Dar es Salaam. Baada ya Sikukuu ya Krismasi, kipindi kinachotajwa kuwa cha matumizi makubwa ni Januari.
Bado siku tano kuingia Januari Mosi, mwezi unaofahamika na wengi kama wenye changamoto za ukosefu wa pesa.
Baadhi ya watu wanasema, changamoto za Januari huchochewa na watu kufanya matumizi mengi kipindi cha mwezi Desemba na kupelekea wengine kuwa kwenye madeni.
“Ni kipindi ambacho pia wengi wetu tunalipa kodi za nyumba na ada za shule, usipokuwa makini unaweza kuona mwezi Januari kuwa mgumu kuliko yote,” amesema Denis James.
Anitha John amesema, wengi wanaichukulia Januari kama mwezi mgumu kutokana na aina ya maisha wanayotaka kuishi kinyume na kipato.
“Mshahara wa Januari ni uleule unaopokea miezi mingine kwa wafanya kazi, kipi kinakushinda kujipanga ili usitoke kwenye reli? amehoji.
Hata hivyo kwa Mohammed Juma ni tofauti kidogo, amesema kipindi cha Januari, ukiachana na sikukuu za mwisho wa mwaka, kinachoifanya iwe ngumu zaidi ni mshahara.
“Mshahara wa Desemba unalipwa Tarehe 18 au 20, hapo kunakuwa na siku kama 10 mbele ili mwezi huo uishe, kisha kuanza Januari ambayo ina siku 31, unakuwa na siku 40 za kusubiri mshahara.
“Kuna wale ambao Desemba ni kutumia tu, ikifika Januari 2, hata nauli ya kazini hana, kwa staili hii lazima uione Januari ya moto,” amesema Juma.
Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema Januari huonekana ndefu kwa wale ambao hawana mipango na hawakuweka akiba kwa ajili ya mwezi huo.
“Tunafahamu Januari ina ada, kodi na mambo mengine shule, ni kipindi ambacho wengi wanatoka kutumia pesa nyingi Desemba hadi robo tatu ya kipato chao, kwa mtu ambaye anategemea mshahara na hajajipanga, lazima Januari iwe ndefu,” amesema.
Amesema ili kuondoka kwenye changamoto hiyo, ni kuanza kuweka akiba kidogo kidogo kuanzia Januari ili ikifika Desemba uwe na akiba ya kutosha.
“Ikiwezekana inapofika robo ya mwisho ya mwaka kuanzia Oktoba, uanze kulipa kidogo kidogo ada ya Januari au kodi ya nyumba ili gharama hizo zisijirundike na kuwa za mwezi mmoja.
“Kuna watu, hata akipokea mshahara wa Januari, bado hautoshi kutokana na madeni aliyoingia Desemba, hivyo utaishia kulipa madeni lakini kama angekuwa amedunduliza kidogo kidogo na kulipa vile vitu vya muhimu kama kodi, ada na vingine mapema, wala asingeiona Januari ni ngumu,” amesema.
Amesema, unapokuwa kwenye vikundi vya kuweka na kukopa, navyo vinasaidia kuifanya Januari yako kuwa rahisi.
“Ukiwa mwanachama utakopeshwa na kulipa kidogo kidogo, hivyo ni kama unakuwa umelazimishwa kuweka akiba, lakini kama huna kikundi, hujaweka akiba, ndipo pale utaiona Januari ndefu na ngumu.
“Utaanza kuomba mwenye nyumba au shuleni wakuvumilie, jambo ambalo ni gumu kidogo, kwa kuwa masuala ya ada, au kodi na matumizi mengine ya shule ni mipango ya muda mrefu sio na ukizingatia hilo, Januari inakuwa rahisi,” amesema.
Akizungumzia kisaikolojia, Mchungaji Daniel Sendoro amesema fikra zilizojengeka za ugumu wa Januari huwa zinadhalishwa na mitazamo potofu.
“Mitazamo hii inadhalishwa na mambo makubwa mawili, kwanza ni kutokuwa na nidhamu ya fedha mwisho mwa mwaka na kutokuwa na mipango mahususi. Kama mtu una mipango, Januari huwa haina maana mbaya kwake kwa kuwa anajua utafikia mwezi huo ukiwa na nidhamu ya fedha,” amesema.
Amesema wengi inawajengea kuwa Januari ni mwezi mgumu kwa kuwa kisaikoloji ni kitu kinatajwa tajwa.
“Hata hivyo ili kuondoa fikra hizo na Januari kuwa ya kawaida kwako ni kuwa na mipango na kuishi ndani ya mipango hiyo,” anasema.