Kicheko asali ya Tanzania ikisafirishwa kwenda China

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema mazao ya nyuki ikiwemo asali kuanza kusafirishwa kuuzwa kwenye soko la nchini China ni fursa kwa wazalishaji wa bidhaa hiyo nchini.

Huku akiwashauri walina asali na wadau nchini kuzingatia kanuni na taratibu za kitaalamu ili kuzalisha bidhaa bora itakayosaidia kuongeza thamani na kuitangaza katika soko la dunia.

Akizungumza Dar es Salaam, katika hafla ya kuaga kundi la kwanza la asali ya Tanzania kabla ya kusafirishwa kwenda China na kampuni ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), Waziri Jafo amesema changamoto ya utafutaji soko kwa walina asali nchini inaenda kuisha.

“Historia inazidi kutengenezwa nchi yetu inauwezo wa kupanua masoko yake ya uuzaji wa asali nchini China, jambo hili litaleta tija katika utunzaji wa mazingira na wananchi watakuwa wanajishughulisha na uzalishaji wa asali na kutengeneza uchumi wao,” amesema.

Dk Jafo amewapongeza walina asali na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wanaosimamia misitu na EACLC kwa kufungua masoko kwa kuanza kusafirisha tani 10 yenye thamani ya Sh100 milioni kwani soko linaenda kupanuka.

Awali, Meneja wa Kampuni ya Tanzania Future Enterprises Company Limited, inayojihusisha na upakiaji asali, Jackson Mponela amesema kupatikana kwa kampuni hiyo na kupata soko la nje ya nchi nifaraja kwao.

 Mponela katika hizo tani 10 kampuni yao imechangia kiasi kukubwa zaidi ya tani tatu huku akieleza walikuwa na uwezo wa kuchangia kiwango kikubwa lakini walishindwa kwa sababu ya kukosa vifungashio.

“Tumezoea kutumia chupa za plastiki lakini wenzetu wanataka chupa za grasi naamini tunapaswa kujipanga zaidi ili kukamata soko la duniani hasa kwa mataifa makubwa,”amesema

Akimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Karim Solyambingu amesema uasili wa asali ya Tanzania ndio unaoipa ubora katika soko la kimataifa.

Amesema sifa na upekee wa asali ya Tanzania unatokana na uzalishwaji wake ambao hauhusishi mchanganyiko wa uchafu na kemikali za kwenye mashamba.

 “Hii inatokana na kuhimiza wafugaji wa nyuki wafuge mbali na maeneo yanayotumia viatilifu na kemikali za kupulizia dawa kwenye mazao.

Zaidi ya asilimia 90 ya wafugaji wanafuga nyuki kwenye misitu iliyo chini ya TFS na huko ni sehemu salama kwakuwa hakuna kemikali zozote,” amesema Solyambigu.

 Ameongeza kwamba kitendo cha kuuza asali China ni fursa kwa Watanzania kutokana na uhitaji wake sokoni na kiwango cha uzalishaji kilichopo.

“Hii iwe chachu kwani wanataka asali nyingi na kiwango kinachopatikana kichache, tunazalisha na sisi pia tunatumia kama kiungo na nje wanataka. Tunaendelea kutoa wito watanzania waendelee kuzalisha kwa wingi,” amesema Solyambingu.

Amebainisha kwamba Tanzania inauwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 100,000. “Tumetoa ofa kwa mtu yeyote ambaye anatamani kufuga nyuki na hana shamba wala eneo yeye aje TFS tutampa eneo afuge bure aje na mizinga tu,” ametoa taarifa hiyo.

Balozi wa China hapa Tanzania Chen Mingjian amesema kitendo cha kuuza asali nchini China ni hatua muhimu katika ushirikiano wa kibiashara, na kiuchumi kati ya China na Tanzania.

Amesema pia ni sehemu muhimu ya maendeleo ya hali ya juu ya urafiki wa China Tanzania katika nyanja za kiuchumi na kibiashara.

“Tanzania ni washirika wakubwa zaidi wa kibiashara barani Afrika kulingana na takwimu za Uchina mnamo 2023, kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili kilikuwa ni bilioni 8.78, dola za Kimarekani,” amebainisha.

Related Posts