata nafasi katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya JKT Tanzania, amesema: “Ni kweli tunapambana kila dakika, lakini hii si kazi ya mtu mmoja. Kila mchezaji ana jukumu lake.”
HESABU KWA SINGIDA BS
Baada ya kumalizana na JKT Tanzania ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Charles Jean Ahoua, kocha Fadlu anasema kwa sasa hesabu zimehamia kwa Singida Black Stars, mechi itakayopigwa Desemba 28.
Simba itakuwa na kibarua kigumu katika mchezo huo kutokana na kiwango cha Singida Black Stars ambao nao wanahitaji kumaliza msimu wakiwa katika nafasi nne za juu. Singida inajivunia kuwa mastaa mbalimbali kwenye kikosi chao wenye uwezo wa kufanya kitu kwenye mechi kubwa kama vile Elvis Rupia, kinara wa mabao akiwa na manane.